Ugonjwa wa kipindupindu, kuharisha ulivyowatesa Watanzania mwaka 2025
- Magonjwa ya kuharisha ulikuwa ni ugonjwa ama hali iliyoripotiwa zaidi.
Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakatakiwa kuchukua tahadhari za kiafya zaidi ili kujikinga na magonjwa ya kipindupindu na kuharisha ambayo takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya zinayataja kuwasumbua zaidi wananchi mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuharisha ni hali ya kiafya inayohusisha kujisaidia choo chepesi zaidi kuliko kiwango cha kawaida kwa zaidi ya mara tatu kwa siku, hali ambayo huchangiwa zaidi na maambukizi ya bakteria na virusi vinavyoathiri mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Wakati mwingine kuharisha, hutajwa kuwa miongoni mwa dalili za ugonjwa wa kipindupindu unaosababishwa na bakteria aitwaye Vibrio cholerae, ambao kwa miaka ya nyuma ulitajwa kuchangia idadi kubwa ya vifo.
Takwimu za Mfumo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa (IDSR), zilizotolewa Februari 2, 2026 na Wizara ya Afya zinabainisha kuwa karibu nusu ya visa vyote 369,864 vya magonjwa yanayoripotiwa nchini vinatokana na ugonjwa wa kuharisha.
Visa 176,797 vilihusishwa na magonjwa ya kuharisha, sawa na asilimia 47.8 ya visa vyote vilivyoripotiwa katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2025.

Kila mtu hupata kuhara mara kwa mara, lakini inapodumu zaidi ya wiki nne, huchukuliwa kuwa kuhara sugu. Picha/ Gastro florida.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa karibu mgonjwa mmoja kati ya wawili waliokwenda katika vituo vya afya alikuwa anakabiliwa na tatizo la kuharisha kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Miongoni mwa mikoa iliyoongoza kwa visa vingi vya kuharisha ni Dodoma yenye visa 13,770 (asilimia 7.8), ikifuatiwa na Mara visa 13,622 (asilimia 7.7), Morogoro visa 11,879 (asilimia 6.7) na Rukwa visa 11,494 (asilimia 6.5).
Mwezi wa Mei uliongoza kwa idadi kubwa ya visa, ambapo viliripotiwa visa 78,496 sawa na asilimia 21.2 ya visa vyote ikichangia vifo 33.
Mbali na Kuharisha kipindupindu pia kiliwatesa Watanzania mwaka 2025, visa 3,433 na vifo 26, sawa na asilimia 78.8 ya vifo vyote vikiripotiwa.
Nimonia, ‘typhoid’ pasua kichwa
Ripoti ya Wizara ya Afya inayataja magonjwa mengine yaliwasumbua Watanza ndani ya mwaka 2025 kuwa ni ugonjwa wa nimonia ambapo visa 133,310 vilirekodiwa ikifuatiwa na homa ya matumbo (typhoid) uliokuwa na visa 31,760.

Pneumonia ni maambukizi ya papo hapo ya njia ya hewa yanayohusisha alveoli na njia za hewa za mbali. Picha/ Dr J Suri.
Pia, kulikuwa na visa 12,062 vya kung’atwa na wanyama na visa 6,183 vya kung’atwa na nyoka, maambukizi makali ya njia ya hewa (SARI) yalishika nafasi ya sita kwa visa 4,213 pamoja na vifo saba vilivyoripotiwa.
Homa ya dengue pia yenye visa 84 na kichaa cha mbwa (rabies) kilichokuwa na visa 25 kiliingia katika orodha hiyo ya magonjwa 10 yaliyowatesa Watanzania suala linaloacha mzigo mkubwa wa udhaifu wa mwili kwa wananchi.
Latest