Matukio makubwa ya kisiasa ya kukumbukwa mwaka 2022
- Miongoni ni kujiuzulu kwa Spika Job Ndugai kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
- Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na wakuu wa mikoa.
Dar es salaam. Tofauti na dini, mpira, muziki, na siasa ni miongoni mwa mambo yanayowakutanisha Watanzania kwa wingi na hujadiliwa kwa upana kwa sababu inagusa maisha yao ya kila siku.
Katika vijiwe vya kahawa, kwenye usafiri wa umma, hata maeneo ya kazi na biashara huko kote wanajadili kuhusu siasa za vyama, kauli a wanasiasa na hata matukio ya kisiasa ikiwemo ziara na mikutano ya viongozi na wananchi.
Mwaka 2022 umekuwa na matukio mengi ya kisiasa yaliyoibua mijadala mikubwa ndani na nje ya nchi kutokana na namna yalivyotendeka.
Historia mpya zimeandikwa na rekodi zimevunjwa, fuatana nami katika makala haya nikiangazia baadhi ya matukio ya kisiasa yaliyoitikisa Tanzania mwaka 2022.
Ziara za Rais Samia Suluhu Hassan
Disemba 14, 2022, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alishiriki mkutano wa viongozi wa Afrika na Marekani uliofanyika kwa siku tatu jijini Washington DC nchini Marekani.
Hiyo si safari yake ya pili nchini humo kwa mwaka 2022, kwani tayari alishakwenda Aprili kwa ajili ya uzinduzi wa filamu maalumu ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania iliyopewa jina la “The Royal Tour” ambayo ilizinduliwa Aprili 18 jijini New York.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Samia amejitofautisha na mtangulizi wake kwa kufanya ziara za mara kwa mara nje ya nchi jambo linalotajwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na jumuiya za kimataifa.
Nje ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2022, Rais Samia amefanya ziara Msumbiji, Ghana, Oman, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC), Qatar, Ufaransa, Ubelgiji pamoja na China akiwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kufanya ziara China tangu janga la Corona (Uviko-19) lipungue makali.
Ziara ya siku 10 ya Rais Samia kwa nchi za Ulaya inatajwa kuwa na mafanikio zaidi kwa Tanzania kwani ilisaidia kupatikana kwa fedha za msaada Euro milioni 450 sawa na Sh1.17 trilioni ambazo zilizuiliwa.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii, kufungua fursa za biashara na uwekezaji pamoja na kukuza uhusiano wa kidiplomasia.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwenye picha ya pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden mara baada ya kuwasili Ikulu ya Marekani Jijini Washington DC Desemba 14, 2022. Kulia ni Jill Biden Mke wa Rais wa Marekani Joe Biden. Pichal Ikulu
Mabadiliko ya wakuu wa mikoa
Julai 28, mwaka 2022 kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu yalitangazwa mabadiliko ya wakuu wa mikoa nchini ambapo wakuu wa mikoa wapya tisa waliteuliwa, saba walihamishwa vituo huku 10 wakiendelea na vituo vyao.
Hayo yanakuwa mabadiliko ya pili kwa Rais Samia kuyafanya tangu alipoingia madarakani ukiachana na yale aliyofanya Mei 2021.
Rais Samia aliwatema wakuu wa mikoa tisa akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Binilith Mahenge na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti
Kilichozua gumzo katika mabadiliko ya pili ni kurejea kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Albert Chalamila ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wakuu wa mikoa wanawake na kufikia wanane kati ya 26 wa Tanzania Bara.
Chalamila alitoa kauli tata wakati akiwakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Samia Mkoani Mwanza ambayo wengi walihisi ndio sababu ya kutenguliwa kwake mwaka jana.
Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa walioteuliwa Agosti 1, 2022, Ikulu jijini Dar es salaam alisema licha ya uchapakazi wake Chalamila si mtulivu wa akili hivyo ataendelea kumfuatilia kwa jicho la karibu.
“Wewe ni mfanyakazi mzuri lakini mtundu mno nilikuacha nje kipindi hicho nimeamua kukurudisha, naomba ukakue, ukue akili itulie uende ukafanye kazi unisaidie eneo ulilopangiwa, nakuangalia kwa ukaribu sana,” alisema Rais.
Waziri wa Tamisemi Angela Kairuki (kulia), Waziri wa Ulinzi Innoctent (Bashungwa katikati) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Pindi Chana wakila viapo vya kutumikia nyadhifa zao mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Pichal Ikulu
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan tayari ameshafanya mabadiliko mara tano kwenye Baraza la Mawaziri huku matatu yakifanyika mwaka 2022.
Januari 8, 2022 yalifanyika mabadiliko ya kwanza kwa mwaka 2022 yakiwa ni ya tatu tangu Rais Samia aingie madarakani ambapo ziliundwa wizara mpya pamoja na mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri.
Wizara ya Uwekezaji iliyokuwa chini ya Waziri Mkuu iliunganishwa pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo sasa inaitwa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara.
Mabadiliko hayo pia yalihusisha kuundwa kwa wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii ambayo ilitolewa kutoka Wizara ya Afya, ambayo inaongozwa na Dk Dorothy Gwajima.
Mawaziri walioachwa katika mabadiliko hayo ni William Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Palamagamba Kabudi aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Wengine ni Prof Kitila Mkumbo aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na na Geofrey Mwambe aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji.
Machi 31, 2022 Rais Samia alifanya mabadiliko mengine madogo kwenye Baraza ma Mawaziri ambapo alimhamisha George Simbachawene kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.
Dk Damas Ndumbaro aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii alihamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria huku Balozi Pindi Chana akiteuliwa kuchukua nafasi ya Ndumbaro.
Mabadiliko ya tano ambayo huenda sio ya mwisho katika Baraza la Mawaziri yalitangazwa Oktoba 2 mwaka huu ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula alitenguliwa.
Nafasi hiyo ilichukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Dk Stergomena Tax, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Innocent Bashungwa aliyehamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Waziri mpya aliyeingia katika mabadiliko hayo ni Angellah Kairuki ambaye alichukua nafasi ya Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Tamisemi.
Soma zaidi:
- Mfumo wa ‘mali kauli’ unavyowaumiza wanawake sokoni Tanzania
- Deni la Serikali lazidi kupaa, Tanzania ikisisitiza kuendelea kuchukua mikopo
- Ndugai na deni la Taifa: Nimekosa mimi, nimekosa sana
Freeman Mbowe atoka gerezani
Siku ya Ijumaa Machi 4, 2022, huenda ikawa miongoni mwa siku ambazo hazitasahaulika kwa wapenzi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe mara baada ya mwenyekiti wao kuachiliwa huru.
Mbowe na wenzie watatu walikuwa mahabusu kwa tuhuma kadhaa ikiwemo ya kula njama za kupanga kufanya na kufadhili ugaidi, ambapo alikaa mahabusu kwa muda wa siku 216 sawa na miezi nane tangu alipo kamatwa Julai 21 mwaka 2021 akiwa jijini Mwanza.
Wafuasi wa chama hicho waliofurika kwa wingi mahakamani hapo, mbali ya kuonyesha hisia za furaha walikosoa namna kiongozi wao alivyotumbukia kwenye kesi hiyo.
Saa chache mara baada ya Mbowe kuachiwa alialikwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam ambapo alinukuliwa akisema miongoni mwa waliyozungumza ni pamoja na kuwa na maridhiano.
Siku 16 baada ya kuachiwa akiwa mkoani Iringa, Mbowe aliutangazia umma kuwa Chadema hakitashiriki mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, TCD uliopangwa kufanyika Machi 30 na 31 mjini Dodoma.
Mbowe alisema kuwa Chadema haijashirikishwa kwenye masuala yaliyopo kwenye ripoti ya TCD ambayo inaamini imeweka kando kipaumbele muhimu cha suala la katiba mpya.
Pia alisisitiza chama chake kuendelea na ajenda ya Katiba Mpya na kutafuta maridhiano ya kitaifa kuelekea katika ujenzi wa demokrasia bora na yenye uhuru nchini.
Saa chache mara baada ya Mbowe kuachiwa alialikwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam ambapo alinukuliwa akisema miongoni mwa waliyozungumza ni pamoja na kuwa na maridhiano. Picha | Ikulu.
Polepole atenguliwa ubunge, ateuliwa kuwa balozi
Machi 15 mwaka 2022, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole aliapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 14.
Polepole ambaye alikuwa Mbunge baada kutenguliwa kama Katibu mwenezi wa CCM alizua gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akikosoa baadhi ya mambo katika Serikali.
Kupitia kipindi chake alichokiita Shule ya Uongozi alikuwa akizungumza mambo mbalimbali kuhusu Serikali na CCM ambacho hata hivyo kilifungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA ).
Disemba 11 Polepole alikutana na waandishi wa habari na kudai kuwa ameitwa na (TCRA) kuhojiwa juu ya maudhui ya “Shule ya Uongozi’” anayoyarusha kupitia mtandao wa ‘Youtube’ na kuwashambulia baadhi ya watu aliowaita ni ‘wahuni’ wasiojali masilahi ya Taifa.
Miongoni mwa makada wa CCM akiwemo Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo alisema Polepole hamheshimu Rais Samia hivyo Kamati ya Maadili inayoongozwa imuite na kumhoji.
Tulia Ackson alipokuwa akiapa kuwa Spika wa bunge la Tanzania mara baada ya kuibuka mshindi katika kiti hicho kwa kupata kura zote 376. Pichal Bunge
Dk Tulia Ackson achaguliwa kuwa Spika wa Bunge
Zikiwa zimepita siku 25 tangu Tanzania iandike historia ya kujiuzulu kwa spika wake kwa mara ya kwanza, historia nyingine ya kumpata Spika wa sita wa Bunge la Tanzania akiwa mwanamke wa pili kuongoza bunge hilo mara baada ya Anna Makinda iliandikwa.
Dk Tulia Ackson ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini alichaguliwa kuwa spika kwa kupata kura zote 376 za wabunge waliohudhuria katika uchaguzi uliofanyika Februari 1, bungeni Jijini Dodoma.
Alichukua nafasi hiyo baada ya mtangulizi wake Job Ndugai kujiuzulu baada shinikizo la watu kutokana na kauli alizotoa kuhusu Tanzania kukopa pesa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Tanzania sasa ina viongozi wawili wanawake wanaoongoza mihimili ya dola (Serikali na Bunge).
Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Tulia wameingia madarakani baada ya matukio mawili makubwa kutokea la kifo cha Hayati Rais John Magufuli mwaka 2021 na kujiuzulu kwa Ndugai mwaka huu.
Kuingia kwao katika ngazi za juu za uongozi kumekuwa na mjadala mpana huku baadhi ya watu wakisema hiyo ni dalili njema kwa Tanzania kuelekea 50 kwa 50 katika uongozi.
Tangazo
Kujiuzulu kwa Spika Job Ndugai
“Naomba kutoa taarifa kwa umma wa Watanzania kuwa leo Tarehe 06 Januari 2022 nimeandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…., “
Ndivyo yalivyosomeka baadhi ya maneno katika barua yake ya kujiuzuru baada ya kupata mashinikizo ya kujiuzuru wadhifa wa Uspika wa bunge la Tanzania kutoka kwa viongozi wa wa kisiasa wakiwemo wabunge.
Shinikizo hilo lilitokana na kile kilichotafsiriwa na wengi kama kubeza juhudi za Rais wa Tanzania baada ya kauli ya Ndugai kuhusu Serikali kuchukua mikopo ya maendeleo.
Disemba 28 alipokuwa katika Mkutano wa kimila wa kabila la wagogo Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa alitetea uamuzi wa bunge kupitisha tozo za miamala ya simu kuliko Serikali kuendelea kukopa.
“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya ku-run nchi (kuongoza nchi) hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii” alihoji Ndugai
Mara baada ya kauli hiyo uliibuka mjadala mkubwa nchini Tanzania uliofuatiwa na kauli za baadhi ya wanasiasa wakimtaka Ndugai ajiuzulu akiwemo Josephat Gwajima ambaye ni Mbunge wa Kawe.
Licha ya Ndugai kutoa ufafanuzi wa kauli yake Januari 3 mwaka 2022 bado juhudi zake hazikutuliza hali ya hewa na akaamua kuachia kiti na kusababisha kuahirishwa vikao vya Kamati za Bunge ambavyo vilipangwa kuanza wiki moja tu mbele.
Wewe unakumbuka tukio gani katika siasa za Tanzania ambalo unafikiri unaweza kutushirikisha? Tufuatile katika mitandao yetu ya kijamii ya Twitter, FaceBook kwa @NuktaTanzania na @nuktatz Instagram.