Mahaba au Nchi: Mwanamfalme katika njiapanda

January 28, 2022 1:51 pm · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni filamu ya Royal treatment inayomuhusu binti anaeangukia katika huba na mwana mfalme wa Lavania.
  • Licha ya kuwa mwana mfalme alisha chumbia, huba kwa binti huyo linashindwa kufichika.

                               


Dar es Salaam. Ukiitazama filamu hii, utaamini msemo usemao maisha ni bahati, kwani unaweza “kuhustle” kimaisha ukahisi kukata tamaa lakini ukaangukiwa na bahati ambayo ikabadilisha sekunde zote zinazofuata kwenye maisha yako.

Hayo yote yanamkuta Izzy mmiliki wa saluni ya kike katika jiji la New York.

Licha ya kuwa na saluni hiyo, Kwake ni sawa na kumlazimisha mkulima afuge kwani kazi hiyo siyo ndoto yake kabisa.

Kwa urembo wake, Izzy ana macho mengi nyuma yake. Namaanisha wananume wengi wanamwinda kama fisi awindavyo kitoweo chake.

Hata hivyo, siku za furaha za binti huyu zinafikia ubeti wa mwisho.Sikumoja, “microwave’ iliyopo saluni kwake inaungua na kusababisha moto.

Uzuri ni kuwa, mali haziungui zote lakini moto huo ulikuwa ganda la ndizi kwa mwenye nyumba kwani wakati maumivu kwa Izzy hayajapoa, tayari mwenye nyumba alikuwa anabisha hodi kutaka alipwe fedha ya matengenezo kutokana na uharibifu wa jengo hilo.

Izzy anajikuta akivunja kibubu chake alichojitunzia kwa muda mrefu kwa ajili ya kusafiri sehemu mbalimbali duniani.

Hebu imagine na maisha yalivyo magumu, umejinyima mwenyewe ukatunza fedha zako siku uende zako Zanzibar halafu siku ikifika, unaibiwa simu au unagundua kuwa fedha zako kwenye kibubu, zimeliwa na panya. 

Maumivu yake hayasimuliki.

Hata hivyo, hasara ya Izzy inazaa baraka nyingine. Ni ipi hiyo?

     

Hasara inayoleta bahati

Akiwa bado anaugulia maumivu ya hasara aliyoipata, namaanisha, pesa ya utalii kulipia fidia na baadhi ya vitu vyake kuungua, muda wa kufuta machozi yake unawadia.

Ni siku ambayo Prince Thomas, mtoto wa Mfalme wa Lavania anapoingia mjini New york kumvisha pete mchumba wake, Lauren.

Usiogope, hakuna ndoa inayovunjika ila zali linalomuangukia Izzy ni saluni yake kuchaguliwa kama sehemu ya kumpatia huduma Prince Thomas.

Mwana mfalme huyo anaridhishwa na huduma za binti Izzy hivyo anaamua kuongeza muda wa huduma yake. Anampa dili la kuwapamba watu siku ya harusi yake. Bahati iliyoje.

Mabegi yanafungashwa, nguo za safari zinaandaliwa, tayari kwa Izzy na timu yake kukwea pipa hadi Lavania kwa ajili ya maandalizi ya harusi.


Soma zaidi


Huba mpya inazaliwa

Kumbuka nilisema hakuna ndoa inayovunjika eeh? Nilikudanganya.

Wakiwa Lavania, Izzy na Prince thomas wanakaribiana kupitiliza na hapo ndipo huba inapojengeka. Prince anashindwa kujizuai na wazo la kuwa alikuwa ameshachumbia mtu linapotea kabisa.

Siyo makosa ya Prince Thomas. Usije kusema men are shoes. Ukweli ni kuwa, mwana mfalme huyo hajawahi kumpenda Lauren. Alikubali ndoa hiyo ili kuikoa Lavania ambayo imeingia kwenye anguko la kiuchumi.

Njia pekee ya kuokoa nchi yake ni ndoa katika ya Prince huyo na Princess Lauren.

Wakati wawili hao wakihisi dunia inazunguka kwa ajili yao tu, mama yake Lauren anashitukia kinachoendelea. Anagundua ya kuwa, Prince Thomas ameshazama kwa Izzy na hata kamba ya kumuokoa haiwezi kumfikia.

Kina cha huba yake kwa Izzy, ni kirefu kuliko hata cha ziwa Tanganyika.

Inakuwaje? Atafanyaje? Lavania itafikia wapi? Ni maswali ya wewe kujibu.

Sitakusimulia hayo ili ukajionee mwenyewe kwenye filamu hii inayopatikana kwenye jukwaa la ‘Netflix’.

Enable Notifications OK No thanks