Simu kinara kumilikiwa na wakulima Tanzania

August 18, 2021 2:11 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Asilimia 81.5 ya kaya hizo zinamiliki simu za mkononi.
  • Mali zingine zinazomilikiwa kwa wingi ni tochi, vifaa vya sola na baiskeli.
  • Vifaa hivyo huwasaidia kuwasiliana na usafirishaji wa mazao.

Dar es Salaam. Kama bado unajiuliza ni mali ipi inaongoza kwa kumilikiwa na kaya zinazojihusisha na kilimo Tanzania, basi fahamu kuwa simu ndiyo baba lao katika jamii za watu hao. 

Kaya zinazojihusisha na kilimo huusisha kaya za wakulima, wafugaji na wafugaji wa samaki kwenye mabwawa ambazo hutegemea shughuli hizo kuendesha maisha.

Kwa mujibu ripoti ya Sensa ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2019/20 iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kaya hizo ziko milioni 12 ambapo asilimia 65 ya kaya hizo zinajihusisha na kilimo cha mazao.

Kati ya kaya hizo, milioni 11.6 ziko Tanzania Bara ambapo hujumuisha wakulima wadogo na wakubwa. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kaya hiyo zinamiliki mali mbalimbali zikiwemo zisizohamishika na zinazohamishika lakini simu ndiyo mali/kifaa kinachoongoza kumilikiwa na kaya hizo ambazo nyingi hupatikana maeneo ya vijijini.

Kaya milioni 6.4 zinazojihusisha na kilimo ndiyo zinamiliki simu sawa na asilimia 81.5 za kaya zinazotegemea kilimo Tanzania. Hiyo ni sawa na kusema kaya nane kati ya 10 zinamiliki simu. 

Takriban kaya nane kati kaya 10 za wakulima, wafugaji na wafugaji wa samaki kwenye mabwawa zinamiliki simu za mkononi. Picha| Ars technica.

Bidhaa iliyofuata kwa kumilikiwa zaidi ni tochi ambayo inamilikiwa na kaya milioni 6.8 au sawa na asilimia 63.3 ya kaya zinazojihusisha na kilimo.

Kwa wafugaji na wakulima, tochi hutumika kwa ajili ya kuangaza mwanga maeneo ya nyumbani nyakati za usiku na katika sehemu za kulaza mifugo hasa kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na nishati ya umeme.

Mali nyingine maarufu miongoni mwa kaya hizo ni redio za kawaida na zinazotumia mikanda almaarufu kama kaseti. Bidhaa hiyo inamilikiwa na watu milioni 3.7 sawa na asilimia 47.8.

Baada ya tochi, vifaa vya umemejua vinafuata kwa asilimia 45.8 na baisikeli kwa asilimia 41.8.

Umemejua umekuwa mkombozi kwa kaya za vijijini na hata mjini ambazo bado hazijafikiwa na gridi ya Taifa hivyo kutumia kwa ajili ya mwanga, kuendesha mitambo ya uzalishaji ikiwemo mashine za kusaga nafaka na kukamua mafuta.

Umeme huo ambao ni miongoni mwa nishati safi na salama umefungua fursa ya watu kujiajiri na kujiingizia kipato. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya hali ya upatikanaji wa nishati Tanzania bara ya mwaka 2016 iliyotolewa na NBS pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), asilimia 24.7 ya nyumba zote Tanzania bara, zinatumia umeme wa sola. 

Mkulima wa mahindi, maharage na karanga huko Sengerema mkoani  Mwanza, Suzana Kasmili amesema kwa vijijini, baiskeli ni chombo muhimu cha usafiri licha ya kuwa kuna pikipiki na bajaj.

“Baiskeli huwa tunatumia kwenda mashineni kusaga unga na kukoboa mchele pia kwa wenye mashamba ya mbali na nyumbani,  baiskeli huwasaidia kuwahi mashambani asubuhi,” amesema Kasimili.


Wakati bidhaa hizo zikiongoza kumilikiwa miongoni mwaka kaya zinazojihusisha na kilimo, vifaa ambavyo zina wamiliki wachache ni pamoja na bajaji  kwa asilimia 0.4), simu za mezani (asilimia 0.6) na majenereta kwa asilimia 1.2.

Kwa upande wa majenereta, Susana amesema wanaomiliki ni wale wanaoonyesha televisheni kibiashara kwani kumiliki kwa matumizi binafsi, jenereta lina gharama za mafuta ambazo wakulima wengi hawapendelei kuziingia.

Simu kuongoza kumilikiwa na kaya hiyo inaweza kuwa inachangiwa na ukweli kuwa kifaa hicho kinarahishamawasiliano baina ya watu na hivyo kaya haziwezi kukosa kuwanacho. 

Kwa kutumia simu hulazimiki kutembea umbali mrefu kuwasiliana, jambo linalosaidia kuokoa muda ambao unatumika katika shughuli za uzalishaji.

Mtaalamu wa sayansi ya kompyuta na intelijensia bandia (Artificial intelligence), Innocent Msangi amesema umiliki wa simu vijijii unajipatia umaarufu kwani watu wa mjini wanawaambukiza wa vijijini matumizi ya teknolojia hiyo.

Msangi amesema taarifa nyingi zinatoka mjini kwenda vijijini na hivyo ili wazipate taarifa hizo kwa wakati, inabidi watumie simu na hapo  ndipo teknolojia hiyo inaposhika  kasi vijijini.

“Teknolojia inakua na sasa pesa zinatumwa kwa njia ya simu na wanahitaji pesa ili kuendeleza kazi zao pia. Haiwezekani katika dunia ya sasa tuanze kutuma pesa kwa njia ya posta. Simu ni rahisi na haraka,” amesema Msangi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW