Serikali kuongeza ushuru bidhaa za gesi asilia, kusamehe kodi
- Itaoongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye gesi asilia kutoka shilingi 0.45 kwa kila futi za ujazo (cubic feet) hadi shilingi 0.55 kwa kila futi za ujazo.
- Itasamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye gesi asilia inayouzwa kwenda kwenye vituo vya kushindilia gesi kwa ajili ya matumizi ya magari.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inapendekeza kuongeza ushuru kwenye bidhaa za gesi na kusamehe baadhi ya kodi ili kuchochea matumizi ya nishati mbadala, kukuza uchumi na kupunguza gharama za maisha.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26 leo Juni 12, 2025 bungeni jijini Dodoma amesema anapendekeza kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye gesi asilia kutoka shilingi 0.45 kwa kila futi za ujazo (cubic feet) hadi shilingi 0.55 kwa kila futi za ujazo.
“Lengo la hatua hii ni kulinda thamani ya fedha kwa kuwa kiwango cha sasa hakijabadilishwa kwa takriban miaka 8 na hakiendani na hali ya uchumi katika kipindi hicho. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh14.92 bilioni,” amesema Dk Mwigulu.
Pia Serikali inapendekeza kutoza ushuru kwa kiwango cha Sh22,000 (takriban dola za Marekani 8) kwa kila tani ya hewa ukaa inayozalishwa kwenye makaa ya mawe na gesi asilia.

Hatua hii itasaidia kudhibiti athari za kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati hizi pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh374.15 bilioni.
Waziri Nchemba amependekeza pia kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye gesi asilia inayouzwa kwenda kwenye vituo vya kushindilia gesi (Compressed Natural Gas Stations) kwa ajili ya matumizi ya magari.
“Lengo la hatua hii ni kuweka unafuu kwa wawekezaji, kuvutia uwekezaji wa vituo vya 83 kusambazia gesi asilia iliyosindikwa kwenye magari na kupunguza utegemezi wa mafuta na uzalishaji wa hewa ya uka,” amesema waziri huyo.
Kwa mujibu wa waziri huyo Serikali itaendelea na maandalizi ya kutekeleza mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa 40 kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) na kutekeleza shughuli za utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati vya Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi – Wembere na 4/1B na 4/1C.
Pia itaendelea kusambaza gesi asilia katika taasisi, viwandani, majumbani na kuimarisha matumizi ya Compressed Natural Gas (CNG) katika vyombo vya moto.

“Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ambapo Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan ni Champion wa jambo hili la kihistoria. Serikali iliandaa na inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) kwa lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema.
Hatua hizo zitapunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambao husababisha uharibifu wa misitu na athari za kiafya kutokana na moshi unaotokana na nishati hizo.
Latest



