Sekta ya utalii: Nguzo muhimu kupambana na Uviko-19
Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha Wanyamapori Trust nchini Kenya. UNEP/Natalia Mroz.
- UN yasema ni chanzo cha ajira na kipato kwa mamilioni ya watu duniani.
- Yataka juhusu kuimarisha sekta hiyo kuwakwamua watu kiuchumi.
Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) umesema sekta ya utalii ni chanzo cha kipato na ajira kwa mamilioni ya watu na kuwa na ukiitumiwa vizuri inaweza kusaidia kupambana na majanga kama Uviko-19.
Kwa mujibu wa UN, nchi nyingi zikiwemo zenye maendeleo duni, mataifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea, nchi za Afrika na nchi za kipato cha kati “utalii ni chanzo kikuu cha uchumi, pato la nje, kodi na ajira.”
Na kwa sababu utalii unaunganisha watu na asili, Umoja wa Mataifa unasema utalii endelevu una uwezo wa kipekee wa kuchagiza jukumu la kulinda na kuhifadhi mazingira.
Umoja huo umeongeza kuwa “zahma yoyote inapoikumba sekta ya utalii basi inasambaratisha na kupindua maisha ya nchi na ya mamilioni ya watu mathalani lilipozuka janga la Uviko-19, utalii umekuwa moja ya sekta ambazo zimeathirika vibaya.”
Pigo kubwa limeshuhudiwa katika nchi za visiwa vidogo zinazoendelea ambako utalii unachangia zaidi ya asilimia 20 ya pato la taifa (GDP) na asilimia zaidi ya 30 ya palo la jumla la nje.
“Sekta ya utalii inasaidia ajira kwa mamilioni ya watu moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja hususani kwa wanawake na vijana na ndio maana mwaka 2020 takriban ajira milioni 120 za moja kwa moja kwenye sekta ya utalii zilikuwa hatarini kutokana na janga la Uviko-19,” imeeleza UN katika taarifa yake kuhusu mnepo wa sekta ya utalii Februari 17, 2023.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO) kuna habari njema kwani “mwaka huu wa 2023 utalii wa kimataifa unatarajiwa kuongezeka na kufikia asilimia 80 hadi 95 ya ilivyokuwa kabla ya janga la Uviko-19 kutegemeana na kiwango cha kudorora kwa uchumi, kujikwamua kwa safari za kimataifa Asia na Pasifiki na mwenendo wa vita ya Urusi dhidi ya Ukraine.”
Takwimu za UNWTO zinaonyesha kuwa mwaka jana 2022 zaidi ya watalii milioni 900 walisafiri kimataifa idadi ambayo ni mara mbili ya ilivyokuwa mwaka 2021.
Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa sekta ya utalii endelevu na wenye mnepo unachangia katika ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu kwa ukuzaji wa uchumi, kupunguza umasikini , kuzalisha ajira na kazi zenye staha kwa wote.
“Tunatoa wito kwa nchi wanachama kuunda mikakati ya kitaifa kwa kujikwamua baada ya majanga ikiwemo kupitia ushirikiano na sekta binafsi na kupanua wigo wa shughuli za sekta hiyo na bidhaa zake,” imeeleza UN.
Latest