Deni la Serikali ya Tanzania lafikia Sh107.7 trilioni

June 12, 2025 5:52 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Laongezeka kwa asilimia 14.9 ikilinganishwa na Sh91.71 trilioni ya Machi 2024.
  • Ongezeko hilo limechangiwa na kupokelewa kwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
  • Serikali yasema deni himilivu na itaendelea kukopa.

Dar es Salaam. Deni la Serikali ya Tanzania limeongezeka kwa asilimia 14.9 hadi kufikia Sh107.70 trilioni Aprili 2025 kutokana na kupokelewa kwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Deni hilo limeongezeka kutoka Sh91.71 trilioni ya Machi 2024 au sawa na Sh15.99 trilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ameliambia Bunge leo Juni 12, 2025 kuwa kati ya deni hilo la Serikali, Sh72.94 trilioni au takriban theluthi mbili ni deni la nje huku deni la ndani likiwa ni Sh34.76 trilioni.

Awali Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo aliyekuwa akiwasilisha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 na Mpango wa Bajeti wa Serikali kwa mwaka 2025/26 alisema deni hilo limeongezeka kutokana na Serikali kupokea mikopo mipya kutoka vyanzo mbalimbali.

“Ongezeko la deni lilitokana na Serikali kuendelea kupokea mikopo mipya kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji,” amesema Prof Mkumbo Bungeni leo asubuhi. 

Deni bado ni himilivu

Dk Mwigulu aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka 2025/26 amesema tathmini iliyofanyika Oktoba 2024 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2024/25 thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55.

“Thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 23.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40 na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180,” amesema Dk Mwigulu.

Kwa nyakati tofauti kumekuwa na mjadala miongoni mwa wadau wa maendeleo nchini juu ya kuongezeka kwa kasi kwa deni hilo huku Serikali ikiendelea kusisitiza kuwa ni himilifu na inakopa kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya Watanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks