Teknolojia ilivyoibua wimbo wa “Mkono wa Bwana” wa Zabron Singers

October 3, 2019 3:32 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wimbo huo kwa sasa ni miongoni mwa zile zinazotazamwa zaidi Youtube.
  • Ulirekodiwa rasmi mwaka 2014 na kuzinduliwa mwaka mmoja baadaye.
  • Baadhi ya vituo vya redio havikuupa nafasi wimbo huo kama nyingine.
  • Hata hivyo, umaarufu wake ulianza baada ya kuwekwa kwenye mtandao wa YouTube.
  • Mkono wa bwana umesaidia kujitegemea na kupata mialiko lukuki ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mpenzi wa kusikiliza ama kutazama nyimbo katika mtandao wa YouTube huenda umeshakutana na wimbo wa “Mkono wa Bwana” ambao umekuwa maarufu zaidi katika siku za hivi karibuni. 

Wimbo huo wa kwaya ya Zabron Singers kutoka Kahama mkoani Shinyanga ndiyo wimbo pekee wa injili ulioingia katika orodha ya nyimbo bora zaidi kwa sasa nchini Tanzania katika mtandao wa Youtube ikishikilia nafasi ya nane hadi mchana wa Oktoba 3. 

Wimbo huo unazidi kupanda chati siku hadi siku katika orodha hiyo ukizungukwa na nyimbo maarufu za Bongo fleva za sasa kwenye chati za umaarufu YouTube zikiwemo “Kijiwe nongwa” ya Rostam na Shilingi ya Mbosso wa Wasafi.

Hata wakati wimbo huo ukizidi kuwa maarufu sasa hadi kuchukua tuzo ya wimbo bora wa kwaya nchini Kenya kwa mwaka 2019, safari yake ni ya milima na mabonde. 

Kwa wanaosikia sasa kwa mara ya kwanza, Mkono wa bwana ulirekodiwa miaka mitano iliyopita na kuzinduliwa mwaka 2015. 

Mashairi ya wimbo huo, “chini hata juu, watu unawainua, sifa na utukufu ni zako milele” yamesuuza zaidi mioyo ya Watanzania na nchi zingine huku ukifikia kiwango cha juu zaidi ya cha umaarufu Septemba 23 hadi Septemba 27 2018. 

Katika kipindi hicho, wimbo huo ulipata alama 100 katika chati za umaarufu za mtandao wa Google “Google trends” ambao hupima umaarufu wa jambo, watu au vitu vinavyotafutwa zaidi mtandaoni.

Muonekano wa jinsi wimbo wa “mkono wa Bwana” wa Zabron singers unavyotafutwa mtandaoniKatika kipindi cha umaarufu huo, harusi, sherehe na tafrija mbalimbali na hata “Status” za mitandao ya kijami zilisheheni vipande vya wimbo huo. Picha| Google trends.

Kabla ya kupata umaarufu huo, kwaya hiyo ilipeleka sauti na video ya wimbo huo katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni lakini vingi viliupuuza miaka minne iliyopita huku baadhi vikiupiga kidogo ukilinganisha nyimbo nyingine za wakati huo. 

“Wakati tunautoa tulijaribu “kuupush” (kuusambaza) lakini hakukuwa na mwitikio kutoka kwenye redio na TV. Tulifikia maamuzi ya kuweka YouTube mwaka 2016 na tangu hapo tulishuhudia ukifanya vizuri” amesema Japhet Zabron, Mwalimu na mtunzi wa nyimbo za kwaya ya Zabron Singers.

Awali wazo la kutumia teknolojia ya mtandao wa Youtube kusambaza wimbo huo halikuwepo miongoni mwa wanakwaya wa kwaya hiyo ya Kanda ya Ziwa. 

Youtube na mitandao mingine ya kusambaza kazi za muziki na video kama Vimeo, Tidal, Amazon, Mkito, Sound Cloud na Spotify imekuwa ni msaada mkubwa kwa wasanii ambao wanahaha kusambaza kazi sokoni. 


Zinazohusiana


Wimbo wachangia kuongeza mapato

Mkono wa Bwana umewawezesha Zabron Singers sasa kuweza kujisimamia na hadi kufikia uwezo wa kujilipia fedha za kurekodi nyimbo studio na hata kuendesha semina mbalimbali kutokana na mapato wanayoyapata kutoka Youtube na mialiko ya matamasha.  

Kabla ya hapo, kwaya hiyo ilitegemea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali ambao baadhi Zabron amewataja kuwa Charles Mbwega na mchungaji Khalid Sadiki wa kanisa la SDA Kahama.

Licha ya kuwa awali wimbo huo ulikosa “sapoti” kwenye vyombo vya habari hapo awali, kwa sasa wimbo unazidi kupigana vikumbo na nyimbo mpya za injili kama za Goodluck Gozbert, Joel Lwaga, na hata Paul Clement kwenye mtandao wa Youtube. 

Hadi sasa Mkono wa bwana umetazamwa marai milioni 9 kufikia Oktoba 3 saa 7 mchana, ukiwa ndiyo uliotazamwa zaidi ukizidi hata Siteketei ya Angel Benard yenye watazamaji na “Umewazidi wote” wa Bahati Bukuku wenye watazamaji milioni 8.3. 

Kwanini wimbo huo ni maarufu kwa sasa?

Zabron amesema wimbo huo unazidi kuwa maarufu kwa sababu ya ujumbe wake wa kumshukuru Mungu kwa mafanikio. 

Amesema watu wengi humshukuru Mungu baada ya mafanikio hivyo ujumbe uliopo kwenye wimbo huo unaufanya kuwa chaguo sahihi la shukrani.

“Unapoimba huo wimbo ni kama unasali. Hauimbi tu bali unarudisha shukrani kwa Mungu. Ujumbe uliopo umegusa watu wengi na ndio maana wanaeupenda,” amesema Zabron.

Tofauti na kwaya zingine, Zabron Singers ni kwaya ya ukoo wa mzee Zabron Ngelela ambayo ilianzishwa mwaka 2006 na kuanza kurekodi nyimbo mwaka 2014. Kwa sasa kwaya ina waimbaji 13 ambao wote ni ndugu na wawili tu wanatoka nje ya ukoo huo.

Wimbo huo wa kwaya ya Zabron Singers kutoka Kahama mkoani Shinyanga ndiyo wimbo pekee wa injili ulioingia katika orodha ya nyimbo bora zaidi kwa sasa nchini Tanzania katika mtandao wa Youtube ikishikilia nafasi ya nane hadi mchana wa Oktoba 3. Picha|Mtandao.

Motisha ya kikundi hicho imetokana na mzee Ngelela ambaye siyo tu alianzisha utumiaji wa magitaa kwenye makanisa ya kisabato ukanda wa ziwa bali alikuwa ni mwalimu wa gitaa na mtunzi mahiri wa nyimbo. Miongoni mwa kazi zake ni wimbo wa “Meli imeng’oa nanga” wa mwaka 1984  ambao ilitikisa masikio ya wasikilizaji wa BBC miaka ya 1980.

Mafanikio zaidi

“Tumefanya semina mwaka huu na watu 40 walijiunga na kanisa letu baada ya semina hiyo. Kwa sasa tunaweza kujitegemea sio kama awali ambapo tulipata msaada kutoka kwa watu kama Charles Mbwega na Mchungaji wetu Khalid Sadiki,” amesema Japhet.

Japhet amesema, ni umaarufu wa wimbo huo uliowapatia safari za kutumbuiza nchini Uganda, Kenya na hadi kufikia hatua ya kuvuka mipaka ya bara ifikapo mwaka 2020.

Bado una kiu ya Habari? Fuatilia uchambuzi wa mambo ambayo hukuwahi fikiria kama utayafahamu kupitia tovuti hii ya habarii.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...