The Archenemy: Filamu inayokupa sababu za kutokumdaharau mtu usiyemjua
- Filamu inamhusu kijana mwenye ndoto za kuwa mwandishi wa habari za uhalifu anayekutana na chokoraa Max Fist.
- Max anasema yeye siyo wa dunia hii na uwepo wake duniani ndio unamfanya asiwe na nguvu zake za maajabu.
- Licha ya kuwa hana nguvu, analazimika kupambana vilivyo kuhakikisha usalama wa rafiki zake dhidi ya magwiji wa dawa za kulevya.
Dar es salaam. Nakumbuka wakati tulivyokuwa watoto, tulifundishwa kutokudharau mtu ambaye hatumjui kwani huenda akakusaidia mbeleni.
Tulifundishwa kusalimia watu pale tunapokuwa ugenini kwani watu hao huenda wakawa msaada pale utakapokuwa umepotea na unahitaji kuelekezwa.
Kwa bwana mdogo Hamster (Skylan Brooks), huenda mafundisho hayo yalimuingia vilivyo kwani anapokutana na Max Fist (Joe Manganiello), bado anamheshimu licha ya kuwa kwa jamii ya Kitanzania, Max angelitambulika kama chokoraa.
Kisa hichi kiko kwenye filamu ya The Archenemy.
Imani ya Hamster juu ya Max ni kubwa kiasi cha kutokutaka kusikia la kuambiwa juu yake kwani anaamini maneno ambayo Max anayasema kuhusiana na nguvu zake za maajabu.
Ikiwa malengo ya kijana huyo ni kuwa mwandishi wa habari za uharifu, anachukua nafasi ya kuwa msaidizi kwa Max ambaye anadai amepoteza nguvu zake.
Kwa wengine, ni vichekesho na wanamchukulia Max kama mtu asiyejielewa na aliyepoteza dira ya maisha yake.
Hata hivyo, anachodai Max ni kuwa yeye siyo mtu wa dunia hii bali ni mwana mpotevu aliyetengwa mbali na dunia yake na uwepo wake duniani unaathiri nguvu za maajabu ama waweza kuziita “super powers” alizokuwa nazo.
“Nilikua nikikaa katika majengo marefu zaidi duniani kwetu na ninaangalia chini kama Mungu,” ni Max akielezea maisha yake ya awali kabla ya kuwa mlevi.
Soma zaidi:
- Huyu ndiye mwanafunzi bora kidato cha nne mwaka 2020
- Yakuzingatia kabla hujasaini mkataba wa ajira
- VIDEO: Fahamu haya kabla haujanunua “makeup”
Anachokidai Max ni kuwa, duniani kwake pombe kidogo tu ingemtosha lakini hata pombe kali zaidi katika dunia ya Hamster, haijafanya lolote kwake.
Filamu hii inamuhusu Hamster na dada yake Indigo (Zolee Griggs) ambao ni yatima wanaopigana kujinasua dhidi ya mtandao wa wauzaji wa madawa ya kulevya na sukari inakolea zaidi wanapokutana na Max ambaye anajitoa mhanga kuhakikisha usalama wa rafiki zake wapya.
Fuatilia filamu hii kupitia skrini za sinema nchini na katika baadhi ya mitandao itakayokuhitaji kuwa na GB za kutosha.
Pia unaweza kuisikiliza habari hii kupitia Soundcloud kwa kubonyeza alama ya “play”