Zaidi ya watu milioni 50 kukumbwa na balaa la njaa Afrika Mashariki
- Zaidi ya watu milioni 50 kukumbwa na balaa la njaa Afrika Mashariki
- Ni kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa mazao.
- Mabadiliko ya tabianchi nayo yachangia.
Dar es Salaam. Zaidi ya watu 50 milioni waishio nchi za Afrika Mashariki kukabiliwa na janga la njaa kwa mwaka 2022, huku sababu kubwa ikiwa ni mabadiliko ya tabia ya nchi, migogoro na changamoto za kiuchumi.
Taarifa ya pamoja ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Mpango wa Chakula wa Dunia (WPF) na Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) iliyotolewa Julai 22, mjini Addis Ababa, Ethiopia, inasema Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, na Sudan ndiyo nchi zilizoathirika zaidi na balaa hili.
“Takwimu tunazotoa ni za kuhuzunisha, na nina wasiwasi kwamba zinaweza kuongezeka zaidi kwani matarajio ya msimu wa mvua wa Oktoba hadi Desemba ni mbaya.” amesema Workneh Gebeyehu, Katibu Mtendaji IGAD.
Taarifa hiyo inafafanua zaidi kuwa janga la njaa kwa mwaka 2022 limeongezeka kwa asilimia 19, ukilinganisha idadi ya watu milioni 42 iliyokubwa na janga la njaa kwa mwaka 2021.
Sambamba na hilo takriban watu 300,000 wanatarajiwa kukabiliwa na janga la njaa la juu ngazi ya tano hususani kwenye nchi za Somalia na Sudan Kusini.
Sababu kubwa ni kushindwa kwa uzalishaji wa mazao na mifugo, kuongezeka kwa gharama za chakula na kukosekana kwa misaada ya kibinadamu.
Janga hilo pia limewakumba watoto milioni 10 walio chini ya umri wa miaka 5, huku wakikabiliwa na utapiamlo mkali.
Soma zaidi:
- corona: njaa kuongezeka mara mbili zaidi afrika mashariki
-
Uamuzi mgumu UN: Nani apatiwe msaada wa chakula Afrika Mashariki?
Tanzania hali ikoje
Wakati baadhi ya Watanzania wakila na kusaza kiasi cha kutupa chakula, ripoti mpya ya usalama wa chakula na lishe Tanzania inakadiria kuwa kuanzia Mei 2022 watu 592,000 watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya maeneo nchini.
Kufahamu zaidi, sikiliza sauti hii kuhusu hali ya chakula nchini Tanzania:
Latest
