Vilio, vicheko bei ya mahindi ikipaa Tanzania
- Bei ya jumla ya gunia la mahindi imepanda mara mbili ndani ya mwaka mmoja hadi Sh84,739 Novemba 2019 kutoka Sh42,362 iliyorekodiwa Novemba 2018.
- Itawafaidisha wakulima wa zao hilo na kuwaumiza watumiaji.
- Bei ya mazao mengine ya chakula ikiwemo mchele, maharage na mtama nayo imepanda katika kipindi hicho.
Dar es Salaam. Bei ya jumla ya gunia la mahindi imepanda mara mbili ndani ya mwaka mmoja hadi Sh84,739 Novemba 2019 kutoka Sh42,362 iliyorekodiwa Novemba 2018 ikiwa ni fursa kwa wakulima na maumivu kwa watumiaji.
Ripoti ya Tathmini ya Uchumi ya mwezi Desemba 2019 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inaeleza kuwa tangu Novemba mwaka juzi bei ya jumla ya gunia la mahindi la kilo 100 imekuwa ikipanda mfululizo.
Mathalan, Septemba 2018 gunia hilo la mahindi liliuzwa kwa Sh71,046 na mwezi uliofuata likauzwa kwa Sh80,967 kabla ya kupanda zaidi tena mwezi Novemba mwaka jana.
Kupanda kwa bei ya mahindi, ni kicheko kwa wakulima ambao wamewekeza nguvu zao kulima zao hilo la chakula ili kujipatia kipato kwa ajili ya familia zao.
Lakini upande wa pili, ni maumivu kwa watumiaji wa zao hilo, kwani bei ikipanda wanalazimika kutoboa mifuko yao zaidi ili kununua zao hilo ambalo hustawi karibu katika mikoa yote ya Tanzania.
Ripoti hiyo, inaeleza kuwa bei ya mazao mengine ya nafaka ukiwemo mchele, maharage, mtama nayo imepanda katika kipindi hicho.
Hata hivyo, bei ya jumla ya gunia moja la viazi mviringo imeshuka kutoka Sh88,209.2 Novemba mwaka juzi hadi Sh70,560.7 Novemba 2019.