Maumivu kwa wakulima, bei ya mahindi yaendelea kushuka Tanzania

April 13, 2021 1:09 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeshuka kwa asilimia 39.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliolipita huku bei ya zao hilo la chakula ikishuka mfululizo kwa miezi mitatu  iliyopita.
  • Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi mwaka ulioishia Februari 2021 ilikuwa ShSh51,450 ikiwa imeshuka kutoka Sh85,038 iliyorekodiwa Februari 2020.
  • BoT yasema kushuka kwa bei ya mahindi ni kiashiria kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya chakula. 

Dar es Salaam.  Unaweza kusema ni maumivu kwa wakulima wa Tanzania baada ya bei ya mahindi kushuka kwa asilimia 39.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliolipita huku bei ya zao hilo la chakula ikishuka mfululizo kwa miezi mitatu iliyopita.  

Kushuka kwa bei hiyo ya mahindi kunawanufaisha zaidi wanunuzi hasa walaji kwa kuwa hawalazimiki kutoboa zaidi mifuko yao kupata chakula hicho muhimu na utengenezaji wa bidhaa viwandani. 

Lakini wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo, kwao ni maumivu kwa sababu inawapunguzia faida ambayo wangepata endapo wangeuza kwa bei ya juu au sawa na ile waliyouza Februari 2020.

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Machi 2021 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa wastani wa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi mwaka ulioishia Februari 2021 ilikuwa ShSh51,450 ikiwa imeshuka kutoka Sh85,038 iliyorekodiwa Februari 2020.

Bei hiyo ya Februari mwaka huu ni pungufu kwa asilimia 39.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia mwezi Februari. 

Hii ina maana kuwa mkulima aliyeuza mahindi Februari mwaka huu alipatata malipo pungufu kwa Sh33,588 kwa gunia la kilo 100 ikilinganishwa na alivyouza kipindi kama hicho mwaka jana. 

Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo za BoT unaonyesha kuwa bei ya zao hilo imeendelea kushuka kidogo ndani ya miezi ya mitatu iliyopita kutoka Sh56,892  Desemba mwaka jana hadi Sh56,886 Januari mwaka huu kwa gunia la kilo 100

“Kushuka kwa bei mazao mengi ya chakula inaashiria kuna akiba ya kutosha nchini,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo BoT katika kipindi ambacho wakulima wako katika msimu wa kulima mazao yao.


 Zinahusiana: 


Pia bei ya mazao mengi ya chakula ikiwemo maharage, mchele na viazi mviringo zilishuka ndani ya mwaka mmoja isipokuwa uwele.

Uwele ulipanda hadi Sh140,094 mwaka ulioshia mwezi Februari kutoka Sh128,249 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.

Bei za mahindi ndani ya mwaka mmoja uliopita zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji. 

Huenda bei ya mahindi ikaendelea kushuka miezi ijayo ikizingatiwa kuwa mwezi uliopita Kenya ilipiga marufuku mahindi kutoka Tanzania na Uganda kuingia nchini humo kwa kile ilichodai kuwa yana sumu kuvu ambayo ina madhara kiafya jambo linaloweza kupunguza mahitaji sokoni. 

Hata hivyo, baada ya mazungumza ya kidiplomasia, Kenya iliondoa marufuku hiyo huku ikiweka masharti mapya yanayosimamia ununuzi wa mahindi katika nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Enable Notifications OK No thanks