Wadau wa habari watoa neno kufungiwa kwa Jamii Forum, wanahabari kukamatwa
- wasema vitendo hivyo ni uvunjifu wa haki za kikatiba na kidemokrasia.
Arusha. Wadau mbalimbali wa habari Tanzania wamepaza sauti kufuatia kufungiwa kwa jukwaa la habari mtandaoni Jamii Forum pamoja na kukamatwa kwa waandishi wa habari wawili jijini Arusha.
Wadau hao ni pamoja na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Taasisi ya waandishi wa habari inayosaidia jamii za pembezoni (MAIPAC),Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Klabu ya Waandishi wa Habari Arusha (APC), na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tanzania (MISA–TAN).
Wengine ni Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) na Kikundi Kazi cha Utawala wa Mtandao Tanzania (IGTWG) kwa pamoja wamekea vitendo hivyo wavitaja kuwa ni ni ukiukwaji wa katiba ya Tanzania na kikwazo cha demokrasia hususani kuelekea uchaguzi mkuu.
“Uamuzi huu unaashiria ukiukwaji mkubwa wa haki ya msingi ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza na kupata habari kama ilivyohakikishwa chini ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, ambayo inasema kila mtu ana haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza habari, imesema taarifa ya Ernest Sungura, Mwenyekiti wa CoRI ikirejea uamuzi wa Jamii Forum kufungiwa.
Agosti 6 mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilisitisha leseni ya kuchapisha maudhui mtandaoni ya kampuni ya Vapper Tech Limited (JamiiForums) na kuzuia upatikanaji wa jukwaa la Jamii Forums kwa siku 90.
Kwa mujibu wa Jamii Forum uamuzi wa TCRA umetokana na wao kuchapisha taarifa ya mwanasiasa Humphrey Polepole kuhusu mfanyabiashara Rostam kumiliki mgodi wa makaa ya mawe kwa asilimia 70 na taarifa za uhusiano kati ya Rais wa Tanzania na mfanyabiashara raia wa Zimbabwe Wicknell Chivayo bila kuzingatia mizania.
Kutokana na uamuzi huo wadau wa haki wameitaka Serikali kukifungualia chombo hicho na kuondoa vikwazo vyote katika vyombo vya habari vya mtandaoni.
“Tunatoa wito kwa TCRA kuondoa mara moja zuio hilo na kurejesha fursa kwa umma kwenye JamiiForums, ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kutumia haki yao ya kutafuta, kupokea na kusambaza habari bila vikwazo visivyostahili.
…CoRI inasisitiza kwamba vikwazo visivyo na uwiano kwenye majukwaa kama vile JamiiForums vinadhoofisha kanuni za kidemokrasia, haki ya umma ya kupata habari, na imani katika utawala. Hatua za kurekebisha mara moja ni muhimu ili kudumisha uhuru wa kujieleza na kupata habari nchini Tanzania., imesema taarifa ya CoRI.
Tukio lingine lilokemewa na wadau wa habari ni Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwashikilia waandishi wawili wa habari ambao ni Ezekiel Mollel wa Manara TV na Baraka Lukas wa Jambo Tv kwa kosa la kuendesha chaneli zo binafsi biila kusajiliwa.
Hata hivyo, wadau hao wa habari wamebainisha kuwa tangu kukamatwa kwao, waandishi hao wawili wamenyimwa dhamana kinyume na Katiba ya Jamhuri yaTanzania na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
“Kwa hivyo sisi tunadai upatikanaji wa haraka wa uwakilishi wa kisheria kwa wanahabari wawili, Ezekiel Mollel na Baraka Lucas, kudai kuachiliwa kwao mara moja kwa dhamana kwa mujibu wa sheria, imesema taarifa ya THRDC iliyotolewa Septemba 7 mwaka huu.
Latest



