Watu bilioni 3 hawamudu lishe bora duniani

October 16, 2021 5:55 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Janga la Corona limechangia watu kukosa chakula cha uhakika.
  • UN yatoa wito wa kuchua hatua ili kufikia uhakika wa chakula kote duniani.

Dar es Salaam. Wakati leo ikiwa ni sku ya chakula duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres  amesema siku hii siyo tu ni kumbusho la umuhimu wa chakula kwa kila mtu duniani, bali pia ni wito wa kuchua hatua ili kufikia uhakika wa chakula kote duniani.

Guterres katika ujumbe wake wa siku hii amesema “Leo hii karibu asilimia 40 sawa na watu bilioni 3 hawawezi kumudu lishe bora. Njaa inaongezeka, sanjari na utapiamlo na utipwatipwa.” 

Amesema kuwa athari za kiuchumi za janga la Corona (Uviko-19) imesababisha hali ya chakula kuwa mbaya zaidi kwani limewaacha watu wengine zaidi milioni 140 wakikosa fursa ya chakula wanachokihitaji. 

“Jinsi watu wanavyozalisha, kutumia na kutupa chakula kunaathiri vibaya dunia yetu. Kunaongeza shinikizo kwa maliasili yetu, hali ya hewa na mazingira na hivyo kutugharimu matrilioni ya dola kila mwaka,” amesema.

Amesisitiza kuifanyia kazi kaulimbiu ya siku ya chakula ya mwaka huu, “Uwezo wa kubadili mwelekeo uko mikononi mwetu. Matendo yetu ndio mustakbali wetu.” 

Mwezi uliopita viongozi wa dunia walikusanyika kwa ajili ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mifumo ya chakula , na nchi wanachama zilitoa ahadi ya kubadili mifumo hiyo ili kufanya lishe bora kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu na kuifanya mifumo ya chakula kuwa yenye ufanisi, yenye mnepo na endelevu katika kila hatua kuanzia uzalishaji, usindikaji hadi uuzaji, usafirishaji na ufikishaji kwa mlaji. 

“Sote tunaweza kubadili jinsi tunavyotumia chakula na kuwa na machaguo bora zaidi kiafya kwa ajili yetu na sayari yetu. Katika mifumo yetu ya chakula kuna matumaini,” amesisitiza Guterres.

Siku ya chakula duniani inasisitiza kila mtu kujiunga na jumuiya ya kimataifa katika kuchukua hatua za mabadiliko  na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu kupitia mifumo ya chakula ambayo itazalisha lishe bora, mazingira bora na maisha bora kwa kila mtu. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW