TMA yatahadharisha upepo mkali katika mikoa 7

February 24, 2025 4:52 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema upepo huo unaweza kuathiri shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi na usafirishaji.

Arusha. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la hali mbaya ya hewa itakayosababisha upepo mkali katika mikoa saba inayopakana na bahari ya hindi ikiwemo Lindi, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa ya TMA iliyotolewa leo Februari 24, 2025, saa 9:30 mchana inafafanua kuwa hali hiyo mbaya ya hewa itadumu kwa siku tano ikitarajiwa kusababisha upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa.

“Athari zinazoweza kujitokeza: Kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi, uvuvi na usafirishaji baharini, zingatia na jiandae,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, TMA imebainisha kuwa uwezekano wa kutokea kwa hali mbaya hiyo ya hewa ni wa wastani huku athari nazo zikitarajiwa kuwa za wastani.

Pamoja na taarifa hiyo, TMA imesema Februari 27 na 28 hakuna tahadhari yoyote hivyo shughuli nyingine za kiuchumi katika pwani ya bahari ya hindi zinaweza kuendelea.

Huenda upepo huo ukapunguza hali ya joto kali iliyoikumba mikoa mbalimbali nchini ambayo kwa mujibu wa TMA imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua.

Katika taarifa iliyotolewa Februari 13 mwaka huu TMA imesema vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi huu wa Februari, 2025 hususan katika maeneo ambayo msimu wa mvua za vuli umeisha.

Hali hiyo inatarajiwa kupungua katika maeneo hayo mwezi Machi, 2025 hususan wakati ambapo mvua za msimu wa masika zitakapoanza.

“Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.” imesema taarifa ya TMA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks