Kicheko maboresho ya kanuni za maudhui mtandaoni Tanzania
- Serikali yaboresha kanuni hizo kwa kufuta baadhi ya leseni
- Watakaofaidika ni waelimishaji na waburudishaji mtandaoni.
- Vyombo vya habari kuendelea kulipia leseni.
Dar es Salaam. Huenda watengeneza maudhui yakiwemo ya filamu watamaliza wiki hii kwa tabasamu baada ya Serikali kufanya marekebisho ya Kanuni ya Maudhui ya Mtandaoni ya mwaka 2020 ambayo imefuta leseni kwa maudhui yanayolenga kuelimisha na kuhabarisha Tanzania.
Kanuni hiyo iko chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta maarufu kama EPOCA ambayo ilikuwa inawataka watengeza maudhui hasa ya kuhabarisha kuwa na leseni ili kupata kibli cha kurusha matangazo yao mtandaoni ikiwemo YouTube wakiwa Tanzania.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alitoa taarifa ya marekebisho hayo Machi 15, 2022) wakati akizungumzia mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani.
Katika maboresho yaliyofanywa, Waziri Nnauye alisema Serikali imefuta ulazima wa kuwa na leseni kwa watengeneza maudhui ya mtandaoni ambayo yanalenga kuelimisha na kuburudisha ikiwemo muziki na filamu.
“Kanuni hizi zimefanyiwa marekebisho kuboresha matumizi ya mtandao na hivyo kukuza fursa ya vipaji,” alisema Waziri Nnauye.
Watakaofaidika na mabadiliko hayo ya kanuni ni watengeneza maudhui yakiwemo ya mapishi, michezo na usanii huku wanaohusika na maudhui ya kuhabarisha na matukio ya kila siku kuendelea kulipia leseni.
“Kwa marekebisho haya, habari na matukio ya sasa (news and current affairs) ambayo hutolewa pia na vyombo vya habari vya kawaida ndiyo zitakazo katiwa leseni lakini hizi huduma zingine hizi, wanaotoa elimu, wanaotoa burudani tumefuta leseni ili tuwaruhusu vijana wajiajiri lakini pia kuongeza wigo wa kazi zao kufika,” alisema Nnauye.
Awali kupakia maudhui yoyote mtandaoni, mtu alitakiwa kuwa na leseni. Picha| iStock.
Wadau watoa ya moyoni
Kauli hiyo ya Serikali imepokewa kwa hisia tofauti na watu mbalimbali kwenye jamii huku baadhi yao wakisema uamuzi huo ni kupigiwa upatu kwa sababu utafungua fursa zaidi za ajira na kuongeza wigo wa kupashana habari, jambo linalosaidia kuimarisha uhuru wa kujieleza na kutoa maoni nchini.
Baadhi ya watengeneza maudhui ya muziki wamesema kuondolewa kwa leseni hiyo kumewapatia ujasiri wa kuendeleza vipaji vyao kwani mlolongo wa kupata leseni hiyo na gharama zilikuwa zikiwakatisha tamaa.
Mwanamuziki wa nyimbo za injili, Humphrey Moses ameiambia Nukta habari (www.nukta.co.tz) kuwa aliwahi kufuatilia leseni hiyo na mlolongo wote na gharama zake “vilimkata maini”
“Nilikuwa naona uzito hata kutangaza kazi zangu nilizokuwa nikiweka YouTube nikihofia kupigwa faini kwa kupakia maudhui bila kuwa na leseni,” ameeleza Moses ambaye ana wafuasi zaidi ya 1,400 kwenye mtandao wa YouTube.
Kufutwa kwa leseni hiyo kumempa Moses morali ya kusambaza maudhui yake bila hofu ya kupigwa faini mbeleni.
Soma zaidi:
- Utajiri uliojificha ufugaji wa kuku wa kisasa
- Umeme unavyompaisha kimaisha binti wa miaka 21 Njombe
- Yaliyojificha nyuma ya mikopo ya vikundi vya wajasiriamali
Ni nafasi ya Watanzania kujiajiri na kuongeza kipato
Mtengeneza maudhui ya kuwasaidia watalii kuielewa Tanzania, Doreen Mbalazi amesema uwepo wa leseni hiyo ulisababisha kuyumba kwa chaneli yake ya YouTube.
Akiwa ni mtengeneza maudhui anayechipukia, Mbalazi amesema ilimuwia vigumu kutengeneza video kwa ajili ya kuwavutia watalii kuja nchini na kwa kipindi chote alichokuwa kimya, watazamaji wake walikuwa wakihoji juu ya maudhui yake.
Kufutwa kwa leseni hiyo kunamrudisha Mbalazi katika shughuli za kutengeneza maudhui ambayo yatachochea watalii kuja nchini na kuongeza pato la taifa.
Watengeneza maudhui ya mapishi wanaoweka kazi zao mtandaoni hawatalzimika kuwa na leseni. Picha| Clifford Sangai.
Walimu watarudi darasani
Mtandao wa YouTube ni sehemu kwa baadhi ya watengeneza maudhui kutoa madarasa ya kufundisha vitu mbalimbali. Wapo wanaofundisha kupika na wapo wanaofundisha jinsi ya kutumia programu na kuendana na teknolojia mbalimbali.
Kati yao, ni mtengeneza Maudhui ya Kiswahili, Richard Maguluko (Richstar) ambaye leseni hiyo ilimlazimu kuifunga chaneli yake ili asubirie kupata leseni.
“Kabla ya leseni, walau nilikuwa najipatia kipato kupitia maudhui yangu na gahrama zilirudi kwenye kulipia gharama za vifurushi, kulipa mtu wa usaidizi na kuazima vifaa,” amesema Richstar.
Kwa mdau huyo wa YouTube, kusimamisha utoaji wa maudhui kumempunguzia watu waliokuwa wanamfuatilia na hata kipato alichokuwa akikipata awali.
Kufutwa kwa leseni hiyo ni habari njema kwake kwani awali alikuwa akihofu kupakia maudhui yake.
“Nakumbuka niliambiwa kuifunga chaneli yangu na nirudi (TCRA) baada ya miezi sita. Nilipoteza karibu nusu ya jamii yangu ya mtandaoni na mchangamano wa maudhui,” amesema Richstar na kuongeza kuwa, “kufutwa leseni hiyo ni habari njema.”
Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mitandaoni), 2018 zilizotengenezwa chini ya Kifungu cha 103 cha sheria ya EPOCA na zilitiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kipindi hicho, Dk Harrison Mwakyembe.
Kupitia kanuni hizo wamiliki wa blogu, radio na televisheni za mtandaoni walipaswa kujisajili ili waweze kuendelea kutoa huduma hizo ikiwemo wanamuziki, filamu na watoa maudhui ya mtandaoni kama Rich Star na Mbalazi.
Latest



