Serikali ya Tanzania yapendekeza bajeti Sh56.49 trilioni 2025

June 12, 2025 8:25 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Yapanga kukopa Sh14.95 trilioni kutoka vyanzo vya ndani na nje kugharamia bajeti hiyo.
  • Sehemu kubwa inatarajia kugharamia mishahara, kulipa deni la Serikali, na miradi ya maendeleo.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inapendekeza kukusanya na kutumia Sh56.49 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh6.2 trilioni ndani ya mwaka mmoja huku sehemu kubwa ikitarajiwa kutumika katika miradi ya kimkakati na kulipa deni la taifa. 

Kiwango hicho cha bajeti ni sawa na ongezeko la asilimia 12.3 kutoka Sh50.29 trilioni kilichoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya mwaka wa fedha 2024/25 unaohitimishwa Juni mwaka huu. 

Matarajio hayo ya bajeti hiyo ya Serikali yapo chini kwa Sh550 bilioni kutoka katika kiwango cha Sh57.04 trilioni ambacho utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ulikuwa umetangaza Machi mwaka huu wakati inawasilisha mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka fedha wa 2025/26. 

Ili kufanikisha malengo ya mapato hayo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amewaambia wabunge kuwa Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani ya Sh40.47 trilioni, misaada Sh1.07 trilioni na mikopo yenye thamani ya Sh14.95 trilioni.  

“Kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni Sh32.31 trilioni, mapato yasiyo ya kodi Shi6.48 trilioni, na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sh1.68 trilioni,” amesema.

Kukopa zaidi soko la nje 

Katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 2025, Serikali inatarajia kukopa zaidi kutoka katika vyanzo vya fedha vya nje. Dk Nchemba amesema katika kiwango cha fedha wanachopendekeza kukopa kinajumuisha mikopo mikopo ya ndani ya Sh6.27 trilioni na Sh8.68 trilioni kutoka vyanzo vya nje. 

Serikali inatarajia kuwa bajeti hiyo ya mwisho katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Samia itatumika zaidi katika kulipa stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) Sh9.17 trilioni na ununuzi wa bidhaa na huduma Sh5.58 trilioni.

Pia fedha hizo zinatarajia kulipa riba za mikopo Sh6.49 trilioni na ruzuku (subsidies & transfers) kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa Sh22.17 trilioni. 

“Aidha, Serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 7.72 kugharamia malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje,” amesema Dk Nchemba ambaye alitumia hotuba yake kwa kiwango kikubwa kuipamba Serikali ya Rais Samia na Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwa imesalia miezi minne tu kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV