Mwigulu: Wananchi hawana uelewa kuhusu uhusiano wa kodi na maendeleo ya nchi

January 11, 2023 10:55 am · admin
Share
Tweet
Copy Link

Sehemu ya washiriki wa kongamano la kodi linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Picha | Esau Ng’umbi.


  • Wafanyabiashara watajwa kuwashawishi wateja kutolipa kodi.
  • Awataka Watanzania kufahamu kuwa kodi ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.

Dar es salaam. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema bado Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu uhusiano uliopo kati ya kodi na maendeleo na hivyo kusababisha kulegalega kwa ukusanyaji wa mapato nchini. 

Kauli hii ya Mwigulu inakuja zikiwa zimepita siku chache tu tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itangaze kukusanya makusanyo ya nusu ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa asilimia 99 huku mwezi Disemba ukivunja rekodi ya kukusanya mapato mengi zaidi yanayofikia Sh2.7 trilioni.

Mwigulu aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano la kodi kitaifa lililofanyika leo Januari 11,2022 jijini Dar es Salaam amewaambia wahudhuriaji kuwa hali hiyo inatokana na dhana kuwa kinachofanywa na TRA hakihusiani na maslahi ya Taifa.

“Ni vizuri Mtanzania yeyote akafahamu kuwa kila kitu anachokiita maendeleo kwenye nchi yake kinahusiana na kodi anayolipa, hata tukikopeshwa tunalipa kwa kutumia kodi na ili ukopeshwe unalipwa kwa kupimwa uwezo wako wa kukusanya,” amesema Dk Nchemba.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Kiwango cha ukusanyaji wa kodi kimeongezeka kutoka Sh1.2 trilioni Machi 2021 hadi Sh2.76 trilioni Disemba mwaka 2022.


Zinazohusiana 


Waziri Nchemba amesema kulegalega huko kunachochewa zaidi na  baadhi ya wafanyabiashara nchini Tanzania ambao wamekuwa wakiwashawishi wateja wao kutolipa kodi kwa  kuwauzia bidhaa zisizo na risiti za TRA.

“Unakuta mfanyabiashara anamuuliza mteja, nikupe bei yenye risiti ya TRA au isiyo na risiti, na kutokana na utofauti wa bei watu wengi huchagua risiti zizizo za TRA, na hapo anakuwa amemshawishi Mtanzania huyu kutolipa kodi,” amesema waziri huyo kwa msisitizo.

Watumishi wa Serikali wamo

Amewataka watumishi wa umma kutambua umuhimu wa kodi katika kukuza uchumi na kuacha kuwa chanzo cha kukwamisha ukusanyaji wa mapato hasa katika sekta binafsi ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania kwa sasa.

Kongamano hilo linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, limewakutanisha wadau mbalimbali wa kodi ikiwemo TRA, wawekezaji wa sekta binafsi, na watunga sera ili kupata maoni ya kuyafanyia kazi wakati wa kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha mwaka 2023/24.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW