Rais Samia atoa vigezo wakazi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba

March 23, 2022 12:08 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Muonekano wa nyumba mpya 644 za makazi Magomeni Kota jijini Dar es Salaam zilizozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Machi 23, 2022. Picha| Jalilu Zaidi.


  • Wakazi hao ambao wameahidiwa kukaa bure kwa miaka mitano.
  • Wameruhusiwa kulipa gharama za ujenzi baada ya muda huo kuisha.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuruhusu wananchi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa mpangaji ununuzi.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Machi 23, 2022 wakati akizindua nyumba 644 za makazi za Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambazo ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh52 bilioni.

Wakazi hao ambao wameahidiwa kukaa bure kwa miaka mitano, wameruhusiwa kulipa gharama za ujenzi wa nyumba pekee bila ya gharama za ardhi na miundombinu ya jumuiya baada ya muda huo kuisha.

“Nimeridhia kuwa baada ya miaka mitano wananchi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa Mpangaji – Mnunuzi na kurejesha gharama za ujenzi wa nyumba pekee, hatutawatoza gharama ya ardhi kwa sababu tukifanya hivyo mtashindwa kuzinunua,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, wakazi wanaotaka kulipa gharama ya ununuzi kabla ya kufika miaka mitano wanaruhusiwa kulipa kidogo kidogo kwa kipindi cha miaka 10 bila ya riba yoyote.

Rais Samia amewasihi wakazi hao kutunza nyumba hizo na kuzingatia usafi wa ndani na nje na kuchangia huduma jumuishi kwa faida ya kila mmoja.

“Nyumba hizi ni nzuri na zimejengwa kisasa, tumefanya yote ambayo mmeomba hivyo na mimi ninawaomba matunzo ya nyumba hizi.

“Nataka mtengeneze Kamati ambazo zitasimamia usafi wa nyumba hizi, kivyovyote vile sitegemei watu watapikia kuni ndani ya nyumba hizi na badala yake tunategemea watu wapikie gesi,” amesisitiza Rais.


Soma zaidi: 


Aidha, Rais Samia ameziagiza Wakala wa ujenzi Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kampuni ya  Watumishi Housing Corperation (WHC) kukaa na sekta binafsi ili kukubaliana katika ujenzi wa makazi bora kwenye maeneo yanayopaswa kuendelezwa.  

Amesisitiza kuwa, “iliwahi kusema kwamba, popote ambapo Sekta binafsi wanaweza kuweka fedha, Serikali itajitahidi kutoa nafasi kwa sekta hizo na hivi sasa Sekta Binafsi wapo tayari kushirikiana na TBA kwa kujenga maeneo yote ambayo yanahitaji kujengwa.”

Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Oktoba 2016 katika lenye ukubwa wa ekari 32 ambapo zilizotumika sasa ni ekari tisa. Eneo hilo lina majengo ya kibiashara, michezo na mapumziko.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2016 kuhusu mikopo ya ujenzi wa nyumba  inaeleza kuwa mahitaji ya nyumba nchini yanakadiriwa kufikia nyumba 200,000 kila mwaka ambapo mpaka sasa kuna upungufu wa nyumba 3 milioni za makazi ya watu hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam. 

Mahitaji ya nyumba yanachochewa zaidi na ongezeko la idadi ya watu kila mwaka. Hali hiyo ndiyo inayoyafanya mashirika mashirika mbalimbali ya umma na binafsi kujitokeza kuchangamkia fursa ya kujenga nyumba za bei nafuu ambazo hupangishwa au kuuzwa kwa watu.

Enable Notifications OK No thanks