Taasisi nyingine nne zawasilisha gawio la Sh2.75 bilioni kwa Serikali

November 26, 2019 12:02 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Watendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Picha|Maelezo.


  • Hiyo ni baada ya Rais John Magufuli kutoa siku 60 kwa taasisi 187 kuwasilisha gawio serikalini.
  • Taasisi zilizowasilisha gawio leo ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Reli (TRC), na taasisi ya fedha ya Self Microfinance Fund.
  • Waziri Mpango azionya taasisi ambazo bado hazijawasilisha gawio.

Dar es Sal​aam. Siku moja baada ya Rais John Mgufuli kutoa siku 60 kwa taasisi na mashirika kuwasilisha gawio serikalini, taasisi nne kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zimetekeleza agizo hilo leo.

Rais Magufuli jana alizitaka taasisi, mashirika ya umma 187 ambayo hayajatoa gawio au mchango kwa Serikali, yafanye hivyo katika muda uliowekwa kabla hatua hazijachukuliwa.

Taasisi zingine zilizotekeleza wito wa Rais ni pamoja na Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Reli (TRC), na taasisi ya fedha ya Self Microfinance Fund ambapo zote kwa pamoja zimewasilisha Sh2.75 bilioni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyekuwa akizungumza wakati wa kupokea gawio hilo leo (Novemba 26, 2019) jijini Dodoma, amesema kuwa baada ya agizo la Rais alilolitoa jana, hakutakuwa na mzaha kwa taasisi, kampuni na mashirika ambayo hayatatekeleza agizo hilo ndani ya siku 59 zilizobaki.

“Nitasimamia kikamilifu agizo hili la Mheshimiwa Rais, itakapofika siku ya 60 nitatembeza panga bila uoga wala kupepesa macho kwa taasisi, kampuni na mashirika ambayo hayatakuwa yametekeleza agizo hili, hatutanii katika hili,” amesema Waziri Mpango.


Soma zaidi: 


Aidha, Waziri Mpango amezishukuru taasisi hizo kwa kutekeleza agizo la Rais na kuongeza kuwa angependa kuona mashirika yaliyobaki yakitekeleza agizo hilo kwa wakati, kwa kuwa fedha hizo siyo zake wala za Rais bali ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa faida ya Watanzania wote.

Naye, Msajili wa Hazina, Athumani Mbutuka amesema kuwa ametekeleza agizo la Rais Magufuli la kumtaka kuzijulisha taasisi, kampuni na mashirika 187 ambayo hayakuwa yametoa gawio na michango kufanya hivyo ndani ya siku 60.

Rais Magufuli jana alipokea gawio na michango kutoka kwa taasisi, kampuni na mashirika 79 ambayo yalitoa jumla ya Sh1.05 trilioni.

Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Nyingine ni Wakala wa Huduma za Misitu na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambayo yalikabidhiwa cheti kwa kufanya vizuri. 

Aidha, TPA iliyotoa gawio la Sh169 bilioni na TPC (Sh14 bilioni) yalipewa tuzo kwa kutoa gawio kubwa zaidi. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW