Tanzania yaongeza kodi pombe, sigara za kielektroniki

June 12, 2025 6:43 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Serikali kupendekeza kutoza kodi asilimia 30 kwenye vifaa na vimiminika vya sigara za kielektroniki.
  • Lengo ni kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizo na kuongeza wigo wa kodi kwa Taifa.

Dar es salaam. Serikali imependekeza kuongeza kodi kwenye bidhaa za pombe zinazoingizwa kutoka nje na sigara za kielektroniki kwa lengo la kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizo na kuongeza wigo wa kodi.

Serikali inalenga kutoza ushuru wa asilimia 30 kwenye vifaa vya sigara za kielektroniki vinavyotambulika kwa HS Code 8543.90.00 na vimiminika vya sigara za kielektroniki vinavyotambulika kwa HS Code 2404.12.00, hatua itakayopeleka maumivu kwa watumiaji wa bidhaa hizo nchini.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amelieleza Bunge wakati akiwasilisha Makadirio na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2025/2026 kuwa uamuzi huo unatarajiwa kuongeza Sh3.322 bilioni kwenye pato la Serikali

Pombe na sigara ni miongoni mwa bidhaa ambazo hulengwa na Serikali katika kuongeza mapato ya Serikali ili kufanikisha kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo.  Picha | Wizara ya Fedha Tanzania.

Kwa upande wa pombe, Dk Nchemba amesema Serikali imependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji hivyo vinavyo ingizwa kutoka nje.

Kwa mujibu wa Waziri Nchemba ongezeko hilo ni Sh20 kwa lita kwa upande kwa bia zinazotambulika kwa Heading 22.03., Sh30 kwa lita kwa mvinyo unaotambulika kwa Heading 22.04, 22.05, na 22.06 pamoja na Sh50 kwa lita kwa pombe kali na vinywaji vingine vinavyotambulika kwa Heading 22.08.

Kuongezeka kwa kodi kwenye bidhaa hizo, iwapo Bunge litaridhia na kupitisha bajeti hiyo, huenda kukawafanya watumiaji wa bidhaa hizo kutoboa zaidi mifuko yao ili kuzinunua. 

Hatua hii ambayo ni moja ya mikakati ya uanzishwaji wa vyanzo vya mapato kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi na kugaramia Bima ya Afya kwa wote.

Pombe na sigara ni miongoni mwa bidhaa ambazo hulengwa na Serikali katika kuongeza mapato ya Serikali ili kufanikisha kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks