Ahueni Vs maumivu zaidi: Bei ya mahindi yazidi kushuka Tanzania
- Hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa mavuno na changamoto za masoko.
- Pia bei zao hilo la chakula imeshuka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia mwezi Machi 2021.
- Serikali yawatafutia wakulima masoko nje ya nchi.
Dar es Salaam. Matumaini ya kupanda bei ya mahindi katika siku za hivi karibuni huenda yakazidi kupungua miongoni mwa wakulima nchini Tanzania, baada ya bei ya zao hilo kuendelea kushuka kwa miezi minne mfululizo tangu Desemba mwaka jana.
Pia bei zao hilo la chakula imeshuka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia mwezi Machi 2021.
Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Aprili 2021 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa wastani wa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 kwa mwezi Machi 2021 ilikuwa Sh47,963 ikiwa imeshuka kutoka Sh51,450 iliyorekodiwa Februari mwaka huu.
Hiyo ni sawa anguko la asilimia 6.7 au wakulima wamepoteza Sh3,486 kwa kila gunia moja ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Kushuka kwa bei hiyo ya mahindi mwezi Machi siyo bahati mbaya kwa sababu bei hiyo imekuwa ikishuka mfululizo tangu Desemba mwaka jana.
Ripoti hiyo ambayo inatolewa kila mwezi na BOT inaonyesha kuwa mwezi Novemba gunia la kilo 100 lilikuwa linauzwa kwa Sh58,012 ambapo bei ikashuka hadi Sh56,892 mwezi uliofuata kabla haijashuka kabisha hadi Sh47,963 mwezi Machi mwaka huu.

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.
Hata wakati, bei ya mahindi ikishuka miezi minne mfululizo, pia ripoti hiyo inaeleza kuwa wastani wa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Machi 2021 imeshuka hadi Sh47,963 kutoka Sh64,452 iliyorekodiwa Machi 2020.
Hilo ni sawa na kuwa wakulima wamepoteza Sh16,489 kwa kila gunia la kilo 100 ndani ya mwaka mmoja, jambo linalowapunguzia faida ambayo wangepata endapo wangeuza kwa bei ya juu au sawa na ile waliouza Machi 2020.
“Kushuka kwa bei hiyo kunaashiria hali nzuri ya uwepo wa chakula nchini,” imesema BoT katika ripoti hiyo.
Hata hivyo, bei za mahindi ndani ya mwaka mmoja uliopita zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji.
Kushuka kwa bei hiyo ya mahindi kunawanufaisha zaidi wanunuzi hasa walaji kwa kuwa hawalazimiki kutoboa zaidi mifuko yao kupata chakula hicho muhimu na utengenezaji wa bidhaa viwandani.
Zinahusiana:
- Kigoma kinara usajili wa mashamba Tanzania bara
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki
Mikakati ya Serikali kuwasaidia wakulima
Wakati wakulima wakilalamikia uwepo wa hifadhi kubwa ya mahindi katika maghala yao kwa sababu ya kukosa masoko, Serikali imesema imeweka mikakati mbalimbali kutatua changamoto hiyo ikiwemo kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa ili yanunue mahindi hayo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Mei 3, 2021 alisema wanafanya mazungumzo na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambao wameonyesha nia ya kununua mahindi zaidi ya tani 150,000 za mahindi.
Bashe, aliyekuwa akitolea ufafanuzi suala la wingi wa mahindi bungeni, siku hiyo alisema kwa sasa wanatoa vibali bure kwa wafanyabiashara waliopata masoko nje ya nchi ili wauze mahindi ya Tanzania.
“Nitumie nafasi hii kuziomba halmashauri zisizuie mahindi, mpunga, mchele unaouzwa popote nje ya mipaka yetu kwa sababu kufanya hivyo itakuwa kutokumtendea haki mkulima,” alisisitiza Bashe bungeni jijini Dodoma.
Pia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Kenya huenda ikaleta neema kwa wakulima na wafanyabiashara wa mahindi, baada ya Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta kutoa wiki mbili kwa watendaji wa Serikali yake kumaliza mgogoro wa mahindi ya Tanzania yaliyokwama katika mpaka wa Namanga jijini Arusha.
Machi mwaka huu, mahindi ya Tanzania yalizuiliwa kuingia nchini Kenya ambako ni soko kubwa la zao hilo kwa kilichodaiwa kuwa yana sumu kuvu ambayo ina madhara kiafya na hivyo kuwaacha wafanyabiashara wengi katika njia panda ya masoko.
Latest