Kimbunga Kenneth kuikumba Mtwara, Lindi

Daniel Samson 0717Hrs   Aprili 24, 2019 Habari
  • Kimbunga hicho kitajiimarisha zaidi katika ukanda wa pwani ya Mtwara ambapo kinaweza kutatiza shughuli zinazofanyika katika fukwe na usafirishaji wa anga na majini. 
  • Kimbunga hicho kinaambatana na mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari
  • Wananchi wametakiwa kufuatilia kwa ukaribu tahadhari inayotolewa na TMA kila mara ili kuchukua hatua.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wanaotumia fukwe za bahari ya Hindi kuchukua tahadhari ya kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kutokana na kimbunga Kenneth kuongeza nguvu katika pwani ya Mtwara. 

Kimbunga hicho kinatarajiwa kufika pwani ya kusini ya Tanzania na kaskazini mwa msumbiji kuanzia usiku wa Alhamisi (Aprili 25, 2019) ambapo katika kipindi cha saa 24 zilizopita kimejiimarisha kwa kiwango cha kimbunga kamili. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Pascal Wanita aliyekuwa akitoa ufafanuzi wa kina kuhusu kimbunga hicho leo (Aprili 24, 2019) amesema mifumo ya hewa inaonesha kimbunga Keneth kilichopo eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo.

“Kimbunga hicho kinaendelea kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, hivyo kusababisha ongezeko la mvua zinazoambatana na ngurumo za radi pamoja na upepo mkali kadri kinavyokaribia maeneo ya ukanda wa pwani,” amesema Dk Wanita. 

Kwa mujibu wa TMA, mpaka mchana wa leo (Jumatano) kimbunga hicho kipo kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kina kasi ya kilomita 130 kwa saa ambapo hadi kufikia usiku wa leo, Aprili 24 kimbunga hicho kitakuwa kilomita 250 kutoka pwani ya Mtwara na kusafiri kwa kilomita 150 kwa saa.

Lakini kesho mchana (Aprili 25, 2019) kitaongeza nguvu ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.


Kutokana na mwenendo wa kimbunga hicho, shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu zinaweza kuathirika hasa katika mkoa wa Mtwara na maeneo ya jirani hasa Lindi na Mtwara kutoka umbali wa kilomita 500 kutoka eneo hilo. 

Dk Wanita amesema wavuvi na watu wanahusika na shughuli za utalii katika fukwe za bahari ya Hindi wanapaswa kuwa makini kwa sababu maeneo hayo yanaweza kukumbwa na mpepo mkali pamoja na mvua. 

“Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali, uharibifu wa mazao mashambani, miundombinu kutokana na mafuriko na upepo mkali, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi kifupi (storm surge),” ameeleza Dk Wanita.


Soma zaidi: 


Pia  Aprili 26 kunategemewa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo wananchi wanatakiw akuchukua tahadhari. 

TMA imesema  inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa kimbunga hicho kusini magharibi mwa bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo mingine ya hali ya hewa kwa ujumla na itaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

Related Post