ATCL ilivyojitanua kimataifa

January 12, 2019 3:21 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Inafufua safari za ndani katika mikoa ya  Mtwara, Ruvuma, Mpanda na Pemba ili kupata abiria na mizigo inayosafirishwa nje ya nchi.
  • Inakusudia kuzifikia nchi za Kusini mwa Afrika hivyo kuongeza ushindani kwa mashirika ya Kenya Airways na Ethiopia Airways. 
  • Imepewa changamoto ya kusimamia vizuri  ndege za Serikali ikishindwa itanyang’anywa.

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)  linaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya miundo mbinu na kuongeza idadi ya safari zake ili kufaidika na soko la ndani na nje ya nchi katika usafiri wa anga. 

Katika  kipindi hichi ambacho Serikali imenunua ndege mpya na kupelekea  kuongezaka kwa  ushindani baina ya  mashirika ya  Precision Air na Fastjet ambayo imesimamisha safari zake zote kwa sababu ya changamoto za uongozi na madeni. 

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi aliweka wazi maboresho hayo jana (Januari 11, 201) wakati wa mapokezi ya ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyonunuliwa na Serikali na kufanya ndege zilizonunuliwa na kukabidhiwa kwa ATCL kufikia sita. 

Matindi amesema katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (2017/2022) wanakusudia  mwaka 2019 kufufua safari za ndani hasa katika mikoa ya Iringa, Mtwara na Ruvuma sambamba na kuwa na ratiba ya uhakika katika maeneo hayo.

“Upanuzi wa mtandao wetu wa safari za ndani unatazamiwa kutekelezwa kwa haraka zaidi huku kipaumbele kwa mwaka 2019 kufuatana na mpango mkakati wa miaka mitano ni kurudisha safari za Mtwara na Songea mara tu ukarabati mkubwa wa uwanja wa Songea utakapokamilika.

“Kuanza safari kati ya Iringa na Dar es Salaam mara tu ukarabati wa uwanja wa Nduli kukamilika na kuanza safari za Mpanda na Pemba. Suala la kurudisha safari za Mtwara tunalifungamanisha na kukamilika kwa ukarabati wa uwanja wa Songea,” amesema Matidi. 

 Ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyonunuliwa na Serikali ilipotua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kufanya ndege zilizonunuliwa na kukabidhiwa kwa ATCL kufikia sita. Picha| Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali.

Katika hatua nyingine, amesema maboresho ya  huduma za ndani shirika lina kusudia  kuvutia abiria wanaosafirisha mizigo kwa njia ya ndege ambapo msisitizo umewekwa katika kubeba mizigo ya kibiashara.

Amebainisha kuwa uwezo wa kubeba mizigo kwa ndege zilizopo ni takribani tani 90.6 ikijumuisha ndege mpya aina ya Airbus A220-300 yenye uwezo wa kubeba tani 19 kila moja. 

“Uwezo wetu wa kubeba mzigo ni fursa kuhakikisha biashara yetu inakuwa endelevu. Tayari tumefanikiwa makubaliano ya usafirishaji wa nyama ya mbuzi inayouzwa nje ya nchi kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na mashirika mengine,” amesema.

Sambamba na hilo wameanza mazungumzo ya awali ya uuzaji wa mbogamboga nje ya nchi ili zisafirishwe kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuachana na utaratibu wa kutumia nchi za jirani ikiwemo Kenya. 


Zinazohusiana: 


Suala lingine la kimkakati ni uendelezaji wa miundombinu ya utoaji wa huduma baada ya ATCL kurudishwa katika mfumo wa uuzaji wa tiketi duniani unaoratibiwa na Shirika la mashirika ya ndege duniani (ICAO).

Hatua hiyo itawezesha upanuzi wa awamu ya pili ya safari za Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, China, Thailand na India. 

“Tunatazamia pia kutoa huduma za ndege kwa saa 24 kupitia kituo chetu cha ‘Call Center kinachoendelea kufanyiwa ukarabati,” amesema Matindi. 

Ikiwa shirika hilo litafanikiwa kujiimarisha litaongeza ushindani kwa mashirika mengine ya nje ikiwemo Kenya Airways na Ethiopia Airway ambayo yanatawala soko la usafiri wa anga Afrika. 

Katika kuliongezea nguvu shirika hilo, Rais John Magufuli ameagiza ndege mbili za Serikali zipakwe rangi ya ATCL ili ziwe zinabeba abiria kipindi ambacho hazibebi viongozi ili kukuza wigo wa mapato na fursa za utalii nchini. 

Hata hivyo, ametoa angalizo kuwa ikiwa ATCL watashindwa kuzisimamia na kuziendesha ndege zilizonunuliwa na Serikali watanyang’anywa na kupewa mashirika mengine kama Precision Air. 

Enable Notifications OK No thanks