Majaliwa akabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa mafuriko Hanang
- Ujenzi wa nyumba hizo umewawezesha wananchi 745 kupata makazi.
- Majaliwa atoa wito kwa wananchi wengine kuhamia.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekabidhi nyumba 109 zilizojengwa na Serikali katika kijiji cha Gidagamowd kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi leo Disemba 20, 2024 amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo umezingatia ubora na zitakidhi mahitaji ya waathirika hao wa ambao tangu kutokea kwa tukio hilo hawakuwa na makazi maalum.
“Nyumba hizi zimejengwa kwa kuzingatia viwango bora vya ujenzi, vikiendana na jografia nya Wilaya ya Hanang ambayo ina mvua nyingi na uwezekano wa matetemeko ya ardhi, nyumba hizi zinauwezo wa kuhimili hayo yote,” amesema Majaliwa.
Serikali ya Tanzania imekabidhi nyumba hizo kwa wahanga hao ikiwa ni mwaka mmoja tangu kutokea kwa janga hilo Disemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu 89 na majeruhi 139.
Mbali na vifo maporomoko hayo yalisababisha uharibifu wa mashamba na miundombinu ya barabara katika wilaya ya Hanang huku nyumba za kuishi na maduka zaidi ya 100 zikibomoka na kuathiri watu 5,600.
Ujenzi wa nyumba hizo 109 zilizofadhiliwa na Serikali, Shirika la Msalaba Mwekundu na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) umewawezesha wananchi 745 kupata makazi.
Nyumba hizo ambazo ni makazi mapya kwa waathirika hao zina ukubwa wa mita za mraba 29 na vyumba vitatu vya kulala, sebule, jiko, bafu na choo pamoja na miundombinu ya maji, umeme na barabara.
Aidha, katika eneo hilo pia kuna jumla ya viwanja 269 vya makazi pekee vikiwa 226, biashara viwanja 26, na viwanja 17 kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya utoaji wa huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa Majaliwa ujenzi wa miundombinu mingine ikiwemo shule ya msingi umeanza na unatarajiwa kukamilika Januari, 2025 huku mingine kama kituo cha afya na soko kubwa la kudumu ukitarajiwa kukamilishwa hivi karibuni.
Muonekano wa nyumba mpya zilizojengwa na Serikali kwa ajili ya waathirika wa maporomoko ya tope Hanang.
Watanzania Karibuni Gidagamowd
Licha ya nyumba 109 kujengwa katika eneo hilo, Majaliwa amewakaribisha Watanzania kutoka maeneo mengine wanaotamani kuanzisha makazi katika kijiji cha Gidagamowd.
Anayetaka kuhamkia katika kijiji cha Gidagamowd anapaswa kufuata utaratibu wa ununuzi wa ardhi uliowekwa na halmashauri kununua mojawapo ya viwanja 161 ambavyo tayari vimepimwa .
“Yeyote anaetaka aende halmashauri afate masharti, alipe, ajenge ili tuwe na mji…hiki sio kituo cha waathirika ni cha wenyeji wa Hanang, tusiwafanye hawa kama watu ambao wamefungwa mahali, nataka kuona wengine wanakuja wanajichanganya na mamlaka zitafanya kazi mpaka huku,” amesema Majaliwa.
Kwa upande mwingine, miti ya 600 ya matunda itagawiwa kwa wananchi wote watakao hamia eneo hilo, sambamba na mingine 4,256 ikijumuisha ya matunda, kivuli na mbao itakayopandwa na Wakala wa Misitu Tanzania kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya hiyo na Shirika la Save the Children.