Serikali yatoa mwelekeo mpya ujenzi nyumba za NHC
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Novemba 16, 2022 amezindua Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), hafla hiyo inafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JKICC). Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Yataka wabia wachunguzwe kabla ya kupewa kazi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
- Waziri Mkuu asema hiyo itasaidia ujenzi wa nyumba zenye viwango na kwa wakati.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha linachambua na kupata wawekezaji wenye uwezo wa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa miradi ya ubia ili kuharakisha ukuaji wa sekta ya nyumba nchini.
Amesema kuwa kupitia sera mpya ya ubia Serikali inatarajia kuona wawekezaji na shirika hilo wanajenga ubia imara utakaosaidia ukuaji wa sekta ya nyumba nchini ambayo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Novemba 16, 2022 wakati akizindua sera ya ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) amesema lengo la sera hiyo ni kuishirikisha sekta binafsi kuwekeza mitaji yake katika kujenga nyumba na majengo makubwa yenye tija kwa uchumi wa Taifa.
“Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika Sshughuli mbalimbali utaongeza kasi na kuwa chachu ya mabadiliko katika miji yetu, hivyo Serikali itashirikiana na wawekezaji kuondoa changamoto zitakazojitokeza ili azma ya kuwekeza mitaji katika sekta hiyo iweze kutimia,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema amefurahi kuona kuwa Shirika hilo limedhamiria kuishirikisha sekta binafsi katika kujenga nyumba za ghorofa katika maeneo inayoyamiliki ambayo ama yamepitwa na wakati ama yana viwanja ambavyo havijaendelezwa.
Tangu kuanza kwa sera ya ubia mwaka 2012 shirika hilo limeingia mikataba 194 na sekta binafsi ambapo mikataba 73 ilifutwa kwa sababu ya ukiukwaji wa masharti. Pia mikataba 111 yenye thamani ya Sh300 bilioni 300, utekelezaji wake umefanyika huku mikataba 81 yenye thamani ya Sh240 bilioni utekelezaji wake umekamilika.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2021 kuhusu mikopo ya ujenzi wa nyumba inaeleza kuwa mahitaji ya nyumba nchini yanakadiriwa kufikia nyumba 200,000 kila mwaka ambapo kuna upungufu wa nyumba milioni 3 za makazi ya watu hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam.
Mahitaji ya nyumba yanachochewa zaidi na ongezeko la idadi ya watu kila mwaka. Hali hiyo ndiyo inayoyafanya benki kutoa mikopo ili kujipatia faida wakati zikirahisisha maisha ya watu kwa kuwawezesha kupata makazi bora ya kuishi.
“Upungufu huo, unachangia wamiliki wa nyumba binafsi kutoza kodi kubwa na wakati mwingine kudai kodi ya mwaka mzima kwa mkupuo mmoja,” amesema Majaliwa akiitaka NHC kujenga nyumba nyingi ili kuwasaidia Watanzania.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula amesema kuwa maboresho ya sera ya ubia ya NHC yamelenga kuongeza ufanisi na tija kwa wabia wa shirika hilo.
Amesema shirika hilo litafanya uchambuzi wa kina ili kupata wawekezaji makini ambao watashiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali na kuhakikisha wanaopata fursa hiyo ni wale wenye uwezo wa kuridhisha wa kukamilisha miradi kwa wakati na viwango.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Nehemia Mchechu amesema kuwa sera hiyo imezingatia fursa za uchumi katika kipindi hiki, mafanikio na changamoto katika sera zilizopita.
“Sera hii pia itaongeza uwazi na mtu akitaka kuwezekeza kwenye miradi yetu isiwe lazima kumfahamu mtu yeyote ili uweze kupata fursa za miradi ya Shirika la Nyumba,” amesema Mchechu.
Latest