Taarifa muhimu ya muendelezo wa kimbunga Kenneth Tanzania

Mwandishi Wetu 0518Hrs   Aprili 25, 2019 Habari
  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka mamlaka na wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kuchukua tahadhari ya kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kwa sababu kimbunga hicho kimejiimarisha.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kuchukua tahadhari ya kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kutokana na kimbunga Kenneth kuongeza nguvu katika pwani ya Mtwara. 

                     

Kutokana na mwenendo wa kimbunga hicho, shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu zinaweza kuathirika hasa katika mkoa wa Mtwara na maeneo ya jirani hasa Lindi na Mtwara kutoka umbali wa kilomita 500 kutoka eneo hilo. 

Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali, uharibifu wa mazao mashambani, miundombinu kutokana na mafuriko na upepo mkali, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi kifupi (storm surge).

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na itakuwa inatoa taarifa muhimu na nini mamlaka husika zinapaswa kufanya ili kuwalinda wananchi na mali zao.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi amesema kimbunga hicho kipo katika visiwa vya Comoro lakini hadi kufikia saa 9:00 mchana kitakuwa kinasogea pwani ya Mtwara na kitakuwa na kasi ya kilomita 140 kw saa.

         


Mamlaka zilivyojipanga

Kutokana na utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu kutokea kwa Kimbunga hicho na mvua kubwa Aprili 25, 2019 kitakachoathiri maeneo ya pwani ya Kusini mwa nchi na kusababisha madhara mbalimbali. 

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linawataka  wananchi wote waishio katika maeneo hatarishi, maeneo yaliyopo pembezoni mwa bahari na kandokando ya mito, kuchukua tahadhari katika kipindi hiki kwa kuyahama maeneo hayo haraka.


"Wananchi wanatahadharishwa kuchukua tahadhari katika kipindi hiki na kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka Hali ya Hewa Tanzania na kusikiliza vyombo vya habari pamoja na kuzingatia tahadhari zinazotolewa, ushauri na miongozo ya kitaalam ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza," imeeleza taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Operesheni wa jeshi hilo, Billy Mwakatage.

Amesema wananchi waepuke kukaa au kuegesha vyombo vya Usafiri na Usafirishaji chini ya miti mikubwa, maana matawi au mti vyaweza kuangukia chombo na kusababisha uharibifu mkubwa wa Mali hata kudhuru Maisha.


Kutokana na Kimbunga hiki kikali kinachoambatana na mvua kubwa kuna uwezekano wa mawe makubwa au udongo kuporomoka kutoka milimani au miti kuanguka na kuziba barabara, hivyo madereva wanapaswa kuwa makini kwa kuendesha vyombo kwa mwendo unaokubalika ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Kwa upande wake, chama cha msalaba mwekundu Tanzania (Red Cross) kimeandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wafanyakazi wake wa kujitolea wako tayari kutoa msaada ikiwa maafa yatajitokeza katika maeneo yaliyotajwa.




Related Post