Mei Mosi 2023: RC Malima ataka uadilifu mahala pa kazi
Baadhi ya watumishi wakiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi 2023 ambapo kwa Mkoa wa Mwanza yamefanyika katika viwanja wa Mnadani wilayani Sengerema. Picha | Mariam John.
- Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima asema hiyo itasaidia kuleta tija kazini.
Mwanza. Wafanyakazi wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mahala pa kazi ili kuondoa malalamiko ya wananchi wanaowahudumia ili uzalishaji uwe na tija.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi 2023 amesema amekuwa akipokea malalamiko yanayohusiana na uadilifu kutoka pande zote mbili za mwajiri na mfanyakazi.
“Tuendelee kushirikiana na kushikamana na kusisitiza uwajibikaji na uadilifu mahali pa kazi, waajiri wamekuwa wakilalamikia suala la uadilifu na uaminifu lakini na wafanyakazi pia, najua tukiwa waadilifu na kufanya kazi kwa kujituma tija itaongezeka, fikra yangu hatuna budi kuondoa tofauti hizi ili kuongeza tija,” amesema Malima.
Mkuu huyo wa Mkoa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Kazi na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) waendelee kutembelea maeneo ya kazi kwa ajili ya kuwaelimisha wafanyakazi haki na wajibu wao pamoja na kutatua changamoto.
“Hili jambo halitakiwi kusubiri Mei mosi, tunatakiwa tuwe tunalielewa, hivyo taasisi hizo zifanye majukumu yake kikamilifu ili kuondoa changamoto maeneo ya kazi,” amesema Malima wakati akijibu maombi ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuhusu kuboresha mazingira ya kazi.
Soma zaidi:
Pia amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, kusimamia kwa karibu Idara ya Kazi Mkoa wa Mwanza ili iweze kufanya kazi kwa karibu na kufuatilia masuala ikiwemo utaratibu wa wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi na utoaji wa mikataba ya wafanyakazi.
Awali Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza, Athuman Zebedayo amesema bado wafanyakazi wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mishahara kutokidhi mahitaji ya sasa hasa ukizingatia hali ya maisha imepanda.
Changamoto nyingine iliyowasilishwa ni pamoja na baadhi ya waajiri hasa taasisi binafsi kutowasilisha michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na wengine kushindwa kuwalipa wafanyakazi wao posho pale wanapokuwa kazini saa ya ziada.