Ahueni kwa wakulima bei ya mahindi ikipanda kidogo Tanzania
- Imepanda hadi Sh57,105 Desemba 2021 kutoka Sh56,892 ya Desemba 2020.
- Bei ya mazao mengine ya chakula yashuka mwezi Desemba 2021.
Dar es Salaam. Wakulima na wafanyabiashara huenda wakaendelea kunufaika na kilimo cha mahindi, baada ya bei ya zao hilo kupanda kidogo kwa Sh213 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, huku ikiiacha maumivu kwa wanunuzi wa chakula nchini Tanzania.
Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Januari 2022 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka unaoishia Desemba 2021 ilikuwa Sh57,105 ikipanda kutoka Sh56,892 iliyorekodiwa kipindi kama hicho 2020.
Bei iliyotumika Desemba ni sawa ongezeko la Sh213 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kupanda kwa bei ya mahindi kutawafaidisha zaidi wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo ili kujipatia kipato cha kuendesha familia.
Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele na ulezi.
BoT katika ripoti hiyo imeeleza kuwa tangu Septemba 2021 bei ya mahindi imekuwa ikipanda mfululizo kwa miezi minne.

Mathalan, mwezi Septemba 2021, bei ya jumla ya zao hilo linalotegemewa na kaya nyingi ilikuwa Sh44,365 ikapanda mwezi uliofuata hadi S48,11 na ilipofika Novemba ikiwa Sh49,683.
Kupanda kwa bei ya mahindi kunaweza kuwa kumechangiwa na juhudi za Serikali kuwatafutia wakulima masoko ya zao hilo ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba mwezi uliopita aliliomba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP), kununua shehena ya nafaka kutoka kwa wakulima hapa nchini kwa ajili ya matumizi yake ya kulisha wakimbizi maeneo mbalimbali wanayoyahudumia.
Katika kuimarisha soko la nafaka nje ya nchi, Serikali ya Tanzania imejenga vituo viwili vya kuhifadhia nafaka katika jiji la la Juba (Sudan Kusini) na Lumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC).
Pia Serikali inaendelea kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) na imefungua milango kwa wakulima kuuza mahindi nje ya nchi.
Soma zaidi:
Akiba ya chakula yaongezeka
Wakati bei za mazao makuu ya chakula zikipanda, akiba ya chakula katika ghala la (NFRA imeongezeka katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa akiba ya chakula ya NFRA imeongezeka hadi tani 214,968 mwezi Desemba 2021 kutoka tani 209,057 mwezi Novemba mwaka jana.
Kiwango hicho cha chakula kwa mwezi Desemba ndiyo cha juu zaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akiba hiyo inajumuisha mazao yakiwemo mahindi, mtama na mpunga ambapo BoT inaeleza kuwa ongezeko la akiba ya chakula limetokana na ununuzi uliofanywa na NFRA katika msimu wa mavuno.
Mwenendo wa uhifadhi wa chakula katika ghala hilo ambalo huifadhi chakula kwa ajili ya dharura kama njaa umekuwa wa kupanda na kushuka katika miaka mitano iliyopita.
Latest