Matukio matano yaliyotikisa Tanzania 2025

December 20, 2025 11:54 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Matukio hayo ni pamoja na vifo vya watu vilivyotokana na ajali, maandamano ya Oktoba 29, vifo vya watu mashuhuri pamoja na kesi na kutoweka kwa viongozi wa siasa. 

Dar es Salaam. Kila mwaka mpya unapoanza, nuru mpya huchomoza ikiashiria mwanzo wa safari ya matumaini kwa siku 365 ikisheheni malengo na ndoto zinazotajia kutimizwa.

Licha ya ndoto na malengo hayo, kila siku, wiki na mwezi hugubikwa na matukio yanayoacha alama na kumbukumbu zisizofutika zinazoweza kuleta furaha au huzuni.

Hivyo hivyo, mwaka 2025 unaweza ukawa ni mwaka usiosahaulika kwa Taifa la Tanzania kutokana na matukio ambayo yametikisa na kuacha historia kwa Watanzania walio wengi.

Nukta Habari imefanya upembuzi na kuainisha matukio yaliyotikisa zaidi nchini Tanzania mwaka 2025 kwa kuzingatia athari, na mapokeo katika jamii, yapo ambayo yametokea kwa mara ya kwanza huku mengine yakijirudia.

Uchaguzi Mkuu

Oktoba 29, 2025 itabaki kuwa tarehe ya kukumbukwa katika historia na vichwa vya Watanzania wengi. Siku hiyo haitakumbukwa tu kwa sababu ilikuwa ni siku ya uchaguzi mkuu bali matukio yaliyoambatana na uchaguzi huo.

Licha ya tukio hilo kuzoeleka na kujirudia kila baada ya miaka mitano lakini uchaguzi wa mwaka 2025 ulikuwa wa aina yake ukibeba zaidi hisia za huzuni kuliko zile za furaha na kuacha mioyo ya Watanzania ikivuja damu.

Huzuni na maumivu hayo yalichagizwa na kile viongozi wa Serikali walichokiita ‘vurugu za wakati na baada ya uchaguzi mkuu’ zilizopelekea vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa miundombinu, mali za umma na binafsi.

Oktoba 29 haitakumbukwa tu kwa sababu ilikuwa ni siku ya uchaguzi mkuu bali matukio yaliyoambatana na uchaguzi huo. Picha | DW.

Wakati wa vurugu hizo intaneti ilizimwa kwa siku tano hadi Novemba 3, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alipoapishwa rasmi kuongoza Tanzania kwa kipindi cha pili hadi mwaka 2030.

Baada ya kutokea kwa vurugu hizo Rais Samia aliunda tume maalum ya watu nane kwa ajili ya kuchunguza matukio hayo na kubaini sababu na waliohusika kuyaratibu ili wachukuliwe hatua.

Vifo vya watu mashuhuri

Mwaka 2025 pia uliingia katika historia ya Tanzania kama mwaka wa majonzi, kufuatia vifo vya watu mashuhuri waliokuwa na mchango mkubwa katika siasa na utumishi wa umma.

Miongoni mwa vifo vilivyotikisa nchi ni kuondoka kwa Cleopa David Msuya, mmoja wa vigogo wa uchumi na siasa nchini Tanzania. Cleopa Msuya aliyefariki Mei 7, 2025 alikumbukwa kama kiongozi mtulivu, mwenye busara na mchango mkubwa katika kujenga misingi ya kiuchumi ya Taifa, hususan kupitia nafasi yake ya Waziri wa Fedha na Waziri Mkuu katika vipindi tofauti vya uongozi wa nchi. 

Jenista ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe bungeni alifariki Desemba 11, 2025 kutokana na maradhi ya moyo akiacha pengo kubwa bungeni, Serikalini na kwa wana Peramiho ambao tayari walimpa nafasi ya kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo. Picha | Bunge

Miezi michache baadae Tanzania ikapoteza tena kiongozi mashuhuri ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kilichotokea Agosti 6, 2025.

Kifo cha Ndugai kilipokelewa kwa mshtuko mkubwa kikifuatiwa na kifo kingine cha Jenista Mhagama, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.

Jenista ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe bungeni alifariki Desemba 11, 2025 kutokana na maradhi ya moyo akiacha pengo kubwa bungeni, Serikalini na kwa wana Peramiho ambao tayari walimpa nafasi ya kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu

Moja kati ya matukio yanayoambatana na hekaheka za kisiasa nchini ni kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi, Aprili 9, 2025 alipokuwa katika mkutano wa kisiasa wa chama chake mkoani Ruvuma na kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Aprili 10, 2025 na kusomewa mashitaka yake.

Kwa wengi, kukamatwa kwa Lissu halikuwa tu habari ya siku moja, bali ni sura ya kihistoria itakayobaki ikitajwa katika mijadala ya siasa za Tanzania kwa miaka mingi ijayo. Picha | DW

Kukamatwa kwa Lissu na kufunguliwa mashitaka ya uhaini kumegeuka kuwa moja ya masuala yanayochochea mjadala mpana wa kisiasa, kisheria na kijamii, ikivuka mipaka ya vyumba vya mahakama na kuingia moja kwa moja katika mioyo na fikra za Watanzania wengi.

Tundu Lissu, ambaye kwa muda mrefu amekuwa sura na sauti ya upinzani mkali, amefanya kesi hiyo inayomkabili kubeba taswira pana ya uhusiano kati ya Serikali na vyama vya upinzani nchini na kuleta mvutano mkubwa wa kisiasa uliogusa misingi ya demokrasia, uhuru wa kisiasa na haki za kiraia.

Kujiuzulu na kutoweka kwa Humphrey Polepole

Huwezi kusimulia mwaka 2025 bila kugusia sakata la kujiuzulu pamoja na kutoweka kwa madai ya kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.

Julai 13, 2025 Polepole aliandika barua ya kujiuzulu Ubalozi wa Cuba kupitia akaunti za mitandao yake ya kijamii kwenda kwa Rais Samia akitaja sababu ni kutoridhishwa na mwelekeo wa uongozi usiojielekeza katika kusimamia haki, amani na kuheshimu watu.

Uamuzi huo ulizua mjadala mpana, hasa ikizingatiwa historia yake kama kada wa muda mrefu wa chama tawala na kiongozi aliyewahi kusimama kidete kutetea misingi ya maadili ya uongozi.

Hata mara baada ya kujiuzulu nafasi hiyo, Polepole alikuwa akiikosoa vikali Serikali kupitia kauli na maandiko yake katika mitandao ya kijamii, akisisitiza masuala ya uwajibikaji, na uongozi unaozingatia haki. 

Kujiuzulu kwake, ukosoaji wake wa wazi dhidi ya Serikali, na madai ya kutoweka kwake viligeuza jina la Humphrey Polepole kuwa kitovu cha mjadala wa kitaifa, kwa wengi, likiwa si tukio la mtu mmoja bali mjadala mpana katika Tanzania ya mwaka 2025. Picha | The Chanzo

Septemba 15, 2025, Jeshi la Polisi lilitangaza kufungua jarada la uchunguzi kuchunguza tuhuma mbalimbali ambazo Polepole amekuwa akizitoa kwa Serikali tangu kujiudhuru kwake likimtaka kuwasilisha ushahidi kwa kuwa tuhuma alizozitoa zinaashiria uwepo wa makosa ya kijinai hivyo zinatakiwa kuthibitishwa iwapo zitafikishwa mahakamani.

Hata hivyo, Oktoba 5, 2025 taarifa za kupotea kwa madai ya kutekwa kwa Polepole zilienea baada ya ndugu zake kueleza kuwa ametekwa na watu wasiojulikana, na Polisi kutangaza kuchunguza tuhuma hizo na hadi sasa hakuna taarifa zaidi zinazoeleza ikiwa kapatikana au lah.

Kujiuzulu kwake, ukosoaji wake wa wazi dhidi ya Serikali, na madai ya kutoweka kwake viligeuza jina la Humphrey Polepole kuwa kitovu cha mjadala wa kitaifa, kwa wengi, likiwa si tukio la mtu mmoja bali mjadala mpana katika Tanzania ya mwaka 2025.

Vifo vilivyotokana na ajali

Mwaka 2025 pia umekuwa mwaka wa huzuni kwa familia nyingi nchini Tanzania, kutokana na mlolongo wa ajali za barabarani zilizoua mamia ya watu, kujeruhi wengine na kuacha majeruhi wenye ulemavu wa kudumu huku jamii ikiomboleza kwa watu waliopoteza wapendwa wao.

Juni 28, 2025, katika eneo la Sabasaba, Same Wilaya, mkoani Kilimanjaro, mabasi mawili yalianguka na kugongana uso kwa uso na kuteketea kwa moto.

Ajali hiyo iligharimu maisha ya abiria wengi ambao walikuwa wakisafiri kwa shughuli za maisha yao ya kila siku, awali ripoti zilionyesha vifo 38 vilitokea kwenye ajali hiyo, lakini baadaye idadi iliongezeka hadi 42 kutokana na watu wengine kuendelea kufariki kutokana na majeraha. 

Mwaka 2025 pia umekuwa mwaka wa huzuni kwa familia nyingi nchini Tanzania, kutokana na mlolongo wa ajali za barabarani zilizoua mamia ya watu, kujeruhi wengine na kuacha majeruhi wenye ulemavu wa kudumu huku jamii ikiomboleza kwa watu waliopoteza wapendwa wao. Picha | Mwanahalisi

Mbali na tukio hilo kubwa la Kilimanjaro, ajali nyingine nyingi za barabarani pia ziliripotiwa mwaka huu, zikitokea maeneo kama Mbeya, ambapo Juni 9, 2025 ajali iliyohusisha lori na magari mengine ilisababisha takriban vifo vya watu 28 na kujeruhi wengine wengi.

Kwa jumla, matukio haya matano yameufanya mwaka 2025 kubaki hai katika kumbukumbu za Watanzania, si kwa sababu ya idadi ya siku ulizojaza kwenye kalenda, bali kwa uzito wa matukio uliyobeba. 

Kuanzia misukosuko ya kisiasa, majonzi ya kuondokewa na viongozi, sintofahamu za kiusalama, hadi vifo vya kusikitisha vilivyotokana na ajali, yote yameacha maswali, funzo na tafakari ya pamoja kama Taifa. 

Tunapoagana na mwaka 2025, tukibakiza kumbukumbu zake, changamoto zake na funzo zake, tunakaribisha mwaka 2026 kwa matumaini, amani na heri na mwaka uliojawa na kumbukumbu za matukio ya furaha. Heri ya Mwaka Mpya 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks