Kutana na mbunifu wa majiko yanayotumia mawe Tanzania

Lucy Samson 0817Hrs   Agosti 24, 2023 Ripoti Maalum
  • Ni Raymond James, ukosefu wa ajira ndio ulimhamasisha kuja na ubunifu huo.
  • Linatumia mawe, chenga za mkaa wa vifuu vya nazi pamoja na umeme.
  • Limetengenezwa kwa bati zito linalosaidia kutunza joto wakati wote wa matumizi.


Dar es Salaam. Nishati ya kupikia ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya binadamu duniani kote, hiyo ndio huwezesha mapishi ya aina mbalimbali za vyakula tunavyokula ili kuimarisha afya na kuwezesha utendaji wa shughuli za kila siku.

Watu wengi wanatambua gesi, mkaa, umeme, mafuta pamoja na kuni kama ndio vyanzo vya nishati ya kupikia kwa kuwa ndio ambavyo vinatumika kwa kiasi kikubwa kwa sasa huku jitihada nyingi zikielekezwa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hata hivyo, jijini Dar es Salaam kuna ubunifu mpya wa nishati ya kupikia inayotumia mawe, ambapo inatajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kupikia kwa gesi, umeme, mkaa au nishati nyingine.

Ndiyo! Ubunifu, udadisi pamoja na uthubutu umewezesha ugunduzi huu ambapo sasa mawe yanayopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi nchini Tanzania yanaweza kutumika kama chanzo cha nishati ya kupikia.

Raymond James (25) maarufu kama Mr Majiko, ndiye mbunifu wa majiko hayo yanayotumia mawe, umeme kidogo pamoja na chenga za mkaa mbadala zinazotokana na vifuu vya nazi.

Kijana huyo mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, ameiambia Nukta Habari kuwa kukosa ajira ndio sababu kubwa iliyommchochea kubuni majiko hayo ili aweze kujiingizia kipato kitakachomuwezesha kuendesha maisha.

“Baada ya kumaliza kidato cha sita nikawa sina kazi yoyote mtaani ikabidi nirejee kwenye elimu yangu je ni nini kitanisaida, nikaanza kujishughulisha na ubunifu ili nipate pesa maisha yaendelee,” anasema Raymond.

Mawe yanayotumika katika jiko hili yakikolea unaweza kuzima umeme na kupikia kwa  joto linalozalishwa na mawe hayo.Picha |Daudi Mbapani/Nukta Africa.

Elimu ya kidato cha kwanza yawezesha ubunifu

Tofauti na wabunifu wengine ambao husomea taaluma fulani inayohusiana na kifaa wanachokitengeneza, Raymond aliyeishia kidato cha sita hajasomea popote ubunifu huo.

Raymond, anabainisha kuwa alianza ubunifu huo mwaka  2019 akiwa hana uzoefu wowote wa kuchomelea majiko au kuunganisha zaidi ya kumbukumbu za ‘madesa’ ya somo la Kemia aliyoyapata akiwa kidato cha kwanza mwaka 2013.

“Ilikuwa kama najaribisha tu…ikabidi nirejee elimu yangu ya kidato cha kwanza, nilisoma kuhusu metal (metali) na non metal ndipo nikafikiria kuhusu mawe na nikaanza kuyatumia kwenye majiko ya kawaida,” anasimulia Raymond.

Kwa kuwa hakutaka kutumia mkaa kama chanzo cha kuyafanya mawe yapate moto, ilimlazimu Raymond kuingia darasani kupitia machapisho, majarida pamoja na kujifunza kwa wengine ni kwa namna gani anaweza kufanikisha hilo.

Mwaka moja baadae yaani 2020 ndipo alipopata njia mbadala ya kuzalisha chanzo cha moto katika majiko yanayotumia mawe ambacho ni chenga za mkaa zilizotengenezwa kwa kutumia vifuu vya nazi.

“Ili moto uwake nafahamu kuwa unahitaji oksijeni hivyo nikaenda kusoma zaidi nikafamu jinsi inavyozalishwa nikaanza kuunganisha feni ndogo zitakazolazisha upepo utakaosaidia moto kuwaka kwa haraka,” amebainisha Raymond. 

Kadri miaka ilivyoenda ndivyo kijana huyo alivyozidi kufanya maboresho na ubunifu zaidi mapaka sasa jiko hilo linatumika na zaidi ya watanzania 100 waliopo maeneo mbalimbali nchini.


Zinazohusiana


Jiko la mawe kiundani

Majiko yaliyobuniwa na  Raymond yametengenezwa kwa kutumia bati zito kwa nje linalosaidia kutunza joto, kwa ndani lina nafasi kubwa kiasi inayomuwezesha mtumiaji kuweka mawe kwa ajili ya kupikia.

Pembeni ya jiko hilo, limeunganishwa na feni ndogo inayozalisha upepo unaokoleza moto pindi ikiunganishwa na umeme.

Ili uweze kutumia jiko hilo itakulazimu kulipia Sh80,000 kwa jiko dogo la nyumbani na Sh120,000 kwa jiko kubwa unaloweza kulitumia kwenye biashara ya chakula au mgahawani.

Baada ya kununua jiko hilo ni lazima uunganishe jiko hilo na umeme ili liweze kuwaka kwa haraka na ukiridhika na kiwango cha moto unaweza kuzima feni kwa kubonyeza 'switch' ndogo iliyopo pembeni ya jiko hilo.

“Jiko hili linatumia umeme kidogo, lina Wati120 yaani umeme wa uniti moja unaweza kutumia hata wiki nzima…linatumia umeme wowote ule wa jua au wa gridi ya taifa,” ameongeza Raymond.

Jiko hilo la bati linalotumia umeme halina hatari yoyote, mpaka sasa hakuna ripoti yoyote ya jiko hilo kulipuka au kusababisha madhara kwa watu.

Licha ya uzuri wa jiko hilo, bado halina sehemu ya kupunguza au kuongeza moto, utakapotaka kupunguza moto  basi ni lazima uzime feni na ukitaka kuongeza utaiwawasha.


Chenga za mkaa zitokanazo na vifuu ni njia mbadala ya kuzalisha nishati inayowezesha mawe kuwaka vizuri na kwa muda mrefu kulinganisha na mkaa utokanao na miti unaochangia uharibifu wa mazingira.Picha|Daudi Mbapani/Nukta Africa.

Linaokoa gharama

Festo Paulo, muuza chips Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa  tangu ameanza kutumia jiko hilo ameokoa gharama zilizokuwa zinapotea katika matumizi ya mkaa.

“Zamani nilikuwa natumia mkaa wa Sh15,000 mpaka Sh20,000 kwa siku lakini sasa hivi nikichanganya na mawe unakuta natumia chenga za Sh4,000 au Sh3,000 kwa wiki…kuhusu umeme hauliki sana,” anasema Festo.

Mbali na kuokoa gharama jiko hilo linamsaidia Festo pamoja na vijana wengine wanaofanya biashara ya kuuza chipsi katika eneo hilo kuhudumia wateja kwa haraka kutokana na urahisi wa kuwasha jiko hilo na uwezo wake mkubwa wa kutunza moto.

Kwa upande wake Anastazia Mkule, mama lishe kutoka Majohe, Gongo la Mboto anasema ubunifu wa aina hiyo unaweza kuwasaidia wafanyabiashara wa chakula kama yeye kuokoa gharama na muda.

Soko bado changamoto

Licha ya ubunifu huo wa kuvutia bado Raymond amekuwa akikumbana na  changamoto ya Soko la jiko hilo huku wengine wakisumbua kwenye malipo baada ya kupata huduma yake.

kutokana na ufinyu wa soko la majiko yake wakati mwingine  hulazimika kuwaachia wateja majiko kwa muda wa  siku mbili au tatu ili wayaribu kwa kabla hajawauzia ambapo baadhi yao huwa si waaminifu.

Hata hivyo, matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa msaada mkubwa katika utafutaji wa wateja kwa kuwa inamuwezesha kuwafikia hata wateja waliopo mikoa mingine.

Ripoti ya takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo ya pili ya mwaka 2023 (Aprili hadi Juni 2023) imebainisha kuwa watumiaji wa mtandao nchini wamefikia milioni 34.

Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya nusu ya watanzania wote waliopo nchini wanatumia mtandao, jambo linaloweza kufungua fursa kwa wafanyabiashara kujitangaza na kuwafikia watu wengi.

Ni chanzo cha mapato

Kupitia ubunifu huo Raymond sasa anaweza  kujipatia kipato kinachoendesha maisha yake huku kikimuwezesha kuajiri kijana mwingine mmoja ambaye naye anajikimu kupitia kazi hiyo.

Pius Francis, fundi aliyeajiriwa na Raymond amebainisha kuwa kazi hiyo imekuwa msaada kwa kumuwezesha kupata fedha za kujikimu, tofauti na alivyokuwa awali wakati amemaliza kusomea ufundi wa kuunga vyuma mwaka mmoja uliopita.

“Nimefanya nae kazi (Raymond)kwa muda mfupi lakini kwa muda huo wote nimejipatia kipato ambacho kinanisaidia katika kuendesha maisha yangu,” anasema Pius

Jiandae kwa ubunifu zaidi 

Raymond anasema anaendelea kujifua zaidi na huenda akaja na ubunifu mwingine wa majiko kama hayo ambayo yatawaka bila kutegemea nishati ya umeme.
Huenda majiko hayo yakawa mkombozi kwa wakazi waishio vijijini ambapo hakuna kabisa nishati ya umeme na vyanzo pekee vya nishati ya kupikia vilivyopo ni vile vinavyoharibu mazingira ambavyo ni kuni pamoja na mkaa.

Tanzania inakusudia kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.

Malengo ya Raymond ni kufungua kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa majiko hayo na aina nyinginne mpya zinazotumia teknolojia ya kisasa yakayoenda kupunguza matumizi ya mkaa na kuni yanayochangia vifo zaidi ya watu 33,000 kila mwaka kutokana na moshi wenye sumu.

Unaweza kuwasiliana na Raymond James kufahamu zaidi kuhusu majiko ya mawe kupitia namba 0767743318.

Related Post