Madaktari bingwa 20 wapiga kambi Mwanza kupambana na magonjwa
Wanachi wakiendelea kupatiwa matibabu na madaktari bingwa walioweka kambi katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekouture, Picha | Mariam John.
- Watatoa huduma za kibingwa kwa siku tano.
- Huduma hizo za uchunguzi zinapatikana Rufaa ya Kanda ya Bugando na Sekou-Toure.
Mwanza. Timu ya madaktari bingwa 20 kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando na Sekou-Toure wameweka kambi ya siku tano katika hospitali hiyo kutoa huduma za afya.
Mganga Mfawadhi wa hospitali Dk Bahati Msaki amesema wameamua kuweka kambi hiyo ili wananchi waweze kuchunguza afya zao mapema kisha kupata matibabu kabla madhara hayajawa makubwa.
“Tumeweka kambi hii na tunawaalika wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kupima afya zao pamoja na huduma za kibingwa pia huduma za vipimo mbalimbali kama CT-Scan, X-ray na Eco vitatolewa,” amesema Dk Msaki.
Pia vipimo vya moyo sukari, ugonjwa wa tumbo, sikoseli na saratani ya damu vinatolewa katika kambi hiyo.
Ameanisha huduma zitakazotolewa kwenye kambi hiyo ni pamoja na huduma za kibingwa za macho, mionzi, watoto, meno, magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya mfumo wa damu na chakula, akili, kusafisha damu pamoja na maabara za dawa.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya sikoseli Dk Gloria Mapunda amesema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaoripotiwa katika hospitali hiyo ni wa sikoseli na kueleza kuwa ugonjwa huo unazuilika iwapo wagonjwa watatibiwa kwa wakati.
Amesema takwimu zinaeleza kuwa zaidi ya watoto 11,000 huzaliwa na vinasaba vya ugonjwa wa sikoseli nchini asilimia 7 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano hutokana na ugonjwa huo.
Hata hivyo, amewatoa hofu wananchi kuwa vipimo vya ugonjwa huo vinapatikana na iwapo mgonjwa atabainika na ugonjwa huo atapatiwa matibabu yatakayosaidia kupunguza maumivu ya mifupa.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kambi hiyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Baladya amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ili kuwa na afya njema.
“Ni muhimu kuwa na afya njema hivyo niwaombe mjitokeze kwa wingi ni muhimu kutumia fursa hiyo kuliko kusubiri hadi uanze kuumwa,” amesema Baladya.
Baadhi ya wananchi waliofika kwenye vipimo hivyo akiwemo Mariam Idd ameipongeza Serikali kwa maamuzi ya kusogeza huduma hizo za kibingwa na kuomba ziwe endelevu.
“Usiwe mwanzo wa huduma hizi zije mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi kuchunguza afya zao lakini pia huduma hizi zipelekwe vijijini kwa kuwa kuna wananchi wanashida na hawana uwezo wa kufika kwa ajili ya matibabu,” amesema Idd.
Ibrahim Lyimo, mkazi wa jijini hapa amesema huduma hiyo ni nzuri na inapatikana kwa nadra na kuwaomba wataalam wa afya kuitoa mara kwa mara.
Tangazo

Latest
