Njia rahisi kutimiza malengo yako unapoanza mwaka mpya

December 27, 2024 2:51 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutumia fedha kwa nidhamu na kuzingatia bajeti.
  • Jenga utamaduni wa kuweka akiba kila unapopata fedha. 

Dar es Salaam. Desemba ya kila mwaka ni kipindi ambacho kinaambatana na shamrashamra mbalimbali za kusherehekea sikukuu za kumaliza mwaka na kuanza mwaka mwingine kama Krismasi na Mwaka Mpya.

Ni kipindi cha familia, ndugu, jamaa na marafiki hujumuika pamoja kufurahia kwa namna tofauti.

Sambamba na hayo mwisho wa mwaka ni kipindi cha mahesabu kwa baadhi ya watu. Ni muda ambao watu hufanya tathimini ya malengo ya mwaka mzima na kupanga mipango ya mwaka mpya.

Wakati baadhi wakiambatanisha furaha zao katika kusherehekea sikukuu kwa kutimiza malengo ya maendeleo waliyojiwekea walipoanza mwaka, wengine humaliza kwa kulalamika na kujilaumu kutokana na kushindwa kutimiza dhamira na malengo waliyojiwekea kwa mwaka huo. 

Watu wengi hujiwekea malengo pindi mwaka mpya unapoanza lakini ni watu wachache ambao hufikia malengo hayo mwisho wa mwaka. Hii ni kutokana na changamoto ya fedha kutimiza malengo husika. 

Wakati ukijiandaa kuingia mwaka 2025 usirudie makosa ya mwaka huu ya kushindwa kutimiza malengo yako kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Zipo njia mbalimbali unazoweza kuzitumia kujiwekea akiba kidogo kidogo ili ufanye kile ulichokipanga. 

Njia za asili na kisasa za kutunza fedha zimeendelea kuwa msingi mkubwa wa kujiwekea akiba, hasa kwa watu wenye kipato cha kawaida.

Kibubu ni njia ya uhifadhi wa fedha ambayo kwa kiasi fulani imesahaulika lakini unaweza kubadili maisha yako kupitia kibubu Picha | Kelvin Makwinya.

Katika mtaa wa Kisopwa barabarani, Mkoa wa Pwani,  Rufina Mrosso, mjasiriamali anayejishughulisha na uuzaji wa bidhaa za nyumbani anasema hutumia kibubu kama njia ya kuweka akiba ya fedha.

“Mimi nimekuwa nikitumia kibubu kwa muda mrefu tangu nikiwa mdogo, na kwa sasa kila siku natenga faida ya biashara yangu na kuweka humo na mwisho wa mwaka naweza kulipa kodi, kuongeza mtaji wa duka langu na kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii kama kuchangia inapotokea suala la sherehe au msiba” anasema Rufina, mama wa mtoto mmoja.

Mjasiriamali huyo anasema kuwa kwa mtu mwenye kipato cha kawaida kama yeye, kujiwekea akiba kwa malengo ni njia muhimu ya kujikwamua kimaisha na kutimiza kidogo kidogo mipango uliyojiwekea.

“Kwa kweli japo sio kwa ukubwa lakini nimepiga hatua sana, kupitia kibubu ndio nilipata mtaji wa kuweza ata kufungua kaduka kangu unakokaona hapo kwa sababu sina mume wa kusema atanipa mtaji. Mimi ni mwanamke ninayeendesha maisha yangu mimi mwenyewe, mwanangu amekua kupitia mia mia ninazojiwekea na hata sasa nakaribia kumaliza ujenzi wa nyumba uko nyumbani,” anaeleza Rufina. 

Kuweka akiba ya fedha kunasaidia kurahisisha shughuli za ujasiliamali pale unapokwama au kupungukiwa na mtaji Picha | Kelvin Makwinya.

Wakati Rufina akitunza fedha zake kwenye kibubu, mwenzake Edwin Tesha (26), dereva wa bajaji Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam hutumia upatu kama njia ya kuweza kujiwekea akiba ya fedha. Tesha alishawishika kujiwekea akiba kwa njia ya upatu kupitia rafiki zake.

Kupitia upatu, Tesha ameweza kujikimu na kuendesha maisha yake kwa kulipia gharama kama vile kodi, chakula, kununua vitu vya ndani na hata fedha za utengenezaji wa bajaji yake inapopata hitilafu ambayo pia ameinunua kupitia kuweka akiba.

“Kila siku tunachanga kiasi cha Sh 20,000, tupo jumla ya watu 144 na kila siku mtu anapokea kiasi cha Sh 2,800,000. Ni kiasi kikubwa sana cha pesa ambacho ukipata unaweza fanya jambo la kimaendeleo, tofauti na kukaa bure kupata kiasi kikubwa kama hicho inakuwa ni ngumu,” anasema Tesha.

Tesha anatoa ushauri kwa vijana wenzie kukumbuka kujiwekea akiba ya fedha mwaka ujao kwa njia ya upatu au zingine zinazofaa.

Anatoa angalizo kutokana na kuwepo kwa vitendo vya utapeli katika vikundi vya upatu huku akiweka wazi kwamba kikundi chao hakitumii mtu binafsi katika kuhifadhi pesa bali hutumia huduma ya M-Koba (huduma ya kuhifadhi pesa kwa vikundi kutoka mtandao wa Vodacom).

“Kikubwa katika kuweka akiba kupitia upatu ni uaminifu tu, kwa sababu kama utatumia mtu kuhifadhi pesa zenu unaweza kujikuta unatapeliwa, ni bora kutumia huduma ata zinazotolewa na mitandao ya simu, kwa mfano sisi tunatumia M-Koba kuhifadhi fedha zetu,” anaeleza kwa msisitizo.

Vijana wanaweza kutimiza malengo yao na kupiga hatua ya kimaendeleo kupitia kuweka akiba Picha | Kelvin Makwinya.

Ukiachana na kibubu na upatu pia kuna njia nyingine za kuweka akiba ya fedha kama vile kufungua akaunti ya benki, kuhifadhi pesa kupitia huduma za kifedha kutoka mitandao ya simu pamoja na vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana kama VICOBA.

Kwa nini akiba ya fedha?

Mtaalamu wa Masuala ya fedha na uchumi kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Abel Alfred Kinyondo anasema kuwa akiba kwa mtu binafsi kazi yake ni kurahisisha matumizi.

Hii ina maana kuwa katika nyakati ambazo mtu huwa na fedha za kutosha anaweza akatunza kidogo na katika nyakati ambazo mtu hukosa anaweza akarudi katika kile alichokitunza ili kujikwamua.

“Nyakati hazifanani, leo unaweza kupata Sh100,000 kesho Sh200,000 mara nyingine hupati kabisa na siku inayofuata ukapataSh50,000 na kadhalika,” anaeleza Profesa Kinyondo.

Akiba inaweza kutumika katika uwekezaji wa miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha. Mtu anaweza kuweka lengo ambalo linahitaji kiasi fulani cha pesa ila asiweze kupata mara moja, hivyo kuweka akiba ya fedha kidogo kidogo mtu huyo anaweza kufikia malengo yake kwa urahisi.

“Unaweza kusema unataka ujenge nyumba lakini huna fedha ya kujenga hiyo nyumba kwa wakati huo, hivyo utaanza kuweka akiba taratibu taratibu ili ukusanye kiasi husika kinachohitajika,” anaeleza Profesa Kinyondo.

Profesa Kinyondo ameweka wazi kuwa mtu anaweza kutumia njia yeyote kuweka akiba lakini jambo la muhimu ni kutambua kiwango chake cha matumizi kwa wakati husika.

Profesa Kinyondo anaeleza kuwa watu wengi hushindwa kuweka akiba ya fedha kwa sababu hutumia kadiri ya wanavyopata na hawana kiwango maalum cha matumizi ili kuweza kujua ni kiasi gani kinahitajika kutumia na kinachobaki kuhifadhi kama akiba.

“Ndiyo maana ripoti zinaonyesha hata watu wanaoshinda michezo ya bahati nasibu, hata wakishinda dola milioni 2 ama tatu baada ya muda wanakuwa masikini kwa sababu hawana kiwango maalumu kwa ajili ya matumizi yao na kingine wakaweka akiba,” anasema Profesa Kinyondo.

Nidhamu ni muhimu

Mhadhiri huyo wa chuo kikuu anasisitiza kuwa nidhamu ni nguzo kuu. 

“Huwezi kufanikisha malengo ya kifedha bila kujizuia kutumia fedha hovyo. Jiulize kila mara: Je, hili ni jambo muhimu?,” anashauri Profesa Kinyondo. 

Anaamini kuwa uelewa wa kifedha ni muhimu kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Wakati mwaka unakaribia kuisha, ni wazi kuwa kuna njia nyingi ambazo mtu anaweza kutumia kujijengea mustakabali wa kifedha ulioimara. Kila njia ina changamoto zake, lakini kwa nidhamu, mafunzo, na usaidizi kutoka kwa jamii na wataalamu, ndoto za kifedha zinaweza kutimia. 

Kujiwekea akiba leo kunaweza kuwa msingi wa maisha bora kesho. Anza mwaka 2025, kwa maazimio ya kujenga tabia ya kuweka akiba hata kama ni ndogo ili kufikia malengo yako uliyojiwekea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks