Mikopo sekta binafsi yaongezeka Tanzania baada ya maumivu ya Uviko-19

March 23, 2022 5:45 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeongezeka kwa asilimia 10 katika mwaka ulioishia Januari 2022 kutoka asilimia 2.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2021
  • Ukuaji huo umechagizwa na uboreshaji wa mazingira ya kibiashara na sera zinazosimamia  sekta ya fedha.
  • Sehemu kubwa ya mikopo imeelekezwa katika  shughuli za watu binafsi na biashara.

Dar es Salaam. Baada ya sekta binafsi kupita katika kipindi kigumu wakati wa janga la Corona (Uviko-19), matumaini ya ukuaji wa sekta hiyo yameanza kuonekana baada ya kiwango cha mikopo sekta binafsi kuongezeka takriban mara nne Tanzania. 

Kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi na fedha ni moja ya kiashiria cha kuimarika kwa sera za fedha na mazingira ya biashara Tanzania.

Takwimu mpya za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaeleza kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa asilimia 10 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, huku sehemu kubwa ya mikopo hiyo ikielekezwa katika shughuli za watu binafsi na biashara. 

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya mwezi Februari 2022 (Economic Monthly Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni imeeleza kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa asilimia 10 katika mwaka ulioishia Januari 2022 ikilinganishwa na asilimia 2.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. 

BoT imeeleza katika ripoti hiyo kuwa ukuaji huo unatokana na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo kuboresha mazingira ya kibiashara na sera zinazosimamia sekta ya fedha ili kukabiliana na athari za Uviko-19. 

“Ukuaji huo mkubwa ulichangiwa zaidi na uboreshaji wa mazingira ya biashara kutoka katika athari mbaya za Uviko-19, pamoja na sera za pamoja za kifedha,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyochapishwa wenye tovuti ya BoT.

Huenda ukuaji  wa mikopo kwa sekta binafsi ukaendelea kukua kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 10, ikiwa utekelezaji wa sera za kifedha utaimarishwa ikiwemo kukuza kiwango cha mikopo na kupunguza riba wanayotozwa wakopaji.

Kwa mujibu wa BoT, sehemu kubwa ya mikopo hiyo imeelekezwa katika shughuli binafsi ambazo zinajumuisha biashara ndogo na za kati kwa asilimia 25.4 na biashara kwa asilimia 19.6.

Kiasi kingine cha mikopo kwa sekta binafsi kilienda kwenye shughuli za uzalishaji kwa asilimia 7 huku uchimbaji madini ukipata asilimia 10.9 ya mikopo hiyo.

Mikopo inayoelekezwa katika sekta binafsi imekuwa chachu ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini kwa sababu hutumika kutunisha mitaji na ununuzi wa malighafi na utoaji huduma katika shughuli mbalimbali. 

Hata wakati mikopo kwa sekta binafsi ikiongezeka, riba inayotozwa na benki za biashara imepungua kidogo katika kipindi hicho, jambo ambalo litakalo wapunguzia maumivu wakopaji na kuwapa motisha ya kukopa zaidi.


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, riba iliyotozwa na benki kwa mwaka ulioishia Januari ilikuwa asilimia 16.30 ikishuka kutoka asilimia 16.63 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Hivi karibuni baadhi ya benki za biashara ikiwemo CRDB zilipunguza riba inazotoza kwenye mikopo yake ili kuwavutia zaidi wakopaji.

CRDB ilitangaza punguzo la riba katika mikopo kwa kundi la wakulima, pamoja na wafanyakazi Januari 24, 2022 ambapo punguzo hilo la riba lilikuja kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa mabenki kuhusu kupunguza riba ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Riba ya mikopo ya kilimo ya CRDB ilipunguzwa hadi asilimia 9 kutoka asilimia 20 iliyokuwa ikitozwa hapo awali, huku riba ya mikopo ya wafanyakazi ikipunguzwa kutoka asilimia 16 hadi asilimia 13.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV