“The Little Things”: Filamu ya kukufikirisha kuhusu umakini wako

February 12, 2021 2:43 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mara ngapi umeshindwa kuangalia vitu vidogo vidogo vinavyoweza kukupa ufumbuzi wa mambo yanayotokea?
  • “The Little Things” ni filamu itakayokufundisha kutokuhukumu kitabu kwa jarada lake.
  • Pale afisa mtetezi anapomuua mtu kwa kudhani kuwa ni mhalifu inamfanya rafiki yake kuchukua  maamuzi magumu kulinda amani ya moyo wake.

Dar es Salaam. Siku zote huwa ni vijimakosa vidogo vidogo vinavyosababisha mambo mbalimbali katika jamii yetu kutokea ikiwemo mwizi kukamatwa baada ya kamera kumnasa, mpenzi kuachika baada ya meseji za mchepuko kufumaniwa na hata mtoto aliyelamba sukari kusahau kufuta mabaki ya sukari yaliyopo mdomoni.

Kwa jambazi, inaweza ikawa ni alama za vidole vilivyobaki katika eneo la tukio, kitambulisho kilichookotwa karibu na eneo la mauaji na hata picha iliyochukuliwa na kamera za ulinzi bila kujua. Huwa ni vitu vidogo ambavyo huenda hatuvifikirii wakati jambo fulani linatokea.

Ilikuwa ni mwaka 1990, mwanadada mmoja alikuwa akiendesha gari akifurahia mandhari na uumbaji  wa dunia. Ghafla, alianza kuhisi kuwa kuna mtu anamfuatilia na alikua dereva wa pikipiki ambaye alikuwa nyuma yake.

Hofu ikimjaa na mapigo ya moyo yakiongezeka, mwanadada huyo anaamua kuingia katika sheli iliyokuwa karibu yake ili atafute usalama lakini kama wahenga wasemavyo, siku ya kufa nyani, miti yote huteleza na yeye sheli hiyo inakuwa imefungwa.

Kuokoa maisha yake, anaamua kushika njia na kukimbilia jangwani ambapo malaika mtoa roho anaahirisha safari yake baada ya dereva wa roli kumuona dada huyo na kugeuka msaada. 

Kwa dada huyo, dereva huyo ni kama mwamvuli ulivyo katika mvua nzito zinazoendelea.

Baada ya Deke kushindwa kutatua kesi yake, kessi mpya inakuwa ni sehemu ya kumtafuta muuaji aliye shindwa kumpata kwa muda mrefu. Picha| Google images.

Sasa turudi kwenye reli…

Ni siku mpya ndani ya jiji la Bakersfield nchini Marekani ambapo Polisi msaidizi wa mji wa Kern Country Joe “Deke” Deacon anaitwa na Idara ya polisi katika Jiji la Los angeles kuchukua vielelezo vya mauaji yaliyotokea hivi karibuni.

Deke ambaye awali alikuwa afisa mpelelezi wa Idara hiyo anaambatana na Mkuu wa upelelezi anayejulikana kwa jina  la Jimmy Baxter kuelekea katika eneo ambalo  mauaji yalitokea.

Kumbuka kuwa Baxter na Deke hawafahamiani sana lakini wanapowasili katika eneo la tukio, Deke anagundua kuwa mauaji yaliyofanyika hayana utofauti na mauaji yaliyofanyika kitambo kidogo ambayo  hakuweza kukamilisha upelelezi wake.

Huenda ni jambo gumu sana kwa Deke hasa kuukumbuka udhaifu wake ambapo siku hiyo iliripotiwa mwanadada aliyefahamika kwa jina la Ronda Rathbun ambaye alikuwa akifuatiliwa na gari wakati akifanya mazoezi ya kukimbia na kutekwa siku iliyofuata.

Kesi hiyo ilimtesa sana Deke hadi kufikia kiasi cha kuachwa na mkewe na kupata shambulio la moyo.

Baada ya Baxter kushauriwa na baadhi ya maafisa kuwa aachane na Deke katika upelelezi huo, Deke hakubali kushindwa kwa mara ya pili, anaomba likizo ili ashirikiane na Baxter kutafuta ufumbuzi wa kesi hiyo.

Ni kesi ya kwanza hiyo lakini haiishii hapo inakuwepo ya pili, ya tatu na namba zinaongezeka na kusababisha FBI kuingilia kesi hiyo  kwani kila shambulio linaliripotiwa, linakuwa limefanyika vile vile na aliyeuwawa ni binti ambaye anajihisisha na uchangudoa.

Kesi hizi zinamleta kwenye mwanga Sparma ambaye ana hulka ya kupenda uhalifu. Wakati Baxter na Deke wakilazimika kufanya msako bila ruhusa katika nyumba ya Sparma bila yeye kuwepo, mauaji yanamfikia  mmoja wa askari polisi.

Sparma hayupo nyumbani, polisi ameuwawa, nani kamuua? Ni swali ambalo kila  mtu anajiuliza.

Kwa Baxter, machale yake ya mwili mzima yanamwambia kuwa mhalifu ambaye anatafutwa ni Sparma lakini kwa kuwa kijana hataki kutoa ushirikiano, inamlazimu afisa mpelelezi kumuua na hivyo kupoteza ushahidi pekee ambao huenda walikuwa nao yeye na msaidizi wake Deke. 

Deakon anapojua kuwa Baxter amemuua Sprama, anamshauri amzike jangwani lakini pale anapoenda jangwani ili akamalize ushahidi wote, anaukuta mwili wa Sparma ukiwa bado unapigwa na jua.

Mpelelezi ameua mtu ambaye hatia yake bado haijathibitishwa. Nani anakuwa na kosa? Baxter anafanya kila awezalo kuthibitisha kuwa Sprama ndiye muuaji ili kesi ifungwe lakini Deke anamshauri aachane na hiyo kesi kwani itamtesa maisha yake yote.

Baada ya kashi kashi zote kuisha, Baxter anapokea bahasha iliyotumwa na Deke. Na ndani yake mna kofia ambayo Ronda Rathbun alikuwa ameivaa wakati anatekwa. 


Soma zaidi:


Akiwa nyumbani kwake, Deke anachoma kila kitu alichokichukua kama ushahidi wakati wa msako wake kwenye nyumba ya Sprama pamoja na kifurushi cha kofia nne kama aliyotumiwa Braxter lakini kifurushi hicho hakina kofia nyekundu.

Wakati filamu inaanza, muuaji alionekana kutembea kawaida tu lakini kwa filamu nzima, Sprama alikuwa akitembea kama anadunda flani hivi, jambo linaloweza kukuonyesha kuwa, huenda yeye sio muaji.

Nani anahusika kufanya mauaji yaliyoonyeshwa? Anaweza kuwa ni Deke, je ni afisa polisi, je, ni mpelelezi au ni nani haswa? Kwani hata baada ya Sprama kuuawa na Baxter, mwili mwingine uliouwawa kwa yeye unaonekana.

Filamu hii inaonyeshwa katika skrini mbalimbali za filamu nchini Tanzania na mara nyingi, gharama ya kuitazama haizidi Sh10,000 katika kumbi za Century Cinemax. 

Kutana na waigizaji waliojenga majina yao katika tasnia ya filamu akiwemo Denzel Washington, Rami Malek na Jared Leto.

Wiki ijayo kuna filamu gani? Endelea kufuatilia Nukta Habari.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...