Tanzania yazidi kuunadi uwindaji wa kitalii kimataifa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro (katikati) akiwa pamoja na ujumbe aliombatana nao kutoka Tanzania wakiwa kwenye picha ya pamoja na mmiliki wa Kampuni ya uwindaji wa Kitalii ya Michel Mantheakis Safaris Ltd, Michel Mantheakis (wa tatu kulia) ambaye ni mmiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini Tanzania, ikiwa ni miongoni mwa Makampuni nane kutoka Tanzania yaliyoshiriki katika mkutano wa 50 wa mwaka wa Uwindaji wa Kitalii (Annual Hunting Convention) ulioanza rasmi leo katika Jiji la Las Vegas, Nevada nchini Marekani. Picha| Wizara ya Maliasili na Utalii.
- Makampuni zaidi ya nane kutoka Tanzania kuitangaza nchi kiutalii Marekani.
- Yashiriki mkutano wa 50 wa mwaka wa uwindaji wa kitalii nchini Marekani.
- Yavutia wawekezaji katika sekta hiyo na wageni kuja kwa wingi nchini.
Dar Es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro ametoa pongezi kwa makampuni zaidi ya nane ya Tanzania yaliyopo nchini Marekani kwa kazi nzuri ya kutangaza sekta ya uwindaji wa kitalii kwa kushiriki katika mkutano wa masuala ya uwindaji wa kitalii.
Mkutano huo wa 50 wa mwaka wa Uwindaji wa Kitalii (Annual Hunting Convention) ulioandaliwa na shirika la Safari Club International (SCI) umeanza leo na unafanyika katika Jiji la Las Vegas, Nevada nchini Marekani
Dk Ndumbaro amesema maonyesho hayo yanatoa fursa kwa Tanzania yakiwemo makampuni, viongozi na maofisa wa Serikali walioshiriki mkutano huo kujifunza na kuinadi Tanzania katika masuala ya uwindaji wa kitalii katika nyanja za kimataifa
“Katika maonyesho haya zaidi ya makampuni 200 yanayofanya biashara ya windaji wa kitalii kutoka kila kona ya dunia yapo hapa ikiwemo kutoka bara la Ulaya, Amerika, Afrika, lakini pia nchi za Canada na Marekani yenyewe,” amesema Dk Ndumbaro.
Amesema pia maonyesho hayo yanatoa fursa kwa nchi kujifunza sekta ya uwindaji wa kitalii kuwa ipo wapi hasa kipindi hiki cha ugonjwa wa Uviko-19.
“Mimi kama Waziri mwenye dhamana na utalii najisikia fahari kuona makampuni zaidi ya nane ya Kitanzania yapo hapa yakiiuza Tanzania kwenye sekta ya uwindaji wa kitalii.
“Huu ni ushahidi tosha kuwa makampuni hayo yanafanya vizuri, na yanakubalika kimataifa lakini pia tumechukua fursa hii ya kuweza kukutana nao kwa ujumla wake, mmoja mmoja kuweza kuzungumza nao na kubadilishana mawazo,’’ amesema Ndumbaro.
Amesema mkutano huo pia umewafundisha kuanza kuitazama sekta ya uwindaji wa kitalii kwa namna ya tofauti ili kuiwezesha kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa.
Soma zaidi:
- Mbinu zilizotumika kukomesha ujangili wa tembo Rufiji
- Botswana yapoteza zaidi ya tembo 300 ndani ya miezi mitatu
- Maajabu ya visiwa 11 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Rubondo
Mmoja wa wanaoendesha biashara ya utalii wa uwindaji nchini Tanzania ambaye yupo kwenye mkutano huo, Michael Mantheakis amesema kuwa mikutano kama hiyo ni muhimu kuhudhuria kwani inawakutanisha na wageni mbalimbali na bila kuhudhuria unakosa fursa muhimu za wateja.
“Hapa kuna Washiriki wa kutoka nchi zote za Afrika hivyo usipohudhuria mkutano huu utakosa soko. Hapa ndipo tunapokutana na wageni wetu tunapata faida ya kuweza kuendesha safari zetu, wateja na mawakala wanapata fursa ya kutufanyia usahili na pia wanaona jinsi tunayonadi bidhaa zetu,” amesema Mantheakis.
Mkutano huo umeanza rasmi Januari 19, 2022 na kufunguliwa rasmi Januari 21, 2022 jijini Las Vegas, Nevada nchini Marekani ukiwa na lengo la kuwakutanisha watunga sera na wafanya maamuzi katika ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali duniani kujadili masuala ya kisera katika kuendeleza sekta ya uwindaji.
Katika mkutano huo, Ndumbaro anazinadi fursa za uwekezaji katika uwindaji wa kitalii zilizopo nchini kwa lengo la kuwawezesha matajiri wakubwa duniani kuchangamkia uwekezaji huo uliopo nchini Tanzania
Kupitia Mkutano huo, Tanzania itaweza kuongeza uelewa zaidi katika masuala ya kisera na maamuzi katika kuendeleza sekta ya uwindaji wa kitalii nchini.
Latest