Riba ya Benki Kuu yabakia 6% Tanzania

October 3, 2024 11:55 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uamuzi huo umetokana kuimarika kwa uchumi nchini na duniani. 

Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2024 itabakia asilimia 6, kiwango ambacho kimedumu tangu kuanzia Aprili mwaka huu. 

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amewaambia wanahabari jijini Dodoma leo Oktoba 3, 2024 kuwa uamuzi huo umeafikiwa kutokana na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la nchi la asilimia 5. 

CBR ni kiwango cha riba ambacho BoT hutumia kufanya biashara na benki za biashara nchini na huwa kama kiongozi cha riba zote sokoni. 

Matumizi ya riba hiyo yalianza baada ya kuanzishwa mfumo mpya wa sera ya fedha inayotumia CBR Januari mwaka huu ikiwa ni miongoni mwa njia zinazotumika na benki hiyo kudhibiti mfumuko wa bei. Kiwango cha kwanza cha CBR katika robo iliyoishia Machi 2024 kilikuwa ni asilimia 5.5. 

Tangu robo ya pili ya mwaka 2024 kiwango hicho cha riba kimebakia kuwa asilimia 6 baada ya kuongezwa kidogo mapema Aprili. 

“Kamati pia inatarajia uchumi kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, sambamba na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani na hapa nchini,” amesema Tutuba. 

Kamati hiyo, iliyoketi Oktoba 2 mwaka huu, inatarajia kuwa uchumi wa dunia utaendelea kukua sambamba na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha.

Tutuba amesema kuwa kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha ulifanikiwa kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5. 

Mfumuko wa bei Tanzania umeendelea kuwa imara ukiwa kati ya asilimia 3.0 na asilimia 3.2 ndani ya mwaka mmoja. Katika mwaka unaoishia Agosti 2024, mfumuko wa bei uliongezeka kidogo hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.0 iliyorekodiwa Julai, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).  

“Katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, uchumi ulikua kwa asilimia 5.6, huku shughuli za ujenzi, kilimo, fedha na bima, na usafirishaji zikichangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huu,” amesema. 

Kwa mujibu wa viashiria vya awali, amesema uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.8 na asilimia 5.6 katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka 2024, mtawalia, na unatarajiwa kuendelea kukua katika viwango hivyo katika robo ya mwisho wa mwaka.

Ukuaji huo unatarajiwa kuchangiwa zaidi na kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi nchini kunatokana na maboresho katika biashara na uwekezaji na kuboreka kwa uchumi duniani. 

Upatikanaji wa fedha za kigeni kuimarika

“Uzalishaji katika shughuli za kilimo unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na matumizi ya pembejeo (mbolea na mbegu bora), viwatilifu na uwekezaji katika miradi ya umwagiliaji,” ameeleza bosi huyo. 

Uchumi wa Zanzibar, kwa mujibu wa BoT, ulikua kwa asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, ukichochewa na shughuli za usafirishaji, fedha na bima, na ujenzi.

BoT inatarajia kuwa upatikanaji wa fedha za kigeni utaendelea kuimarika, kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks