Zingatia haya kabla hujatangaza bidhaa mtandaoni

October 12, 2021 8:40 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Andaa tangazo linaloendana na vipimo vya mtandao husika.
  • Weka taarifa muhimu kwenye tangazo ikiwemo mawasiliano na eneo la kazi.
  • Ukumbuke kufanya mapitio baada ya tangazo lako kuisha.

Dar es Salaam. Bila shaka, wafanyabiashara wote wanakubaliana na msemo wa kuwa “biashara ni matangazo” kwani, siyo jambo geni kumsikia mama muuza mboga asubuhi akipita nje ya nyumba akitangaza biashara yake kwa sauti kubwa inayotosha kukuamsha.

Pia, kwa mitaa ya Mwenge, Karume, Kariakoo na kwengineko wanapouza mitumba, vipaza sauti, mabango na wengine wametunga hadi nyimbo za za kutangaza bidhaa au huduma zao.

Kadiri siku zinavyokwenda na teknolojia inavyobadilika, mifumo ya kuwafikia watu kwa matangazo nayo inabadilika. Mifumo mbalimbali ya kutangaza mtandaoni kwa wajasiriamali wadogo na wakubwa imeibuka na kurahisisha maisha.

Hata hivyo, baadhi ya wajasiriamali wamekuwa hawapati matokeo mazuri kibiashara kwa kutangaza kwa kutumia mifumo ya kidijitali ikiwemo mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na Twitter.

Wapo wanaolalamika matangazo kutokusaidia chochote hasa kuongezeka kwa wafuasi na mauzo.

Hali hiyo inasababishwa na kutokuwa na uelewa wa mambo ya kuzingatia pale unapochagua mitandao ya kijamii kuwa sehemu ya wewe kutangaza biashara yako.

Kila mtandao unamahitaji ya vipimo kwa ajili ya picha na video. Vizingatie. Picha| Behance.

Uzingatie nini? Dondoo za wataalamu wa masoko hizi hapa:

Tengeneza tangazo lako kustahimili mfumo wa simu

Kuanzia vipimo vya tangazo kwa upana na urefu, muda wa tangazo lako na mvuto pia.

Unapoandaa tangazo kwa ajili ya kuweka kwenye mitandao ya kijamii fikiria kuwa una sekunde mbili za mwanzo za kumvutia mtu kabla hajachagua kulichinjia tangazo lako baharini.

Hakikisha vipimo vya picha yako vinatosha mtu kuona tangazo lako lote na pia maandishi yaliyopo kwenye tangazo yanaonekana vyema kwa mtumiaji wa simu.

Mtaalamu wa masuala ya masoko, Theresia Venance ameiamba Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, kila mtandao wa kijamii una vipimo kwa ajili ya picha na video zake. 

Kama utatangaza tangazo lako kwa mitandao mbalimbali hakikisha vipimo pia vinazingatiwa.


Chagua mtandao sahihi 

Kila mtandao wa kijamii una watu wake wenye kariba tofauti tofauti. Kuanzia Linkedin, Facebook, Twitter na WhatsApp, kila mtandao una watumiaji wake.

Mathalan, Linked in kwa jamii ya watu wenye taaluma, waajiri na waajiriwa. Instagram ya wajasiriamali na watu maarufu na Facebook ya watumiaji wengi wa simu janja.

Venance amesema, “angalia kama tangazo lako linalenga watu wa kawaida au watu wa maofisini uchague jukwaa stahiki.”

Mtaalamu huyo amesema, mara nyingi kama unataka ufikie watu wengi zaidi, unaweza kutumia Facebook kwani ndiyo mtandao wenye watumiaji wengi duniani wanaofikia bilioni 2.8.


Tangazo

Fuatilia habari sauti (podcast) zenye maudhui ya filamu pamoja na ripoti maalumu zilizofanywa na Nukta Habari kupitia Spotify, Anchor, Apple Podcasts na kokote unaposikiliza podcast zako. 


Tumia vizuri mifumo ya mitandao ya kijamii

Mitandao ya kijamii inaambatana na mifumo tofauti tofauti. Mfano WhatsApp ina mfumo wa makundi sogozi, meseji za matangazo (broadcast masages), ‘status’ na meseji za kawaida. 

Vivyo hivyo kwa Instagram yenye TV, Posts, Reels na Stories. Unaweza kutengeneza tangazo lako kuelekea mifumo mipya ya mtandao husika kwani huwa na wafuatiliaji wengi zaidi. 

Fahamu malengo ya wewe kutangaza

Inashauriwa pia kufahamu malengo ya wewe kutangaza ili kutengeneza tangazo zuri. Inaweza kuwa kuongeza wafuasi au kuongeza mauzo.

Mfano kama ni kuongeza mauzo, itakuwa rahisi kujua namna tangazo lako liwe ili kuvutia mtu kununua bidhaa yako.

Pia kama ni kwa ajili ya kuongeza wafuasi (followers) itakuwa rahisi kwako kujua namna tangazo linapaswa kuwa ili kuwavutia watu wakufuatilie.

Kuwa “simpo” kadri iwezekanavyo na tangazo lako lisiwe na mambo mengi kiasi cha kumchanganya mtazamaji. Kumbuka, una sekunde 60 tu kwa video kukamilisha tangazo lako ili lilete matokeo mazuri.

Kama lengo la wewe kutangaza ni kuvuta wafuasi wengi zaidi, tengeneza tangazo lako kuvutia watu wachague kukufuata. Picha| Sabma Digital.

Hakikisha tangazo lako limejitosheleza

Hauhitaji tangazo ambalo linawaacha watu na maswali. Mfano bei ya bidhaa zako, mahala unapopatikana na matumizi ya bidhaa yako.

Venance ameshauri kuhakikisha tangazo lako linatoa taarifa zote muhimu kuhusu biashara au huduma unayoitoa.

Ni vyema kuweka taarifa za mawasiliano kwa ajili ya kurahisisha ufikiwaji wako pale mtu anapohitaji kupata huduma unayoitoa au kununua bidhaa unayouza.


Fanya mapitio baada ya tangazo lako kuisha

Kwa mifumo ambayo matangazo yanalipiwa mfano Twitter, Facebook na Instagram, huwa mifumo ina kawaida ya kutoa taarifa fupi ya mafanikio ya tangazo lako kuanzia watu waliofikiwa na hatua zilizochukuliwa na watu.

Mfano wafuasi walioongezeka kutokana na tangazo lako, watu waliotembelea tovuti yako na watu waliotuma tangazo lako kwa wengine.

Venance amesema ni muhimu kufanya mapitio baada ya kutangaza ili ufahamu kama njia hiyo ya utangazaji inakufaa au la.

Unataka kutangaza kwa kutumia mtandao gani, tuulize tukusaidie kupitia +255 677 088 088.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW