Tanzania yafungua anga, kuanza kupokea ndege za kimataifa
- Ndege za watalii na kibiashara zitaruhusiwa kutua nchini.
- Hatua hiyo inakuja baada ya anga hilo kufungwa zaidi ya mwezi mmoja kuepuka maambukizi ya Corona.
- Ndege za Air Tanzania zatakiwa kurejesha safari zake.
Dar es Salaam. Tanzania imefungua rasmi anga lake ili kuruhusu ndege za kimataifa za watalii na kibiashara kutua nchini baada ya Serikali kusema kuna mwenendo mzuri wa ugonjwa wa virusi vya Corona.
Aprili 11, Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ilizuia ndege za abiria za kimataifa kutua nchini ikiwa ni hatua ya kuilinda nchi dhidi ya maambukizi mapya ya virusi hivyo. Ndege za mizigo pekee ndiyo ziliruhusiwa kuingia nchini lakini kwa wahudumu wa ndege hiyo kujiweka karantini kwa gharama zao.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa sasa anga la Tanzania limeshafunguliwa leo na ni fursa kwa ndege za nchi nyingine kuingia nchini bila kipingamizi.
Amesema TCAA inatakiwa kuanza maandalizi ya kuweka mambo sawa katika viwanja vyake ili kupokea ndege ambazo zitaanza kuingia nchini zikiwa na abiria.
“Tunaposema leo (tumefungua anga) ili waanze kujiandaa, taarifa kamili zitatoka leo au kesho asubuhi kulingana na sheria ya ICAO (Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga),” amesema Mhandisi Kamwelwe na kuwataka maandalizi yaanze mapema.
“Kwenye viwanja vya ndege waanze kujiandaa kufanya mazoezi ya kupokea ndege na kutoa kipaumbele kwa upimaji wa watu ambao watakuwa wanaingia nchini,” ameongeza.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
Aidha, ameliagiza Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kujipanga na kuanza kurejesha huduma za ndege katika nchi ambazo lilikuwa linatoa huduma hasa zile ambazo zimefungua anga zao.
Ndege imekuwa ni usafiri unaotegemewa na abiria wa kimataifa kusafiri kutoka nchi moja na nyingine kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za biashara na utalii kutokana na kuchukua muda mfupi kusafiri umbali mrefu.
Rais John Magufuli jana akiwa Chato mkoani Geita aliagiza watalii kutoka nje ya nchi waruhusiwe kuingia nchini na kwenda kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa sababu wagonjwa wa Corona wamepungua.
Alisema wakifika nchini hawatalazimika kukaa karantini kwa siku 14 bali watapimwa joto na ikibainika hawana dalili za corona waruhusiwe kwenda kutazama wanyama.
Utalii ni moja ya sekta ambazo zimeathirika zaidi na athari za COVID-19 huku wizara ya maliasili na utalii ikitarajia kuwa idadi ya watalii nchini itashuka mara nne zaidi ya matarajio ya mwaka huu.