Facebook, Instagram kuanza kulipa wazalisha maudhui Tanzania
- Ni kupitia matangazo yatayoonekana katika maudhui yao.
- Ni fursa ya kujiingizia kipato, kupunguza tatizo la ajira.
Dar es Salaam. Wazalishaji wa maudhui ya mtandaoni kupitia majukwaa ya Instagram na Facebook nchini huenda sasa wakapata chanzo kipya cha mapato baada ya kampuni ya teknolojia ya Meta kutangaza kuwa itaanza kuwalipa wazalishaji hao waliopo Tanzania.
Meta, kampuni kubwa ya teknolojia nchini Marekani, ina miliki mitandao ya Facebook na Instagram ambayo inaongoza kwa kuwa na wafuasi wengi duniani.
Hatua hiyo ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za wadau wa mawasiliano, watetezi wa haki za kidijitali pamoja na mamlaka za Serikali kushawishi kampuni hiyo kuanza kuwalipa wazalisha maudhui wa mtandaoni.
Taarifa iliyotolewa na Meta Agosti 7, 2024 ilibainisha kuwa mwezi huu wataweka kipengele cha kuonesha mapato ambayo mzalishaji wa maudhui atayapata ikiwa ni sehemu ya kampuni hiyo kutoa faida ya mapato iyapatayo.
Hata hivyo, watengeneza maudhui watatakiwa kwanza kukidhi masharti kadhaa kabla ya kunufaika na programu hiyo yakiwemo kuzingatia sera za mapato kutoka kwa washirika wa Facebook.
Mtengeneza maudhui anapaswa kuwa awe na umri wa miaka 18 na zaidi na awe anaishi katika nchi iliyoruhusiwa na kutimiza masharti ya kupata matangazo ndani ya maudhui.
“Masharti kunufaika na video zinazohitajika (video on demand), muandaaji anapaswa kuwa na wafuasi 5,000, dakika 60,000 zilizotizamwa katika siku 60 zilizopita na ukurasa uwe na angalau video tano,” imebainisha taarifa ya Meta.
Aidha, kuhusu masharti ya kunufaika na video mbashara (live streaming), muaandaaji anapaswa kuwa na wafuasi 10,000 na jumla ya dakika 600,000 zilizotizamwa katika siku 60 zilizopita.
Meta si kampuni ya kwanza
Uamuzi huo wa Meta, unaongeza idadi ya kampuni zinazowalipa wazalishaji wa maudhui nchini na kufikia tatu wakitanguliwa na YouTube pamoja na X (zamani Twitter).
Aidha, yapo majukwaa mengine yanayowalipa wazalishaji wa maudhui hasa ya muziki na podcast kama Boomplay, Audiomark, Deezer, Sportfy pamoja na Apple Music.
Ni jambo lililosubiriwa muda mrefu
Mdau wa masuala ya kidigiti, Baraka Mafole ameiambia Nukta Habari kuwa uamuzi huo wa Meta umesubiriwa kwa muda mrefu nchini Tanzania kwa sababu baadhi ya mataifa ya Ulaya na Amerika yalishaanza kunufaika na programu hiyo miaka mingi iliyopita.
“Kwa Meta kuruhusu malipo kwa wazalisha maudhui kwanza itakuwa na faida kwao kwa kuwa watapata watu wengi watakaovutiwa na majukwaa yao lakini pia ni fursa kwa wazalishaji maudhui kupata sehemu ya kujiingizia kipato cha ziada na hii itakuwa chachu kwa mitandao mingine kufuata nyayo za Meta,” amesema Mafole.
Mafole amesisitiza kuwa ni muhimu Serikali pamoja na wazalisha maudhui wakubwa nchini wakaongeza jitihada za kushawishi mitandao mingine kuanza kuwalipa wazalisha maudhui.
Mtaalamu huyo ametolea mfano namna Serikali ya Kenya kwa kumtumia Rais wake William Ruto alivyoshirikiana na watengeneza maudhui kufanikisha hilo.
Ni fursa ya kupunguza tatizo la ajira
Mafole ambaye amekuwa akihamasisha vijana kwa muda sasa kutumia mitandao ya kijamii kujiingizia kipato amesema uamuzi huo wa Meta sio tu utabadilisha mitizamo ya wengi kuhusu mitandao hiyo bali itasaida kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.
“Tamanio langu ni kuona siku moja watoto wana ndoto za kuwa wazalisha maudhui, ndo dunia inaelekea huko, katika nchi zilizoendelea watu wanaingiza kipato kizuri kupitia kazi hiyo,” amebainisha Mafole.
Chanzo kimoja cha habari kimeeleza kuwa Meta watakuwa na kongamano na wazalishaji maudhui Agosti 15 jijini Dar es Salaam kutoa elimu namna ya kunufaika na mpango huo wa malipo.
Tangazo hilo la kulipwa litakuwa ni ahueni pia kwa vyombo vya habari nchini ambavyo vimeshuhudia ukuaji dumavu wa mapato yatokanayo na habari za mtandaoni.
Sehemu kubwa ya mapato ya mtandaoni hutwaliwa na kampuni kubwa za teknolojia kama Meta, Google, X Corp, Amazon huku wakiwaachia watengeneza maudhui na malipo kiduchu.
Hata hivyo, mbali na baadhi ya mitandao kuanza kulipa, miongoni mwa changamoto kuu imekuwa ni kupata mfumo rafiki wa kuweza kutoa fedha hizo kwa kuwa kampuni nyingi zinatumia huduma ya PayPal na nyingine ambazo si rahisi kutoa fedha taslimu ukiwa Tanzania.
Latest
