Dk Mpango aagiza udhibiti mikopo haramu akizindua mfumo wa iCBS

July 30, 2025 4:26 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema wakopeshaji hao wanahatarisha usalama wa taarifa binafsi za wananchi na kuendeleza mzunguko wa umaskini.

Dar es Salaam .Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, ametoa agizo kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na taasisi nyingine husika kudhibiti kwa haraka wakopeshaji haramu wanaotoa mikopo bila kufuata sheria, akisisitiza umuhimu wa kulinda wananchi dhidi ya ulaghai wa kifedha unaoendelea kushamiri kupitia majukwaa ya kidijitali.

Akizungumza leo Julai 30, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS), Dk Mpango amesema wakopeshaji hao si tu wanavunja sheria, bali pia wanahatarisha usalama wa taarifa binafsi za wananchi na kuendeleza mzunguko wa umaskini kwa riba kandamizi zisizodhibitiwa.

“Limeibuka wimbi la wakopeshaji wa mitandao ya simu. Wapo wengine wanajiita yako mkopo, pesa yako,  pesa mkopo na kadhalika. 

Hawa licha ya kutotambuliwa kisheria wanaendesha shughuli hizo bila kufuata taratibu za ukopeshaji,” amesema Dk Mpango.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa, badala ya kukopa bila mpango, wananchi wapewe elimu ya fedha ili kuepuka mikopo inayowaumiza, na kutumia fursa za mikopo halali kama ile inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba katika picha akiwa katika ziara Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, uliopo jijini Lilongwe. Picha/ BoT.

Agizo hili linaunga mkono kauli ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, ambaye awali alionya kuhusu mikopo yenye riba kubwa na mikakati ya kuwakandamiza wakopaji.

Nchemba aliyekuwa akizindua Jukwaa la kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 alisema taasisi hizo zimekuwa zikiwaumiza wananchi kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa pamoja na kupanga njama za kuwafilisi wale ambao wanajua wazi hawatoweza kulipa mikopo hiyo.

Katika hotuba yake, Dk Mpango pia ameagiza usimamizi madhubuti wa mfumo wa iCBS na mifumo mingine ya malipo, akiwataka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na wizara zinazohusika kuhakikisha ulinzi wa mifumo hiyo dhidi ya uhalifu wa kimtandao. 

Aidha, ameihimiza BoT kuongeza kasi ya matumizi ya malipo ya kidijitali na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu.

“Ninasisitiza BoT kuchukua tahadhari zote katika kuulinda na kuhami mfumo huu na mifumo mingine ya malipo dhidi ya uhalifu wa kimtandao,” ameeleza Dk Mpango.

Hata hivyo, Makamu wa Rais ameihimiza BoT na wadau wengine kuendeleza ubunifu wa ndani, kuongeza bajeti ya utafiti, kuanzisha vituo vya ubunifu na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu na Serikali.

“Baada ya kuunda mfumo wa iCBS, Afrika na dunia nzima inatutazama. Tumethibitisha kile ambacho tunaweza kukifanya hata zaidi ya wengine,” amesisitiza Makamu wa Rais.

Dk Mpango pia ameitaka BoT kushirikiana na wizara na taasisi za miliki bunifu kuhakikisha ulinzi wa hakimiliki ya mfumo wa iCBS, pamoja na kuhamasisha usomaji wa mifumo ya taasisi zote za Serikali ili iweze kushirikiana na iCBS.

Aidha, ameagiza taarifa za papo kwa papo kutumika kwenye maamuzi ya Serikali kupitia mfumo wa kitaifa wa takwimu, na kuhamasisha matumizi ya makumbusho na maktaba za kidijitali kama chanzo cha maarifa kwa wanafunzi, watafiti na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema kwa kutumia wataalamu wa ndani, utekelezaji wa mfumo huo umetumia Sh10.63 bilioni pekee badala ya Sh91.9 bilioni endapo ungenunuliwa kutoka nje, na hivyo Serikali kuokoa Sh81 bilioni.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV