Taasisi za fedha zatakiwa kutumia kigezo cha historia kuwapa mikopo wanawake

November 24, 2022 12:08 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Makamu wa Rais Philip Mpango atembelea banda la Umoja wa Benki Tanzania (TBA) katika ufunguzi rasmi wa wiki ya huduma za fedha kitaifa inayofanyika viwanja vya Rockcity Mall, Mwanza. Picha | TBA.


  • Ni kwa sababu wengi hawana umiliki wa mali.
  • Makamu wa Rais Dk Mpango azitaka kushusha riba kuvutia wanawake wengi.
  • Benki Kuu, TBA kuanza kukopesha kwa kutumia kitambulisho cha Nida.

Mwanza. Serikali imezitaka taasisi za fedha nchini Tanzania kuhakikisha zinaanza kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuhakikisha zinawafikia wananchi wengi hususan wakulima.

Pia zimetakiwa kutazama upya taratibu za udhamini ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kukopa hususani wajasiriamali wanawake ambao wengi hawakopesheki kutokana na kutokuwa na mali isiyohamishika ikiwemo nyumba.

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ametoa maagizo hayo wakati akizindua wiki ya huduma za kifedha iliyofanyika jijini Mwanza leo Novemba 24, 2022 na kueleza kuwa bado riba inawauzimiza wananchi na kushindwa kukopa.

Amesema mwitikio wa mabenki bado ni mdogo kuweza kuvutia wananchi wenye kipato cha chini na kati kuweza kukopa hivyo ni vyema wakalitazama jambo hilo ikiwemo suala la masharti ya mikopo.

Dk Mpango amesema jambo hilo limekuwa kikwazo hasa kutokana na mila za kitanzania kuwa wanawake walio wengi hawana umiliki wa mali hivyo watumie namna nzuri ya kutumia historia ili watu waweze kukopesheka.

“Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitoa rai kwa taasisi hizi za kifedha kupunguza riba ili kuwasaidia wananchi waweze kukopa ambapo kwa sasa wananchi wanakopeshwa kwa riba ya asilimia 9 pekee wakati wao wanaenda kukopa Benki Kuu  kwa asilimia 3 kwa nini wasipunguze na kuweka uwiano sawa angalau ifike asilimia 5?,” amehoji Dk Mpango huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kwenye maadhimisho hayo.

Mpango pia amesema bado kuna upungufu wa huduma za kibenki vijijini ambapo hadi sasa zimefika kwa asilimia 8 pekee na kuzitaka taasisi hizo kuhakikisha zinafikisha huduma hiyo ili kuwasaidia wananchi waweze kunufaika.

Amesema kwa muda mrefu mchango wa huduma za kifedha umekuwa chini ya asilimia 4, na kuitaka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Umoja wa Benki Tanzania (TBA), kufanya tafakuri ya kina kuhusu namna ya kuongeza ubunifu ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika jitihada za kupunguza umaskini na kuongeza maendeleo.


Soma zaidi: 


Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Fausta Ntara ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwakopesha wanawake kwa kuwa walio wengi hawana mali zisizohamishika.

Pia ameiomba serikali kukiangalia chama hicho na kukipatia fursa mbalimbali zinazopatikana serikalini ikiwemo ushonaji wa sare na vitu vingine kwa kuwa chama hicho kinao wataalamu wa mambo mbalimbali.

“’Mheshimiwa Makamu changamoto tunayokutana nayo wanawake wajasiriamali ni pamoja na kushindwa kukopa kwa kuwa moja ya masharti ya mikopo ni kuwa na mali isiyohamishika lakini pia gharama na muda wa mkopo umekuwa ukitolewa mfinyu kiasi cha kushindwa kufanya marejesho,” amesema Ntara.

Akizungumzia suala hilo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema benki hiyo kwa kushirikiana na TBA umeanza kufanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kulegeza masharti hayo ya mkopo.

Amesema baada ya Serikali kuanza kutoa vitambulisho vya Taifa (Nida) wanakusudia kuanza kuvitumia katika kuwakopesha wananchi.

“Tunaendelea kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya fedha lengo ni kuhakikisha inaboresha utolewaji wa huduma hiyo kwa wananchi,” amesema Prof Luoga.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV