Teknolojia ya kuteketeza taulo za kike (pedi) itakavyookoa mazingira Tanzania
- Inachoma kilogramu 100 za taulo za kike kwa saa moja
- Inaokoa muda na ni salama kwa mazingira
Dar es Salaam. Huenda changamoto ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na kutupwa hovyo kwa taulo za kike zilizotumika ikapungua nchini Tanzania baada ya wabunifu kutengeneza mashine ya kutekeza taulo za kike kwa muda mfupi bila kuchafua mazingira.
Katika maeneo kadhaa nchini ikiwemo Mwanza, kumeripotiwa kero ya utupwaji holewa wa taulo za kike jambo linalosababisha kuziba kwa chemba na mitaro ya maji na kuchochea uwepo wa harufu mbaya katika maeneo hayo.
Kampuni ya habari ya Marekani ya ABC inabainisha kuwa kwa wastani mwanamke hutumia kati ya taulo 10,000 hadi 12,000 kwa kipindi cha maisha yake ambapo hatari zaidi ipo katika taulo za kutupa ambazo hutumia miaka 500 hadi 800 kuoza.
Soma zaidi : Teknolojia ya vifuu vya nazi itakavyo waokoa wachimbaji na madhara ya zebaki
Mashine hiyo iliyopewa jina la Mellita, inauwezo kuchoma taulo za kike zilizokusanywa kwenye ndoo tano za lita 20 ndani ya dakika 30 mpaka saa moja na hivyo inatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa mazingira.
Tarsila Mellita (23) ndiye mbunifu wa mashine hiyo, ambapo ameiambia Nukta Habari kuwa, alipata msukumo wa kuitengeneza baada ya kupewa adhabu ya kuteketeza taulo za kike akiwa shule ya sekondari.
Sehemu ya kuchomea taulo za kike kwenye mashine ya Mellita. Pichal Tarsila
Moshi uliotoka kwa wingi katika mtambo wa kuteketezea taka hizo ndio ulimpa hamasa ya kuja na njia bora zaidi itakayokuwa rafiki kwa mazingira na kuokoa muda.
“Ilinichukua saa 48 kuteketeza pedi zote ambapo hewa chafu itokanayo na plastiki ilikuwa ikitoka katika mtambo wa kuchomea, ndipo nikapata wazo la siku moja kuja na njia rafiki ya kuteketeza taulo zilizotumika,” amesema Mellita.
Mafunzo ya nadharia na vitendo aliyoyapata katika Shirika lisilo la kiserikali la Open Map Development Tanzania (OMDTZ) mwaka 2021, yalimuwezesha kupata maarifa ya namna gani angeweza kuitimiza ndoto yake jambo ambalo amekwisha lifanikisha.
Soma zaidi : Kutana na mbunifu wa majiko yanayotumia mawe Tanzania
Inaokoa muda na rafiki wa mazingira
Kwa mujibu wa Tarsila, mashine hiyo hutumia nishati ya umeme kuzalisha joto linalofikia kiwango cha nyuzi joto 700 ambalo huteketeza ndoo tano za lita ishirini zilizojazwa taulo zilizotumika kwa muda wa dakika 30 hadi saa moja tofauti na mashine nyingine ambazo hutumia zaidi ya saa 36.
Aidha, mashine ya Mellita huzalisha majivu yanayoweza kutumika kamba mbolea pamoja na kiwango kidogo cha moshi ambao hutoka dakika tano za mwanzo pekee, jambo linalosaidia kutochafua hewa na moshi wenye kaboni inayotajwa kuharibu tabaka la ozoni.
Mashine hiyo hufikisha kiwango cha nyuzi joto sentigredi 700 zinazoiwezesha kuchoma kilogramu 100 ya taulo za kike ndani ya saa moja. Picha l Tarsila
Jamii inasemaje?
Tarsila ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uchumi katika Chuo Cha Mtakatifu Agustino (Saut) ameiambia Nukta Habari kuwa, mapokeo ya ubunifu wake kwa jamii ni mazuri, hivyo anaendelea kuifanyia maboresho zaidi ikiwemo kuifanya isitoe kabisa moshi ili kulinda afya ya mtumiaji pamoja na mazingira.
“Jamii imepokea vizuri mashine kwani prototype yetu ya kwanza iliweza kuvutia hospitali sita na shule nyingi jijini Mwanza hivyo uhitaji wa mashine hizi ni mkubwa, tunamalizia maboresho kwenye technical parties (masuala ya ufundi) chache kisha ziingie sokoni rasmi,” amesema Tarsila.
Hata hivyo mashine hiyo itakapokamilika haitatumika kuchoma taulo za kike pekee bali hata taulo za watoto (diapers) hivyo inaweza kutumika kwenye taasisi zinazohudumia watu kwa wingi kama shule, hospitali, vyuo pamoja na hotelini.
Soma zaidi : Teknolojia ya utengenezaji mkaa mbadala inavyoweza kupunguza ukataji miti ovyo
Mlima wa kupanda
Pamoja na mashine hiyo kusaidia utunzaji wa mazingira watumiaji watatakiwa kutoboa mifuko yao ili waweze kuipata ambapo itauzwa kwa Sh5 milioni.
Aidha, watu waishio maeneo yasiyo na nishati ya umeme watakosa fursa ya kutumia mashine hiyo kwani lazima kuwe na umeme ili iweze kufanya kazi.
Hata hivyo ubunifu huo umemfanya Tarsila atengeneze ajira kwa vijana watatu wanaoshiriki kuziunda mashine hizo ambao wanajipatia kipato.
Kwa mujibu wa Tarsila mashine hiyo itaanza kupatikana nchi nzima kuanzia Mwezi Disemba mwaka huu.