Corona: Hospitali ya Bugando yakabiliwa na uhaba mitungi ya gesi
- Yasema inahitaji mitungi 500 kukidhi mahitaji.
- Ina mashine za kuzaja mitungi 100 tu kwa siku.
- Serikali yawataka wafanyabiashara kushusha bei ya gesi hiyo.
Mwanza. Wakati mapambano dhidi ya janga la Corona yakiendelea Tanzania, Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza imeripoti kuwa na upungufu wa mitungi ya gesi ya oksijeni takriban 500 kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wenye matatizo ya kupumua wakiwemo wa Corona.
Tanzania imeripoti kuwa ina wagonjwa wa Corona katika wimbi la tatu ambalo linaitesa dunia kwa sasa ambapo Rais Samia hivi karibuni alisema kuna wagonjwa zaidi ya 100 wa Corona.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Fabian Masaga akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao cha wadau wa kupambana na ugonjwa huo kilichofanyika leo Julai 6 jijini Mwanza, amesema hospitali hiyo ina mashine za kuzalisha mitungi ya gesi ya oksijeni 100 kwa siku huku mahitaji ni mitungi 300.
Mkurugenzi huyo amewaomba wadau kutoa msaada ili angalau ipatikane mitungi 500 kwa siku itakayotosheleza mahitaji ya wagonjwa katika hospitali hiyo.
“Idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo wanaohitaji mitungi ya oksijeni ni wengi na kwamba hospitali yetu haina mitungi ya kuzalisha hewa hiyo, hivyo tunaomba wadau wajitokeze kusaidia ili tuweze kuwahudumia kwa kuwa wagonjwa ni wengi,” amesema Dk Masaga.
Gesi ya oksijeni imekuwa ni miongoni mwa tiba inayosaidia kuokoa maisha ya watu waliopata maambukizi ya Corona.
Kukosekana kwa gesi hiyo katika vituo vya afya na hospitali kunazidisha athari za janga hilo kwa binadamu ikiwemo kusababisha vifo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amesema upungufu wa gesi ya oksijeni kwenye hospitali unatokana na kuuzwa kwa bei ya juu na wasambazaji.
Amewataka wazalishaji wa gesi hiyo wakiwemo kampuni ya Taifa Gas kuzalisha kwa wingi na kuziuza kwa bei nafuu ili kila mmoja atakayekumbwa na ugonjwa wa Corona aipate kwa urahisi.
Hospitali ya Rufaa ya Bugando imekuwa msaada kwa wagonjwa wa Kanda ya Ziwa. Picha| Mtandao.
Mikakati ya kupambana na Corona Mwanza
Wakati Bugando ikikabiliwa na changamoto hiyo, Mkoa wa Mwanza umeainisha mikakati itakavyosaidia wananchi kujikinga na ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali.
Gabriel amewataka wadau mbalimbali kujitolea vifaa na kinga tiba vikiwemo ndoo za kunawia mikono, vitakasa mikono na barakoa ili viweke kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo stendi za mbasi, shuleni, sokoni na kwenye ofisi za umma.
Mkuu huyo wa mkoa ameziagiza taasisi za umma, dini na viongozi wa vitengo mbalimbali kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kutoka elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.
“Mlipuko wa ugonjwa huu awamu ya kwanza, viongozi tulifanya vizuri katika kusaidia wananchi kuchukua tahadhari, niombe suala hili lipewe kipaumbele pia kwa kuwa mlipuko huu haichagui rika kama ilivyokuwa kwenye mlipuko wa awamu ya kwanza na pili,” amesema Gabriel.
Wananchi wamehimizwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono na vifaa hivyo viwepo nyumbani, shuleni, minadani, stendi za mabasi, masokoni na maeneo mengine yenye mikusanyiko.
“Kwa wale tunaotoka kazini kabla hatujaanza kucheza na watoto ni vema tukifika nyumbani, tuoge, tubadili nguo kisha tuanze kucheza na watoto hili litatusaidia maambukizi haya kutosambaa,” amesema.
Amesisitiza watu kufanya kula chakula bora na mazoezi na ziundwe timu na wataalam watakaonzisha timu za mazoezi vijijini hadi wilayani, lakini watu watenge walau dakika 30 kwa ajili kufanya mazoezi kila siku.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa pamoja kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa wa corona wimbi la tatu ambapo mkoa huo umeainisha vipengere saba vya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuvaa barakoa na kufanya mazoezi. Picha | Mariam John.
Dalili za wimbi la tatu la Corona
Maganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutanchinzibwa emetaja dalili za ugonjwa huo wa tatu kuwa ni homa, kikohozi kikavu na chenye makohozi, mwili kuishiwa nguvu bila sababu, kukosa hisia za harufu, kupoteza hamu na ladha ya chakula.
Dalili nyingine kuwashwa, viuongo vya mwili kuuma na kuharisha.
Dk Rutanchinzibwa amesema tayari mkoa huo umeunda kamati za uratibu wa kukabiliana na mlipuko huo huku akiwataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima pamoja na kutumia barakoa kila sehemu.