Tahadhari: Kimbunga Jobo pwani ya Lindi, Mtwara
- Kimbunga hicho kiko kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
- Kinaweza kusababisha ongezeko la upepo na mawimbi katika bahari ya Hindi hususan mikoa ya Mtwara na Lindi.
- Wananchi watakiwa kuzingatia tahadhari ya upepo na mawimbi.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka watumiaji wa bahari ya Hindi katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuchukua tahadhari kutokana kuwepo kwa kimbunga Jobo kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar ambacho kinaweza kusababisha kuongezeka kwa kasi ya upepo na mawimbi ya bahari hiyo.
TMA katika taarifa yake iliyotolewa jana usiku Aprili 21, 2021 imesema kumejitokeza mgandamizo mdogo wa hewa ambao umefikia kiwango cha kimbunga hafifu kwa jina Jobo.
Kimbunga hicho kipo kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar katika Bahari ya Hindi umbali wa Kilometa 930 na kilometa 1030 kutoka pwani ya Lindi na Mtwara.
“Uwepo wa kimbunga hicho unatarajiwa kusababisha ongezeko la upepo na mawimbi katika bahari ya Hindi hususan katika Pwani ya mwambao wa mikoa ya Mtwara na Lindi,” imeeleza taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo inaendelea kufuatiliia mwenendo na mwelekeo wa kimbunga Jobo kwa kuzingatia mifumo mingine ya hali ya hewa iliyo jirani zaidi na kimbunga hicho ambayo inaweza kubadili nguvu na mwelekeo wa kimbunga Jobo katika wakati ujao.
“Wananchi waendelee kuzingatia tahadhari ya upepo na mawimbi iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika maeneo husika. Mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi,” imeeleza taarifa hiyo.
Soma zaidi:
- Kimbunga Kenneth kuikumba Mtwara, Lindi
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Taarifa muhimu ya muendelezo wa Kimbunga Kenneth Tanzania
Hali ilivyo leo
TMA imesema kimbunga Jobo kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya Tanzania ambapo leo usiku wa kuamkia Machi 23, 2021 ambapo kinatarajiwa kuwa umbali wa takriban kilomita 410 kutoka pwani ya mkoa wa Lindi.
Hata hivyo, kimbunga Jobo kinatarajiwa kupungua nguvu yake kadri kinavyosogea katika pwani ya Tanzania.
Aidha, izingatiwe kuwa uwepo wa kimbunga Jobo unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya ongezeko la mvua na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa Pwani.
“Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,” imesema TMA katika taarifa yake iliyotolewa leo Aprili 22.
Mwaka 2019, mamlaka hiyo iliripoti uwepo wa kimbunga Keneth katika eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagascar kilichoambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo.
Hata hivyo, kimbunga hicho hakikufika katika mikoa ya Lindi, Mtwara ambayo iko ufukweni mwa bahari ya Lindi.
Taarifa hii imeboreshwa leo Aprili 22, 2021
Latest
