Unataka kufahamu ukomo wa huruma yako? Tazama filamu ya “1917”
Misheni hiyo inabaki kwenye mikono ya Schofield ambaye anamtazama Tom aliyekuwa shujaa wake awali akikata roho polepole. Picha| Flipboard.
- Ni filamu inayosimilia hatma ya wanajeshi 1,600 wanaoenda vitani lakini wanaangukia katika mtego wa kifo.
- Jukumu la kuzuia vifo hivyo, linakabidhiwa kwa mwanajeshi ambaye kaka yake yupo kwenye hati hati ya kuuwawa.
- Filamu hii itakufundisha umuhimu wa kufurahia kila sekunde maishani mwako na kikomo cha huruma yako.
Dar es Salaam. Hatimaye ijumaa ya mwisho wa mwezi wa Januari imewadia na ni dhahiri kuwa unashusha pumzi baada ya mambo mengi yaliyotokea mwezi huu ikiwemo mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii.
Ndiyo, una sababu ya kufurahi kama hujalizwa na “Hamida” wako mwezi huu. Sababu inaendelea kuwa kubwa zaidi kama unatembea mtaani bila kuvaa vitu vya kufunika uso hivyo kuwa na kila haja ya wewe kuendelea kufurahia kila dakika na sekunde inayokuja mbele yako.
Unaonaje ukitupa kule mawazo yako na kufurahia ulimwengu wa filamu kwa kutazama filamu zinazoonyeshwa kwa mara ya kwanza kwenye kumbi mbalimbali za kuangalizia filamu nchini zikiwemo za Century Cinemax?
Kama bado haujaelewa nini kilitokea mwaka 1917, siyo makosa yangu somo la historia lilikupita wakati likielezea vita ya kwanza ya dunia lakini itakuwa ni kosa kama sitakujuza juu ya filamu hii mpya ya “1917”.
Anzia hapa. Endapo ujumbe wa kuahirisha mashambulzi hautafika kwa wakati, wanajeshi 1,600 wanakwenda kuuawa akiwemo Luteni Joseph Blake.
Kufikisha ujumbe huo, Jenerali Erinmore anamtuma Kopro Will Schofield na Tom blake, mdogo wa Luteni Joseph Blake kumjulisha kiongozi wa kikosi, Colonel Mackenzie juu ya kuahirisha oparesheni hiyo ambayo ilikuwa inawakutanisha wote na malaika mtoa roho.
Zinazohusiana
- The Informer: Filamu ya mwisho kuitazama Januari 2020
- Furahia wikiendi yako na filamu ya daktari anayeongea na wanyama
- Filamu ya “Bad Boys for Life” kuwarudisha Smith na Lawrence ulingoni
Akiwa na hofu ya kumpoteza kaka yake, Tom analazimika kuvuka kila kiitwacho kikwazo ili aokoe maisha ya maelfu ya wanajeshi ambao wako hatiani kuvuka mstari mwekundu wa maisha yao. Hata hivyo, huruma inakatisha maisha yake.
Misheni hiyo inabaki kwenye mikono ya Schofield ambaye anamtazama Tom aliyekuwa shujaa wake awali akikata roho polepole.
Nisimalize utamu wa filamu hii iliyogharimu takriban Sh231 bilioni kutengezwa chini ya kiongozi mashuhuri Sam Mendes aliyeongoza filamu kibao zikiwemo za Skyfall na Spactre za James Bond.
Filamu ya 1917, itakufundisha kuwapenda ndugu zako na kufurahia kila iitwayo dakika na sekunde iliyo kwenye maisha yako.
Latest
