Rais Samia awapatanisha wafugaji na wakulima Morogoro

August 3, 2024 2:14 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Awataka kuishi kwa kuheshimiana na kushirikiana akiwaunganisha mikono ili kuanza upya. 
  • Asisitiza kila upande kutambua haki za jamii nyingine na kwamba wote ni muhimu kwa taifa.

Dar es Salaam. Katika jitihada za kumaliza uhasama wa muda mrefu baina ya wafugaji na wakulima mkoani Morogoro, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepatanisha pande hizo mbili zinazosigana akiwataka kumaliza tofauti zao kwa kuwa kila jamii ni muhimu kwa taifa.

Kwa muda mrefu jamii hizo mbili zimekuwa katika migogoro ya kudumu inayohusisha aidha kuwania ardhi kwa ajili ya kilimo na malisho au wafugaji kulisha mifugo yao katika mazao ya wakulima ambapo kila upande umekuwa ukiushutumu upande mwingine kukiuka sheria na taratibu.

Uwepo wa migogoro hiyo umechangia athari mbalimbali ikiwemo ukosefu wa amani katika jamii, vifo, majeruhi pamoja na hasara ya mazao na mifugo jambo linalorudisha nyuma jitihada za kujikwamua kiuchumi.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya “Tutunzane” inayolenga kumaliza migogoro kati ya jamii hizo mbili leo Agosti 3, 2024 Mvomero mkoani Morogoro amewataka wafugaji na wakulima nchini kuishi kwa kutegemeana, kuheshimiana na kushirikiana.

“Mlime, wanaolima na mfuge, wanaofuga, na kwamba tunategemeana wote. Ninyi ndio mnaotupa sisi uhai, mnatupa vitoweo mnatupa na chakula, hakuna haja ya kugombana, hakuna haja ya kuuwana, wote ninyi ni wanadamu,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa.

Kabla ya kauli hiyo mjini Kilosa, Rais Samia aliwaita mbele wawakilishi wawili wa kila jamii na kuwataka kupeana mikono ikiwa ni ishara ya kumaliza tofauti zao na kukubaliana amani.

Watu wanne wakiwemo wanawake wawili na wanaume wawili walijitokeza na kisha aliwaamuru kunyanyua mikono na kuunganisha mikono kama ishara ya kupatana na kumaliza tofauti zao. 

Kilosa ni miongoni mwa maeneo korofi yenye migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji. 

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuheshimu haki ya mtu mwingine akiwataka wafugaji kutoingilia haki za wakulima na wakulima kutoingilia haki za wafugaji.

Kumalizwa kwa migogoro ya wafugaji na wakulima nchini Tanzania kunaweza kuimarisha amani baina ya jamii hizo na kukuza uchumi kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na mifugo au ufugaji. 

Hatua hiyo itasaidia kuongeza tija kwenye sekta hizo zinazotegemewa na mamilioni ya Watanzania kujiingizia kipato na kuchangia zaidi ya theluthi au asilimia 33 ya pato la Taifa.

Kwa mujibu wa Sensa ya Kilimo ya Mwaka 2019 iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kati ya kaya milioni 12 zilizopo Tanzania, theluthi mbili au kaya milioni 7.8 zinajihusisha na kilimo.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 65.3 ya kaya zote zilizopo nchini ambapo kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi cha mwaka 2020 kilichotolewa na NBS kilimo kilichangia asilimia 26.9 ya pato la Taifa.

Kwa upande wa wafugaji takwimu zinaonesha mwaka 2020 kulikuwa na jumla ya kaya milioni 1.1 zinazojihusisha na ufugaji nchini Tanzania ambapo mwaka 2023 sekta ya ufugaji imechangia asilimia 6.5 ya pato la taifa, na kuifanya kuwa moja ya sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...