Udukuzi wa kidijitali unavyotumika kuwafunga midomo waandishi wa habari
- UN yasema vipo vifaa maalum vinavyotumika kudukua taarifa zao.
- Hali hiyo inahatarisha maisha yao na familia zao.
- Wanahabari watakiwa kuongeza umakini.
Dar es Salaam. Ikiwa zimepita saa chache baada ya kuadhimishwa kwa siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari wanakabiliwa na vitisho wanapotimiza majukumu yao ikiwemo kudukuliwa kidigitali na kunyamazishwa kisiasa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kuhusu siku hiyo alioutoa kwa njia ya video amesema pamoja na ukweli kuwa waaandishi wa habari wamekuwa na jukumu kubwa la kuifahamisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo afya na mabadiliko ya tabianchi lakini vitisho wanavyokabiliana navyo wakati wa kuripoti na kusimulia matukio hayo kwa haki na kwa usahihi, vinaongezeka kila siku.
“Kuanzia masuala ya afya duniani hadi janga la tabianchi, rushwa, na ukiukwaji wa haki za binadamu, waandishi wanakabiliwa na ongezeko la siasa katika utendaji wa kazi zao na majaribio ya kuwanyamazisha kutoka pande nyingi,” Guterres amesema.
Licha ya teknolojia kuongeza wigo wa kupata habari, ni changamoto kubwa kwa wanahabari kwa sababu mifumo ya kidijitali imekuwa ikitumika kuwanyamazisha.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Mataifa Michelle Bachelet amesema ongezeko la matumizi ya zana za uchunguzi kama vile “Pegasus au Candiru spyware” hudukua na kuingilia maisha ya watu.
“Zana hizo za kiteknolojia ambazo zimeripotiwa kutumika angalau nchi 45 duniani ni dharau kwa haki ya faragha na kizuizi cha uhuru wa kujieleza na kwamba matumizi yake yamesababisha kukamatwa, vitisho na hata mauaji ya waandishi wa habari, kuhatarisha vyanzo vya habari pamoja na kuweka familia zao hatarini,” amesema Bachelet.
Zinazohusiana:
- LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni.
- Waziri Nape ayafungulia magazeti manne yaliyofungiwa
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Mataifa yote yamekumbushwa kuwa wanahitaji kuanzisha mbinu za kudhibiti ununuzi na usambazaji wa teknolojia za uchunguzi akisema, lazima yahakikishe kampuni husika zinawajibika.
“Kuheshimu haki za binadamu sio jukumu la Serikali pekee bali pia kampuni za uchunguzi wa kibinafsi zithibitishe hadharani wajibu wao wa kuheshimu uhuru wa kujieleza na faragha, kuzingatia haki za binadamu, na kutoa ripoti kwa uwazi kuhusu shughuli zao.
“Muhimu zaidi, hii inapaswa kufanywa kwa mashauriano ya mara kwa mara na mashirika ya kiraia,” amesema Bachelet
Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa Tanzania yaliyofanyika jijini Arusha kati ya Me1 1 hadi 3, 2022 na kuwaleta pamoja wadau wa tasnia ya habari Afrika kujadili kwa kina jinsi ya kuimarisha uhuru wa kujieleza wakati wakizinabili changamoto za kidijitali.
Latest
