Teknolojia, suluhu za asili kuokoa kilimo 2020
Udhibiti endelevu wa maliasili na kulinda bayoanuai kwa ajili ya kufikia mifumo endelevu ya chakula ni muhimu katika kuboresha kilimo na uzalishaji wa chakula. Picha| Erwan Hesry/Unsplash.
- Ni njia muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
- Suluhu za asili zinajumuisha hatua katika mifumo ya udongo, maji, mifugo, bahari na mifumo ya chakula.
- FAO yasema azma hiyo itafanikiwa ikiwa ushirikiano wa wadau wote utahimizwa.
Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema suluhu za asili za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo utunzaji wa misitu ni muhimu na lazima zijumuishe teknolojia ili kuchagiza mifumo bora ya upatikanaji wa chakula.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu akizungumza kando ya mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi (COP25) mjini Madrid, Hispania, amesema ubunifu ikiwemo kujumuisha teknolojia kwa sasa ni kitovu cha maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo.
Katika taarifa iliyotolewa na FAO, Dongyu amezitaja suluhu hizo kuwa zinajumuisha hatua katika masuala ya misitu na mifumo mingine kama udongo, maji, mifugo, bahari na mifumo ya chakula pamoja na mazingira ya chakula na watumiaji.
“Tunajiandaa kubadili mfumo wa chakula, ni lazima tuufanyie mabadiliko mnyororo wa uzalishaji chakula, thamani na wa usambazaji, suluhu pekee ni ubunifu,” amesema Dongyu wakati.
Amesema azma hiyo itafanikiwa ikiwa ushirikiano wa wadau wote utahimizwa, jambo likalosaidia kuboresha sekta kilimo mwaka 2020.
Zinazohusiana:
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki.
- Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima Tanzania kufaidika na fursa ya uhaba wa chakula duniani?
Amesisitiza kuwa udhibiti endelevu wa maliasili na kulinda bayoanuai kwa ajili ya kufikia mifumo endelevu ya chakula ni muhimu katika kuboresha kilimo na uzalishaji wa chakula.
Ametoa mfano wa mradi uliotangazwa mapema jana (Desemba 12, 2019) kati ya FAO, Ujerumani na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wa kuzisaidia nchi zinazoendelea kushughulikia mabadiliko ya tabianchi katika sekta zao za kilimo.
FAO itaendelea kushirikiana na kwa karibu na wadau wote katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, nchi, asasi za kiraia, sekta binafsi, wanazuoni na washirika wote muhimu ili kuongeza ufanisi wa suluhu zilizopo na kuhakikisha kwamba suluhu za asili zinasalia kuwa kitovu kwa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kulinda bayoanuai.
Latest
