Mwigulu: Wataalamu wizara ya fedha wanashughulikia malalamiko ya tozo
- Ni baada ya malalamiko ya tozo kuongezeka huku wananchi wakieleza kuwa zinaendelea kuongeza ukali wa maisha.
- Rais Samia ataka malalamiko hayo yafanyiwe kazi.
- Waziri Nchemba aahidi kufanyia marekebisho baadhi ya sheria za kodi.
Dar es Salaam. Baada ya kuwepo malalamiko lukuki juu ya gharama kubwa za tozo katika miamala ya kielektroniki nchini, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema wameanza kufanyia kazi maelekezo ya viongozi wa juu na maoni ya wananchi ili kuleta unafuu.
Kwa zaidi ya miezi miwili sasa kumekuwa na ongezeko la malalamiko juu ya makato makubwa ya tozo kwenye miamala ya simu na huduma za kibenki tangu kuanzishwa kwake Julai 2021 jambo ambalo limeongeza ukali wa maisha.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Nchemba amesema wizara yake imepokea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi (CCM) kushughulikia malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu gharama za tozo za miamala ya kielektroniki ili kuleta unafuu kwa wananchi.
Waziri huyo, ambaye amekuwa akikosolewa vikali juu ya tozo hizo, amesema wataalamu wa wizara yake wanafanyia kazi maelekezo na maoni hayo na si muda mrefu wataleta majawabu baada ya kufanyia “marekebisho kadhaa ili kuleta unafuu.” Hata hivyo, hakuweka bayana aina ya marekebisho watakayofanya.
“Serikali imepokea maoni ya Watanzania wakati wa kutekeleza nia hii njema ya Serikali kwa wananchi wake na kwa hiyo baada ya kupokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuyazingatia maoni ya wananchi yanayoendelea kutolewa, tunalifanyia kazi suala hilo na punde tutaleta majawabu,” amesema Dk Nchemba.
Kwa mujibu wa utafiti wa Sauti za Wananchi kuhusu Uchumi na Tozo uliofanywa na Shirika la Twaweza zaidi ya nusu ya watu au asilimia 57 ya wananchi walioshiriki kwenye utafiti huo hawakubaliani na tozo zilizowekwa kwenye huduma za fedha kwa njia za simu.
Sababu za tozo zatajwa
Waziri Nchemba aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi ya kutembelea mpaka wa Tanzania na Kenya katika mji wa Sirari Wilayani Tarime mkoani Mara Septemba 12, 2022, amesema Serikali inahitaji fedha kuendelea na miradi mbalimbali na kwamba kuna baadhi ya mambo hayawezi kusimama.
Soma zaidi:
Waziri huyo amesema baadhi ya miradi na matumizi ya Serikali hayawezi kusimama kwa kukosa fedha ikiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere unaogharimu zaidi ya Sh 6 trilioni na ruzuku za mafuta ili kupunguza makali ya maisha kutokana na mfumuko wa bei.
‘Wananchi ungeni mkono Serikali’
Waziri Nchemba amewaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kushiriki katika maendeleo ya taifa lao kwa kulipa kodi kwa hiari na kuwafichua wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Wafichueni wafanyabiashara wanaofanya magendo na kuikosesha Serikali mapato na hivyo kuathiri mwenendo wa uchumi kwa kuleta ushindani usio sawa,” amesema Waziri Nchemba.
Aidha waziri Nchemba ameahidi kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali za kodi zinazokwaza ukuaji wa biashara nchini ili kuifanya sekta hiyo ya biashara iweze kukua, kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Latest